Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. Mteremsho wa Kitabu hiki umetokana na Mwenyezi Mungu,
Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 1

2. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki.
Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu. 2

3. Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale
wanao wafanya wenginewe kuwa ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate
kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina
yao katika wanayo khitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye mwongo
kafiri. 3

4. Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana,
basi bila ya shaka angeli teua amtakaye katika alio waumba. Subhanahu,
Ametakasika na hayo! Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda atakalo. 4

5. Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Hufunika usiku juu
ya mchana, na hufunika mchana juu ya usiku. Na amefanya jua na mwezi vitumike.
Kila kimojapo kinakwenda kwa kipindi kilicho wekewa. Jueni mtanabahi! Yeye ndiye
Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe! 5

6. Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya
mwenziwe katika nafsi ile ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane.
Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu.
Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo
kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi? 6

7. Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi,
lakini hafurahii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala
mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi.
Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema
yaliyomo vifuani. 7

8. Na taabu inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi
naye ameelekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa
akimwitia zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia
yake. Sema: Starehe na ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa
miongoni mwa watu wa Motoni. 8

9. Je! Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na
kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi...Sema:
Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu
wenye akili. 9

10. Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu
Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi
Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu. 10

11. Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi
Mungu kwa kumsafishia Dini Yeye tu. 11

12. Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu. 12

13. Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya Siku Kubwa
nikimuasi Mola wangu Mlezi. 13

14. Sema: Mwenyezi Mungu tu namuabudu kwa kumsafishia
Yeye tu Dini yangu. 14

15. Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye.
Sema: Hakika walio khasirika ni wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku
ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo khasara iliyo dhaahiri. 15

16. Yatawekwa juu yao mat'abaka ya moto, na chini yao
mat'abaka. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawakhofisha waja wake. Enyi waja wangu!
Nicheni Mimi! 16

17. Na wale wanao jiepusha na ibada potovu, na wakarejea
kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu. 17

18. Ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao.
Hao ndio alio waongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili. 18

19. Je! Yule mwenye kustahiki hukumu ya adhabu, je, wewe
unaweza kumwokoa aliyomo katika Moto? 19

20. Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa
zilizo jengwa juu ya ghorofa; chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi
Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. 20

21. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji
kutoka mbinguni. Kisha akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi, kisha kwa maji
hayo akatoa mimea yenye rangi mbali mbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa
kimanjano, na kisha huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa
wenye akili. 21

22. Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua
chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni
sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisio mkumbuka
Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika upotofu wa dhaahiri. 22

23. Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa,
Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu
Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi
Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na
ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa. 23

24. Je! Atakaye kuwa anapambana kwa uso wake na adhabu
mbaya kabisa Siku ya Kiyama (ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye
kudhulumu: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyachuma! 24

25. Walio kuwa kabla yao walikadhibisha , na ikawajia
adhabu kutoka pahala wasipo patambua. 25

26. Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai
wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangeli jua!
26

27. Na bila ya shaka tumewapigia watu mifano ya kila
namna katika hii Qur'ani ili wapate kukumbuka. 27

28. Qur'ani ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu.
28

29. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana
washirika wanao gombana, na wa mtu mwengine aliye khusika na bwana mmoja tu. Je!
Wako sawa katika hali zao? Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu!
Lakini wengi wao hawajui. 29

30. Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa. 30

31. Kisha bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele
ya Mola wenu Mlezi. 31

32. BASI NI NANI dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye
msingizia uwongo Mwenyezi Mungu na kuikanusha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika
Jahannamu makaazi ya hao makafiri? 32

33. Na aliye ileta Kweli na akaithibitisha - hao ndio
wachamngu. 33

34. Watapata watakacho taka kwa Mola wao Mlezi. Hayo
ndiyo malipo ya watendao mema. 34

35. Ili Mwenyezi Mungu awafutie ukomo wa uovu walio
ufanya na awalipe ujira wao kwa mujibu wa ukomo wa wema walio kuwa wakiutenda. 35

36. Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake? Na
ati wanakutishia kwa hao wenginewe wasio kuwa Yeye! Na aliye hukumiwa na
Mwenyezi Mungu kupotea hana wa kumwongoa. 36

37. Na ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa hana wa
kumpotoa. Je! Mwenyezi Mungu si Mwenye nguvu anaye weza kulipiza? 37

38. Na ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi.
Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnao waomba
badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza
kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema
yake? Sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Kwake Yeye wategemee wanao tegemea. 38

39. Enyi watu wangu! Fanyeni mwezavyo, mimi pia nafanya.
Basi mtakuja ona 39

40. Ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye
mshukia adhabu ya daima. 40

41. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu
wote kwa Haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila
ya shaka amepotoka kwa khasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao. 41

42. MWENYEZI MUNGU huzipokea roho zinapo kufa. Na zile
zisio kufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizo hukumiwa kufa, na
huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya
shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. 42

43. Au ndio wanachukua waombezi badala ya Mwenyezi
Mungu? Sema: Ingawa hawana mamlaka juu ya kitu chochote, wala hawatambui lolote?
43

44. Sema: Uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Ni wake
Yeye tu ufalme wa mbingu na ardhi. Kisha mtarejeshwa kwake. 44

45. Na anapo tajwa Mwenyezi Mungu peke yake nyoyo za
wasio iamini Akhera huchafuka. Na wanapo tajwa wenginewe asiye kuwa Yeye basi
wao hufurahi. 45

46. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi!
Mjuzi wa yasiyo onekana na yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako
katika waliyo kuwa wakikhitalifiana. 46

47. Na lau kuwa walio dhulumu wangeli kuwa na vyote
viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa
kujikomboa katika adhabu mbaya hiyo Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa
Mwenyezi Mungu wasiyo kuwa wakiyatarajia. 47

48. Na utawadhihirikia ubaya wa waliyo yachuma,
yatawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. 48

49. Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa
neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo
ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui! 49

50.
Waliyasema haya waliyo kuwa kabla yao, lakini
hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma. 50

51. Basi ukawasibu uovu wa waliyo yachuma. Na wale walio
dhulumu miongoni mwa hawa utawasibu uovu wa waliyo yachuma vile vile. Nao si
wenye kushinda. 51

52. Kwani wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia
riziki amtakaye na akamkadiria? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa
watu wanao amini. 52

53. Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao!
Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi
zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 53

54. Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake,
kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa. 54

55. Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo
teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa
ghafla, na hali hamtambui. 55

56. Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyo
poteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya
maskhara! 56

57. Au ikasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa,
bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa wenye kumchamngu. 57

58. Au ikasema inapo ona adhabu: Lau kuwa ningeli pata
fursa nyengine, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema. 58

59. Wapi! Bila ya shaka zilikujia Ishara zangu, nawe
ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri! 59

60. Na Siku ya Kiyama utawaona walio msingizia uwongo
Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanao
takabari? 60

61. Na Mwenyezi Mungu atawaokoa wenye kujikinga kwa
ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utao wagusa, wala hawatahuzunika. 61

62. Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye
ndiye Mlinzi juu ya kila kitu. 62

63. Yeye anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale walio
zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye kukhasiri. 63

64. Sema: Je! Mnaniamrisha nimuabudu asiye kuwa Mwenyezi
Mungu, enyi majaahili? 64

65. Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa
kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu a'mali zako zitaanguka,
na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kukhasiri. 65

66. Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa
wenye kushukuru. 66

67. Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo
stahiki kadiri yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na
mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Subhanahu wa Taa'la Ametakasika na
Ametukuka na hayo wanayo mshirikisha nayo. 67

68. Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na
waliomo katika ardhi, isipo kuwa aliye mtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa
mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea. 68

69. Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na
Kitabu kitawekwa, na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao
kwa haki, wala hawatadhulumiwa. 69

70. Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyo yafanya, na
Yeye anayajua sana wanayo yatenda. 70

71. Na walio kufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa
makundi. Mpaka watakapo ifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake
watawaambia: Kwani hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za
Mola wenu Mlezi na kukuonyeni mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Kwani! Lakini
limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri. 71

72. Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo.
Basi nayo ni ubaya ulioje wa makaazi ya wanao takabari! 72

73. Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea
Peponi kwa makundi, mpaka watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha
funguliwa. Walinzi wake watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu!
Mmet'ahirika. Basi ingieni humu mkae milele. 73

74. Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za
Mwenyezi Mungu aliye tutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa
katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao! 74

75. Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Kiti cha
enzi cha Mwenyezi Mungu, wakimtakasa na kumsifu Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa
baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola
Mlezi wa viumbe vyote! 75
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani