Tarjuma ya
Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. H'a Mim 1

2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha. 2

3. Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili
mfahamu. 3

4. Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko
kwetu, ni tukufu na yenye hikima. 4

5. Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni
watu mlio pita mipaka kwa ukafiri? 5

6. Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!
6

7. Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.
7

8. Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao.
Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita. 8

9. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi?
Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi, 9

10. Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na
akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka. 10

11. Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji
kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo
tolewa. 11

12. Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na
dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda. 12

13. Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke
neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye
mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. 13

14. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi.
14

15. Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika
mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri. 15

16. Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo
viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume? 16

17. Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia
mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira. 17

18. Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika
mabishano hawezi kusema kwa bayana...? 18

19. Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa
Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na
wao watahojiwa! 19

20. Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli
waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu!
20

21. Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao
wanakishikilia hicho? 21

22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu
wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao. 22

23. Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji
wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta
baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. 23

24. Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye
uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu
hayo mliyo tumwa. 24

25. Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa
walio kadhibisha! 25

26. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu
yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu, 26

27. Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye
ataniongoa. 27

28. Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika
vizazi vyake ili warejee. 28

29. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka
ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha. 29

30. Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na
sisi hakika tunaukataa. 30

31. Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa
kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii? 31

32. Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako
Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na
tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao
wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko
hayo wanayo yakusanya. 32

33. Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli
wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao
pia wanazo pandia, 33

34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea
juu yake, 34

35. Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe
ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye
kumchamngu. 35

36. Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea
Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake. 36

37. Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe
wanadhani kuwa wameongoka. 37

38. Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako
baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu
mno wewe! 38

39. Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo
kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu. 39

40. Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza
kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi? 40

41. Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu
kwao. 41

42. Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka
tuna uweza juu yao. 42

43. Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika
wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. 43

44. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu
yako. Na mtakuja ulizwa. 44

45. Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je!
Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani? 45

46. Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu
ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola
Mlezi wa walimwengu wote! 46

47. Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia
kuzicheka. 47

48. Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa
kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee. 48

49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako
Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
49

50. Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia
kuvunja ahadi. 50

51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi
watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini
yangu? Je! Hamwoni? 51

52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala
hawezi kusema waziwazi? 52

53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au
hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama? 53

54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa
hakika hao walikuwa watu wapotovu. 54

55. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha
wote! 55

56. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha
wote! 56

57. Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako
waliupiga ukelele. 57

58.
Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu?
Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi! 58

59. Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na
tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. 59

60. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu
Malaika katika ardhi wakifuatana. 60

61. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi
usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. 61

62. Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui
yenu wa dhaahiri. 62

63. Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema:
Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana.
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi. 63

64. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na
ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
64

65. Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao
kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu. 65

66. Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na
wala wao hawatambui? 66

67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao,
isipo kuwa wachamngu. 67

68. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala
hamtahuzunika. 68

69. Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa
Waislamu. 69

70. Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa
humo. 70

71.
Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na
vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na
nyinyi mtakaa humo milele. 71

72. Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa
mkiyafanya. 72

73. Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala. 73

74. Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya
Jahannamu. 74

75.
Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
75

76. Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa
madhaalimu. 76

77. Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe
Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo! 77

78. Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika
nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki. 78

79. Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio
tunao pitisha. 79

80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na
minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika. 80

81. Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi
ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu. 81

82.
Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola
Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia. 82

83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe
na hiyo siku yao waliyo ahidiwa. 83

84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika
ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. 84

85. Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na
viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye
mtarudishwa. 85

86. Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza
wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua. 86

87. Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka
watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa? 87

88. Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi!
Hakika hawa ni watu wasio amini. 88

89. Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama.
Watakuja jua. 89
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani