Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI
WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Naapa kwa mlima wa T'ur, 1

2. Na Kitabu kilicho andikwa 2

3. Katika ngozi iliyo kunjuliwa, 3

4. Na kwa Nyumba iliyo jengwa, 4

5. Na kwa dari iliyo nyanyuliwa, 5

6. Na kwa bahari iliyo jazwa, 6

7. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka
itatokea. 7

8. Hapana wa kuizuia. 8

9. Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso, 9

10. Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. 10

11. Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
11

12. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi. 12

13. Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa
nguvu, 13

14.
(Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!
14

15. Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu? 15

16. Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja
kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda. 16

17. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema,
17

18.
Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na
Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni. 18

19. Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya
mliyo kuwa mkiyatenda. 19

20. Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo
pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini. 20

21. Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani
tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika
vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma. 21

22. Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda.
22

23. Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta
maneno ya upuuzi wala dhambi. 23

24. Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu
zilizomo katika chaza. 24

25.
Wataelekeana wakiulizana. 25

26. Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu
tukiogopa; 26

27. Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda
na adhabu ya upepo wa Moto. 27

28. Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu.
Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu. 28

29. Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako
Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu. 29

30. Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia
kupatilizwa na dahari. 30

31. Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika
kutarajia. 31

32. Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao
basi ni watu majeuri tu? 32

33. Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu
hawaamini! 33

34. Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao
wanasema kweli. 34

35. Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote,
au ni wao ndio waumbaji? 35

36. Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na
yakini. 36

37. Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio
wenye madaraka? 37

38. Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo
msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi! 38

39. Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio
mna wavulana? 39

40. Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio
wanaelemewa na uzito wa gharama? 40

41. Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika? 41

42. Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio
kufuru ndio watakao tegeka. 42

43. Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu?
Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye. 43

44. Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka
wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana. 44

45. Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo
hilikishwa. 45

46. Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala
wao hawatanusuriwa. 46

47. Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine
isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui. 47

48. Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe
hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo
simama, 48

49. Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota.
49
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani