Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

1. Huku ni kujitoa Mwenyezi Mungu
na Mtume wake kwenye jukumu la maagano na mlio ahidiana nao katika washirikina. 1

2. Basi tembeeni katika nchi
miezi mine, na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba
Mwenyezi Mungu ndiye anaye wahizi makafiri. 2

3. Na ni tangazo kutokana na
Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu
na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina. Basi mkitubu itakuwa kheri
kwenu, na mkigeuka basi jueni kuwa nyinyi hamumshindi Mwenyezi Mungu. Na
wabashirie makafiri kuwa watapata adhabu chungu. 3

4. Isipo kuwa washirikina ambao
mliahidiana nao kisha wasikupunguzieni chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi
yenu, basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika Mwenyezi Mungu
huwapenda wacha-Mungu. 4

5. Na ikisha miezi mitukufu basi
wauweni washirikina popote mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni
katika kila njia. Lakini wakitubu, wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi
waachilieni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 5

6. Na ikiwa mmoja wapo katika
washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi
Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu
wasiojua kitu. 6

7. Itakuwaje iwepo ahadi na
washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake, ila wale mlio
ahidiana nao kwenye Msikiti Mtakatifu? Basi maadamu wanakwenda nanyi sawa, nanyi
pia nendeni sawa nao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu 7

8. Itakuwaje! Nao wakikushindeni
hawatazami kwenu udugu wala ahadi. Wanakufurahisheni kwa midomo yao tu, na nyoyo
zao zinakataa hayo. Na wengi wao ni wapotovu. 8

9. Wamenunua thamani ndogo kwa
Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakazuilia watu na Njia yake. Hakika hao ni maovu
waliyo kuwa wakiyatenda. 9

10. Hawatazami kwa Muumini udugu
wala ahadi; basi hao ndio warukao mipaka. 10

11. Basi wakitubu na wakashika
Sala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika Dini. Na tunazichambua Aya kwa
watu wajuao. 11

12. Na wakivunja viapo vyao baada
ya kuahidi kwao, na wakatukana Dini yenu, basi piganeni na waongozi wa ukafiri.
Hakika hao hawana viapo vya kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha. 12

13. Je, hamtapigana na watu walio
vunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni
mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope,
ikiwa nyinyi ni Waumini. 13

14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu
awaadhibu kwa mikono yenu, na awahizi na akunusuruni muwashinde, na avipoze
vifua vya kaumu ya Waumini, 14

15. Na aondoe hasira ya nyoyo
zao. Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba ya amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kujua Mwenye hikima. 15

16. Je, mlidhani kuwa mtaachwa
tu, bila ya Mwenyezi Mungu kuwajuulisha wale walio pigana Jihadi kati yenu, na
wala hawakumfanya mwendani wao isipo kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na
Waumini wenziwe? Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda. 16

17. Haiwi kuwa makafiri ndio
waamirishe misikiti ya Mwenyezi Mungu, hali wanajishuhudishia wenyewe ukafiri.
Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika, na katika Moto watadumu. 17

18. Hakika wanao amirisha
misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya
Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu.
Basi huenda hao wakawa katika waongofu. 18

19. Je, mnafanya kuwanywesha maji
Mahujaji na kuamirisha Msikiti Mtakatifu ni sawa na mwenye kumuamini Mwenyezi
Mungu, na Siku ya Mwisho, na akapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu?
Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu. 19

20. Wale walio amini, na
wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na
nafsi zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio
wenye kufuzu. 20

21. Mola wao Mlezi anawabashiria
rehema zitokazo kwake, na radhi, na Bustani ambazo humo watapata neema za
kudumu. 21

22. Watadumu humo milele. Hakika
kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo makubwa. 22

23. Enyi mlio amini! Msiwafanye
baba zenu na ndugu zenu kuwa vipenzi vyenu ikiwa wanastahabu ukafiri kuliko
Imani. Na katika nyinyi atakaye wafanya hao ndio vipenzi vyake, basi hao ndio
madhaalimu. 23

24. Sema: Ikiwa baba zenu, na
wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na
biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi
kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi
ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
wapotovu. 24

25. Hakika Mwenyezi Mungu
amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayni ambapo wingi wenu
ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni kitu. Na ardhi ikawa dhiki kwenu juu
ya upana wake. Kisha mkageuka mkarudi nyuma. 25

26. Kisha Mwenyezi Mungu
akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya Waumini. Na akateremsha
majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu wale walio kufuru. Na hayo ndiyo
malipo ya makafiri. 26

27. Kisha baada ya hayo Mwenyezi
Mungu atawasamehe awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu. 27

28. Enyi mlio amini! Hakika
washirikina ni najsi, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka
wao huu. Na ikiwa mnakhofia umasikini, basi Mwenyezi Mungu atakutajirisheni kwa
fadhila yake akipenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima. 28

29. Piganeni na wasio muamini
Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi
Mungu na Mtume, wala hawashiki Dini ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu,
mpaka watoe kodi kwa khiari yao, hali wamet'ii. 29

30. Na Mayahudi wanasema: Uzeir
ni mwana wa Mungu. Na Wakristo wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo
kauli yao kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi
Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa! 30

31. Wamewafanya makuhani wao na
wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu.
Na wala hawakuamrishwa isipo kuwa wamuabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye.
Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayo mshirikisha nayo. 31

32. Wanataka kuizima Nuru ya
Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu anakataa ila aitimize Nuru
yake ijapo kuwa makafiri watachukia. 32

33. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume
wake kwa uwongofu na Dini ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa
washirikina watachukia. 33

34. Enyi mlio amini! Hakika wengi
katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa baat'ili na wanazuilia
Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu. 34

35. Siku zitapo tiwa moto katika
Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na
migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni
mliyo kuwa mkilimbika. 35

36. Hakika idadi ya miezi kwa
Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu
alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini
iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina wote
kama wao wnavyo pigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na
wachamngu. 36

37. Bila ya shaka kuakhirisha
(miezi) ni kuzidi katika kukufuru; kwa hayo hupotezwa walio kufuru.
Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa
idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo
viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi
Mungu hawaongoi watu makafiri. 37

38. Enyi mlio amini! Mna nini
mnapo ambiwa: Nendeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika
ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha
ya dunia kulinganisha na ya Akhera ni chache. 38

39. Kama hamwendi atakuadhibuni
adhabu chungu, na atawaleta watu wengine, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. 39

40. Ikiwa nyinyi hamtamnusuru
Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni
wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake:
Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia
utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la
walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima. 40

41. Nendeni mtoke, mkiwa wepesi
na wazito, na piganeni Jihadi kwa mali yenu na nafsi zenu katika Njia ya
Mwenyezi Mungu. Haya ni kheri kwenu mkiwa mnajua. 41

42. Na lau ingeli kuwa ipo faida
ya papo kwa papo, na safari yenyewe ni fupi, wangeli kufuata. Lakini wameona ni
mbali na kuna mashaka. Nao wataapa kwa Mwenyezi Mungu: Tungeli weza bila ya
shaka tungeli toka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu
anajua kuwa hakika hao ni waongo. 42
43 
43. Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa ruhusa
kabla ya kubainikia kwako wanao sema kweli, na ukawajua waongo? 43

44. Hawatakuomba ruhusa wale
wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali
yao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua wachamngu. 44

45. Wasio muamini Mwenyezi Mungu
na Siku ya Mwisho na nyoyo zao zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa.
Basi hao wanataradadi katika shaka zao. 45

46. Na ingeli kuwa kweli walitaka
kutoka bila ya shaka wangeli jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia
kutoka kwao, na kwa hivyo akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa! 46

47. Lau wangeli toka nanyi
wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni
fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua
madhaalimu. 47

48. Tangu zamani walitaka
kukutilieni fitna, na wakakupindulia mambo juu chini, mpaka ikaja Haki na
ikadhihirika amri ya Mwenyezi Mungu, na wao wamechukia. 48

49. Na miongoni mwao wapo wanao
sema: Niruhusu wala usinitie katika fitina. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha
tumbukia katika fitina. Na hakika Jahannamu imewazunguka. 49

50. Ukikupata wema unawachukiza,
na ukikusibu msiba, wao husema: Sisi tuliangalia mambo yetu vizuri tangu kwanza.
Na hugeuka kwenda zao nao wamefurahi. 50
51 
51. Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Mwenyezi Mungu.
Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu! 51

52. Sema: Hivyo mnatutazamia
litupate lolote isipo kuwa moja katika mema mawili? Na sisi tunakutazamieni kuwa
Mwenyezi Mungu akufikishieni adhabu itokayo kwake, au kutokana na mikono yetu.
Basi ngojeni, nasi tunangoja pamoja nanyi. 52

53. Sema: Toeni mkipenda
msipende. Hakitopokelewa kitu kwenu, kwani nyinyi ni watu wapotovu. 53

54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa
michango yao ila kwa kuwa walimkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji
kwenye Sala ila kwa uvivu, wala hawatoi michango ila nao wamechukia. 54

55.
Yasikufurahishe mali yao wala
wana wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwayo hapa duniani, na zitoke
roho zao na hali wao ni makafiri. 55

56. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu
kwamba wao ni katika nyinyi, wala wao si katika nyinyi. Lakini ni watu wanao
ogopa. 56

57. Lau kama wangeli pata pa
kukimbilia au mapango au pahala pa kuingia basi wangeli fyatuka mbio kuelekea
huko. 57

58. Na miongoni mwao wapo wanao
kusengenya katika kugawa sadaka. Wanapo pewa wao huridhika. Na wakito pewa
hukasirika. 58

59. Na laiti wao wangeli ridhia
kile alicho wapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakasema: Mwenyezi Mungu
anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila yake - na pia Mtume wake;
hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu! 59

60. Wa kupewa sadaka ni mafakiri,
na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika
kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na
wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kujua Mwenye hikima. 60

61. Na miongoni mwao wapo wanao
muudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni sikio tu. Sema: Basi ni sikio la kheri
kwenu. Anamuamini Mwenyezi Mungu, na ana imani na Waumini, naye ni rehema kwa
wanao amini miongoni mwenu. Na wanao muudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu watapata
adhabu chungu. 61

62. Wanakuapieni Mwenyezi Mungu
ili kukuridhisheni nyinyi, hali ya kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lau kama wao ni Waumini. 62

63. Je, hawajui ya kwamba anaye
shindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata Moto wa Jahannamu
adumu humo? Hiyo ndiyo hizaya kubwa. 63

64. Wanaafiki wanaogopa isije
teremshwa Sura itakayo watajia yaliyomo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni mzaha!
Hakika Mwenyezi Mungu atayatoa nje hayo mnayo yaogopa. 64

65. Na ukiwauliza, wanasema: Sisi
tulikuwa tukipiga porojo na kucheza tu. Sema: Mlikuwa mkimfanyia maskhara
Mwenyezi Mungu na Ishara zake na Mtume wake? 65

66. Msitoe udhuru; mmekwisha
kufuru baada ya kuamini kwenu! Tukilisamehe kundi moja kati yenu, tutaliadhibu
kundi jingine kwa kuwa wao ni wakosefu. 66

67. Wanaume wanaafiki na wanawake
wanaafiki, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba
mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika
wanaafiki ndio wapotofu. 67

68. Mwenyezi Mungu amewaahidi
wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu kudumu
humo. Hayo yanawatosha, na Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu milele. 68

69. Ni kama wale walio kuwa kabla
yenu. Walikuwa wana nguvu na mali na watoto zaidi kuliko nyinyi. Basi
walistarehea fungu lao, na nyinyi mnastarehea fungu lenu, kama walivyo starehe
kwa fungu lao wale walio kuwa kabla yenu. Na nyinyi mkazama katika maovu kama
wao walivyo zama. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na
Akhera; na hao ndio walio khasiri. 69

70. Je, hazikuwafikia khabari za
walio kuwa kabla yao - kaumu ya Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim,
na watu wa Madyana, na miji iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia
kwa hoja zilizo wazi. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini
wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe. 70

71. Na Waumini wanaume na Waumini
wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na
hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao
Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu,
Mwenye hikima. 71

72. Mwenyezi Mungu amewaahidi
Waumini wanaume na Waumini wanawake Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu
humo. Na makaazi mema katika Bustani za kudumu, na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio
kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa. 72

73. Ewe Nabii! Pambana na
makafiri na wanaafiki, na wakazanie. Na makaazi yao ni Jahannamu, na huo ndio
mwisho mbaya. 73

74. Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu
kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya
kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya ambayo hawakuweza kuyafikia. Na
hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kutokana na
fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na wakigeuka Mwenyezi Mungu
atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala hawana katika ardhi mlinzi
wala wa kuwanusuru. 74

75. Na miongoni mwao wapo walio
muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema: Akitupa katika fadhila yake hapana shaka
tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema. 75

76. Alipo wapa katika fadhila
yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza. 76

77. Basi akawalipa unaafiki
kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo kutana naye, kwa sababu ya kuwa
walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyo muahidi, na kwa sababu ya kusema
kwao uwongo. 77

78. Je, hawajui kwamba Mwenyezi
Mungu anajua siri zao na minong'ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuyajua sana ya ghaibu? 78
79 
79. Wale wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka nyingi
na wasio nacho cha kutoa ila kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli. Mwenyezi
Mungu atawakejeli wao! Nao watapata adhabu chungu! 79

80. Waombee msamaha au
usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara sabiini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe.
Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na
Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotofu. 80

81. Walifurahi walio achwa nyuma
kwa kule kubakia kwao nyuma na kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walichukia
kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao, na wakasema: Msitoke nje katika joto!
Sema: Moto wa Jahannamu una joto zaidi, laiti wangeli fahamu! 81

82. Basi nawacheke kidogo;
watalia sana. Hayo ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyachuma. 82

83. Basi Mwenyezi Mungu
akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni mwao - na wakakutaka idhini ya
kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami kabisa, wala hamtapigana na adui
pamoja nami. Nyinyi mliridhia kukaa nyuma mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na
hao watakao bakia nyuma. 83

84. Wala usimsalie kabisa yeyote
katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, na wakafa na hali ni wapotofu. 84

85. Wala zisikushitue mali zao na
watoto wao. Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke
roho zao na hali wao ni makafiri. 85

86. Na inapo teremshwa Sura
isemayo: Muaminini Mwenyezi Mungu na piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale
wenye nguvu miongoni mwao hukutaka ruhusa na husema: Tuache tuwe pamoja na wanao
kaa nyuma! 86

87. Wameridhia kuwa pamoja na
wabakiao nyuma, na nyoyo zao zikapigwa muhuri; kwa hivyo hawafahamu. 87

88. Lakini Mtume na wale walio
amini pamoja naye waliwania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao
pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa. 88

89. Mwenyezi Mungu
amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Huko ndiko kufuzu
kukubwa. 89

90. Na walikuja wenye kutoa
udhuru katika Mabedui ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale walio mwambia Mwenyezi
Mungu na Mtume wake uwongo. Itawafika walio kufuru katika wao adhabu chungu. 90

91. Hapana lawama kwa wanyonge,
wagonjwa, na wasio pata cha kutumia, maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 91

92. Wala wale walio kujia ili
uwachukue ukasema: Sina kipando cha kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao
yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa. 92

93. Ipo njia ya kuwalaumu wale
wanao kuomba ruhusa wasende vitani na hali wao ni matajiri. Wameridhia kuwa
pamoja na wanao bakia nyuma. Na Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri juu ya nyoyo
zao. Kwa hivyo hawajui. 93

94. WATAKUTOLEENI UDHURU mtapo
warudia. Sema: Msitoe udhuru; hatukuaminini. Mwenyezi Mungu amekwisha tueleza
khabari zenu. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wataviona vitendo vyenu. Kisha
mtarudishwa kwa Mjuzi wa ya siri na ya dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa
mkiyatenda. 94

95. Watakuapieni kwa Mwenyezi
Mungu mtakapo rudi kwao ili muwaachilie mbali. Basi waachilieni mbali. Hakika
hao ni najsi, na makaazi yao ni Jahannamu, kuwa ni malipo kwa waliyo kuwa
wakiyachuma. 95

96. Wanakuapieni ili muwe radhi
nao. Basi hata mkiwa radhi nao nyiye, Mwenyezi Mungu hawi radhi na watu
wapotofu. 96

97. Mabedui wamezidi sana katika
ukafiri na unaafiki, na wameelekea zaidi kutojua mipaka ya aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. 97

98. Na katika Mabedui hao wapo
wanao fikiri kuwa wanayo yatoa ni gharama ya bure, na wanakungojeleeni mambo
yakugeukieni. Mageuko maovu yatakuwa juu yao! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia Mwenye kujua. 98

99. Na katika Mabedui wapo wanao
muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaitakidi kuwa wanayo yatoa ndiyo
ya kuwasogeza kwa Mwenyezi Mungu na ya kuwapatia dua za Mtume. Naam! Hayo ni
kweli mambo ya kuwasogeza. Mwenyezi Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira Mwenye kurehemu. 99

100. Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri
na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao
wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo
milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa. 100

101. Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki;
na katika wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui.
Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.
101

102. Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya
vitendo vyema na vingine viovu. Asaa Mwenyezi Mungu akapokea toba zao. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 102

103. Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na
uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. 103

104. Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba
ya waja wake, na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
kupokea toba na Mwenye kurehemu? 104

105. Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na
Mtume wake, na Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua
siri na dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda. 105

106. Na wapo wengine wanangojea amri ya Mwenyezi Mungu -
ama atawaadhibu au atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
106

107. Na wapo walio jenga msikiti kwa ajili ya madhara na
ukafiri na kuwafarikisha Waumini, na pa kuvizia kwa walio mpiga vita Mwenyezi
Mungu na Mtume wake hapo kabla. Na bila ya shaka wataapa kwamba: Hatukukusudia
ila wema tu. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao ni waongo. 107

108. Usisimame kwenye msikiti huo kabisa. Msikiti ulio
jengwa juu ya msingi wa uchamngu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe
usimame ndani yake. Humo wamo watu wanao penda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu
anawapenda wanao jitakasa. 108

109. Je! Mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya
kumcha Mwenyezi Mungu na radhi zake ni bora au mwenye kuweka msingi wa jengo
lake juu ya ukingo wa shimo linalo burugunyika, na likaburugunyika naye katika
Moto wa Jahannamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu. 109

110. Na jengo lao hilo walilo lijenga litakuwa sababu ya
kutia wasiwasi nyoyoni mwao mpaka nyoyo zao hizo zikatike vipande vipande. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima. 110

111. Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi
zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi
Mungu - wanauwa na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyo jilazimisha kwa Haki katika
Taurati na Injili na Qur'ani. Na nani atimizae ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi
furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa, 111

112. (Kwa) wanao tubia, wanao abudu, wanao himidi, wanao
kimbilia kheri, wanao rukuu, wanao sujudu, wanao amrisha mema na wanao kataza
maovu, na wanao linda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na wabashirie Waumini. 112

113. Haimpasii Nabii na wale walio amini kuwatakia
msamaha washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao
ni watu wa Motoni. 113

114. Wala haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila
kwa sababu wa ahadi aliyo fanya naye. Lakini ilipo mbainikia kwamba yeye ni adui
ya Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa mwingi wa kuomba,
mnyenyekevu, mvumilivu. 114

115. Na haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwahisabu watu kuwa
wamepotea baada ya kwisha waongoza mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. 115

116. Hakika Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na
ardhi; huhuisha na hufisha. Nanyi hamna Mlinzi wala Msaidizi isipo kuwa Mwenyezi
Mungu. 116

117. Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na
Wahajiri na Ansari walio mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia
nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao
ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu. 117

118. Na pia wale watatu walio achwa nyuma hata dunia
wakaiona dhiki juu ya ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika
kuwa hapana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwake Yeye. Kisha akawaelekea
kwa rehema yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kupokea toba na Mwenye kurehemu. 118

119. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni
pamoja na wakweli. 119

120. Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio jirani
zao kubakia nyuma wasitoke na Mtume, wala kujipendelea nafsi zao kuliko yeye.
Hayo ni kwa kuwa hakiwapati kiu, wala machofu, wala njaa, kwa ajili ya Njia ya
Mwenyezi Mungu, wala hawendi mahali panapo waghadhibisha makafiri, wala
hakiwapati chochote kutokana na maadui, ila huandikiwa kuwa ni kitendo chema.
Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wanao fanya mema. 120

121. Wala hawatoi cha kutoa kidogo wala kikubwa, wala
hawalivuki bonde, ila huandikiwa, ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo kuwa
wakiya- tenda. 121

122. Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini kwa
nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na
kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha? 122

123. Enyi mlio amini! Piganeni na wale makafiri walio
karibu yenu, na wakute ugumu kwenu. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja
na wacha- Mungu. 123

124. Na inapo teremshwa Sura wapo miongoni mwao wasemao:
Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walio amini
inawazidishia Imani, nao wanafurahi. 124

125. Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi
inawazidishia uovu juu ya uovu wao; na wanakufa hali ni makafiri. 125

126. Je! Hawaoni ya kwamba wanatiwa mtihanini kila mwaka
mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki. 126

127. Na ikiteremka Sura hutazamana wao kwa wao, (kama
kwamba wanasema:) Je! Yuko mtu anakuoneni? Kisha hugeukilia mbali. Mwenyezi
amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu. 127

128. Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi
wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini
ni mpole na mwenye huruma. 128

129. Basi wakigeuka, wewe sema: Mwenyezi Mungu
ananitosheleza. Hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi namtegemea Yeye, na Yeye
ndiye Mola Mlezi wa Kiti Kikuu cha Enzi. 129
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani