Tarjuma ya Quran Tukufu kwa
kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni
talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi
Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila
wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu,
msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi
yake. Hujui; labda Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya. 1

2. Basi wanapo fikia muda wao, ima warejeeni muwaweke
kwa wema, au farikianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu
miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo
ndivyo anavyo agizwa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anaye
mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea. 2

3. Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye
mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri
yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake. 3

4. Na wale walio sita hedhi miongoni mwa wanawake wenu,
ikiwa mnayo shaka, basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, pamoja na ambao
hawapati hedhi. Na wenye mimba eda yao mpaka watakapo zaa. Na anaye mcha
Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi. 4

5. Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu amekuteremshieni. Na
anaye mcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa.
5

6. Wawekeni humo humo mnamo kaa nyinyi kwa kadiri ya
pato lenu, wala msiwaletee madhara kwa kuwadhiki. Na wakiwa wana mimba,
wagharimieni mpaka wajifungue. Na wakikunyonyesheeni, basi wapeni ujira wao, na
shaurianeni kwa wema. Na mkiona uzito kati yenu, basi amnyonyeshee mwanamke
mwengine. 6

7. Mwenye wasaa atoe kadiri ya wasaa wake, na mwenye
dhiki atoe katika alicho mpa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila
kwa kadiri ya alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.
7

8. Na miji mingapi iliyo vunja amri ya Mola wake Mlezi
na Mitume wake, basi tuliihisabia hisabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali.
8

9. Basi ikauonja ubaya wa mambo yake; na mwisho wa
mambo yao ilikuwa khasara. 9

10.
Mwenyezi Mungu aliwaandalia adhabu kali. Basi
mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, mlio amini! Hakika Mwenyezi Mungu
amekuteremshieni Ukumbusho, 10

11. Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo
bainisha, ili kuwatoa walio amini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka
kwenye nuru. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema, atamwingiza
katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Mwenyezi Mungu
amekwisha mpa riziki nzuri. 11

12.
Mwenyezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu
saba, na ardhi kwa mfano wa hizo. Amri zake zinashuka baina yao, ili mjue kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu
amekizunguka kila kitu kukijua vilivyo kwa ilimu yake. 12
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani