Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. H'a Mim 1

2. A'yn Sin Qaf 2

3. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye
hikima anavyo kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako. 3

4. Ni vyake viliomo mbinguni, na viliomo katika ardhi.
Na Yeye ndiye Mtukufu, Mkuu. 4

5.
Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika
wakimtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye
ardhi. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 5

6. Na wale walio wafanya walinzi wengine badala yake
Yeye, Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.
6

7. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili
uwaonye watu wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya
Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni.
7

8. Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote
umma mmoja, lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu
hawana mlinzi wala msaidizi. 8

9. Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini
Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye
ndiye Mweza wa kila kitu. 9

10. Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu
yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye
mtegemea na kwake Yeye narejea. 10

11. Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni
mke na mume katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni
namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
11

12. Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi.
Humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila
kitu. 12

13.
Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na
tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni
Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia.
Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye. 13

14. Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa
sababu ya husuda iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli
kutoka kwa Mola wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka
palingeli hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao
wanakitilia shaka inayo wahangaisha. 14

15. Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama
ulivyo amrishwa, wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha
Mwenyezi Mungu katika Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu.
Mwenyezi Mungu ni Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa
vitendo vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina
yetu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.
15

16. Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya
kukubaliwa, hoja za hawa ni baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo
ghadhabu, na itakuwa kwao adhabu kali. 16

17.
Mwenyezi Mungu ndiye aliye teremsha Kitabu kwa
Haki, na Mizani. Na nini kitakacho kujuulisha ya kwamba pengine Saa ya Kiyama
ipo karibu? 17

18. Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini
wanao amini wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika
hao wanao bishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali
kabisa. 18

19.
Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku
ampendaye. Naye ni Mwenye nguvu, Mtukufu. 19

20. Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika
mavuno yake, na mwenye kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini
katika Akhera hana fungu. 20

21. Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia
dini asiyo itolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la
kupambanua basi wangeli katiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu
watapata adhabu chungu. 21

22.
Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa
sababu ya waliyo yachuma, nayo yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema
watakuwamo katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao
Mlezi. Hiyo ndiyo fadhila kubwa. 22

23. Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja
wake walio amini na wakatenda mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila
mapenzi katika kujikurubisha. Na anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye shukrani. 23

24. Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo?
Mwenyezi Mungu akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu
anaufuta upotofu na anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua
yaliomo vifuani. 24

25. Naye ndiye anaye pokea toba kwa waja wake, na
anasamehe makosa, na anayajua mnayo yatenda. 25

26. Na anawaitikia wanao amini na wakatenda mema, na
anawazidishia fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu chungu. 26

27. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki
waja wake, basi bila ya shaka wangeli panda kiburi katika dunia. Lakini
anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na
anawaona. 27

28. Naye ndiye anaye iteremsha mvua baada ya wao kwisha
kata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi Mwenye kuhimidiwa.
28

29. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na
wanyama alio waeneza. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo. 29

30. Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo
vya mikono yenu. Naye anasamehe mengi. 30

31. Na nyinyi hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala
nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi badala ya Mwenyezi Mungu. 31

32. Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na
kurejea baharini kama vilima. 32

33.
Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo
husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye
kusubiri akashukuru. 33

34. Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyo
yatenda hao watu. Naye husamehe mengi. 34

35. Na ili wajue wanao jadiliana katika Ishara zetu
kwamba hawana pahala pa kukimbilia. 35

36. Basi vyote mlivyo pewa ni starehe ya maisha ya
dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili
ya walio amini, na wakawa wanamtegemea Mola wao Mlezi, 36

37. Na wanayo yaepuka madhambi makubwa na mambo
machafu, na wanapo kasirika wao husamehe, 37

38. Na wanao mwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika
Sala, na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na kutokana na tulicho
waruzuku wakawa wanatoa, 38

39. Na ambao wanapo fanyiwa jeuri hujitetea. 39

40. Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini
mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu.
Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu. 40

41. Na wanao jitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana
njia ya kuwalaumu. 41

42. Bali lawama ipo kwa wale wanao wadhulumu watu, na
wanafanya jeuri katika nchi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.
42

43. Na anaye subiri, na akasamehe, hakika hayo ni
katika mambo ya kuazimiwa. 43

44. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana
mlinzi baada yake. Na utawaona wenye kudhulumu watakapo iona adhabu wanasema:
Je! Ipo njia ya kurudi? 44

45. Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao
wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini
watasema: Hakika wapatao khasara ni hao walio khasiri nafsi zao na ahali zao
Siku ya Kiyama. Ama hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya daima.
45

46. Wala hawatakuwa na walinzi wa kuwanusuru mbele ya
Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote.
46

47.
Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku
isiyo epukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa pa kukimbilia wala
hamtakuwa na cha kukingia. 47

48. Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe
mwangalizi wao. Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi
tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa
sababu ya iliyo yatanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.
48

49. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu;
anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye
watoto wa kiume, 49

50. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya
amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza. 50

51. Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu
amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye
humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.
51

52. Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa amri yetu.
Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo
kwayo tunammwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye
Njia Iliyo Nyooka. 52

53. Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu
viliomo mbinguni na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi
Mungu. 53
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii [email protected]
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani