Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

32.Surat As-Sajdah


image
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

image
1. Alif Lam Mim (A.L.M.) 1

image
2. Huu ni mteremsho wa Kitabu kisicho kuwa na shaka yoyote kinacho toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. 1

image
3. Au wanasema: Amekizua? Bali hichi ni Kweli iliyo toka kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio fikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda wakaongoka. 3

image
4. Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa siku sita, na akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki? 4

image
5. Anapitisha mambo yote yalio baina mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyo hisabu nyinyi. 5

image
6. Huyu ndiye Mwenye kuyajua yasiyo onekana na yanayo onekana. Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. 6

image
7. Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo. 7

image
8. Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu. 8

image
9. Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru. 9

image
10. Nao husema: Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi. 10

image
11. Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi. 11

image
12. Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa. 12

image
13. Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu : Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu. 13

image
14. Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda. 14

image
15. Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni. 15

image
16. Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku. 16

image
17. Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda. 17

image
18. Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa. 18

image
19. Ama walio amini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za makaazi mazuri. Ndio pa kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda. 19

image
20. Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni Motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mliyo kuwa mkiikanusha. 20

image
21. Na tutawaonjesha adhabu khafifu kabla ya adhabu kubwa, huenda labda watarejea. 21

image
22. Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi tutajilipiza kwa wakosefu. 22

image
23. Hakika Sisi tulikwisha mpa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka kuwa kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili. 23

image
24. Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu. 24

image
25. Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye fafanua baina yao Siku ya Kiyama katika waliyo kuwa wakikhitalifiana. 25

image
26. Je! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao, nao wanapita katika maskani zao hizo? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je, hawasikii? 26

image
27. Je! Hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayo kula wanyama wao na wao wenyewe? Je! Hawaoni? 27

image
28. Wanasema: Ushindi huu ni lini, kama mnasema kweli? 28

image
29. Sema: Siku ya Ushindi, wale walio kufuru imani yao haitawafaa kitu, wala wao hawatapewa muhula. 29

image
30. Basi wapuuze, nawe ngonja; hakika wao wanangoja. 30


Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com 
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani