Tarjuma ya
Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na
katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 1

2. Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda?
2

3. Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa
mnasema msiyo yatenda. 3

4. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana
katika Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana. 4

5. Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu!
Kwa nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu
niliye tumwa kwenu? Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke.
Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu. 5

6. Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili!
Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa
kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada
yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu
ni uchawi ulio dhaahiri! 6

7. Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye
mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu madhaalimu. 7

8. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa
vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia.
8

9. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na
Dini ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
9

10. Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayo
kuokoeni na adhabu iliyo chungu? 10

11. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni
Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora
kwenu, ikiwa nyinyi mnajua. 11

12.
Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika
Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za
milele. Huko ndio kufuzu kukubwa. 12

13. Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo
kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini! 13

14. Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi
Mungu, kama alivyo sema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi
wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi
Mungu! Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine
lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye
kushinda. 14
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani