Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu
kinacho bainisha; 1

2. Uwongofu na bishara kwa Waumini, 2

3. Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera
wana yakini nayo. 3

4. Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia
vitendo vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo. 4

5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika
Akhera ndio watapata khasara zaidi. 5

6. Na hakika wewe unafundishwa Qur'ani inayo tokana
kwake Mwenye hikima Mwenye kujua. 6

7. (Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika
nimeona moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho
waka ili mpate kuota moto. 7

8. Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika
moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi
wa walimwengu wote. 8

9. Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye
nguvu, Mwenye hikima. 9

10. Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama
nyoka, aligeuka nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele
yangu Mitume. 10

11. Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada
ya ubaya, basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 11

12. Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka
mweupe bila ya maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu
yake. Hakika hao walikuwa watu waovu. 12

13. Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye
kuonyesha, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri. 13

14. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya
kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi! 14

15. Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na
wakasema: Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye
tufadhilisha kuliko wengi katika waja wake Waumini. 15

16. Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu!
Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo
dhaahiri. 16

17. Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na
watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu. 17

18. Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu,
alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu,
asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua. 18

19. Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili,
na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha
mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema
yako katika waja wako wema. 19

20. Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona
simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu? 20

21. Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au
nitamchinja, au aniletee hoja ya kutosha. 21

22. Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema:
Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na
nakuletea khabari za yakini. 22

23. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye
amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa. 23

24. Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua
badala ya Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia
Njia. Kwa hivyo hawakuongoka 24

25. Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa
yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo
yatangaza. 25

26. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi
wa A'rshi tukufu.. 26

27. Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au
wewe ni miongoni mwa waongo. 27

28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha
waache na utazame watarejesha nini. 28

29. (Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika
nimeletewa barua tukufu. 29

30. Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. 30

31.
Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha
kuwa wenye kusalimu amri. 31

32. Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika
jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie. 32

33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita;
na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha. 33

34. Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji
wanauharibu, na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo
watendavyo. 34

35. Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja
watakayo rudi nayo wajumbe. 35

36. Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema
(Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni
bora zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.
36

37. Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi
wasio yaweza kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili
na wanyonge. 37

38. Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu
atakaye niletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu
amri. 38

39. Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea
kabla hujainuka pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu. 39

40. Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea
kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema:
Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au
nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi
yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu. 40

41. Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone
ataongoka, au atakuwa miongoni mwa wasio ongoka. 41

42. Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako
cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake
wakasema): Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu. 42

43. Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi
Mungu yalimzuilia. Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri. 43

44.
Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo
liona alidhani ni maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman)
akasema: Hakika hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola
wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja na
Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. 44

45. . Na kwa kina Thamud tulimtuma ndugu yao Saleh
kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayo gombana. 45

46. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu
kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe? 46

47. Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja
nawe. Yeye akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi
ni watu mnao jaribiwa. 47

48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi
katika nchi wala hawafanyi la maslaha. 48

49. Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu
tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi
hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli. 49

50. Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga
mipango yetu, na wao hawatambui. 50

51. Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya
kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote. 51

52. Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo
dhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua. 52

53. Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa
wanamchamngu. 53

54. Na Lut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya
uchafu nanyi mnaona? 54

55. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio
badala ya wanawake? Hakika nyinyi ni watu mnao fanya ujinga kabisa! 55

56. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema:
Wafukuzeni wafwasi wa Lut'i katika mji wenu. Hao ni watu wanao jitia usafi. 56

57. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa
mkewe; tukamkadiria katika walio baki nyuma. 57

58. Na tukawanyeshea mvua. Ni ovu kweli kweli hiyo mvua
ya walio kwisha onywa. 58

59. Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi
Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni
bora, au wale wanao washirikisha naye? 59

60. AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na
akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye
kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo mungu pamoja na
Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu walio potoka. 60

61. Au nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na
akajaalia ndani yake mito, na akaweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili
kiziwizi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui. 61

62. Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo
mwomba, na akaiondoa dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu
pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayo yazingatia. 62

63. Au nani yule anaye kuongoeni katika giza la bara na
bahari, na akazipeleka pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu
pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya wanao washirikisha
naye. 63

64. Au nani anaye uanzisha uumbaji, kisha akaurejesha?
Na nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je! Yupo mungu pamoja
na Mwenyezi Mungu? Sema: Leteni hoja zenu kama nyinyi ni wasema kweli. 64

65. Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya
ghaibu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Wala wao hawajui lini watafufuliwa. 65

66. Kwani huo ujuzi wao umefikilia kuijua Akhera? Bali
wao wamo katika shaka nayo tu, bali wao ni vipofu nayo. 66

67. Na wakasema walio kufuru: Tutapo kuwa mchanga, sisi
na baba zetu, hivyo kweli tutakuja tolewa? 67

68. Haya haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani.
Hayakuwa haya ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale. 68

69. Sema: Nendeni katika ardhi, na tazameni ulikuwaje
mwisho wa wakosefu. 69

70. Wala usiwahuzunukie wala usiwe katika dhiki kwa
sababu ya hila zao wanazo zifanya. 70

71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa mnasema
kweli? 71

72. Sema: Asaa ni karibu kukufikieni sehemu ya yale
mnayo yahimiza. 72

73. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye fadhila kwa
watu, lakini wengi wao hawashukuru. 73

74. Na hakika Mola wako Mlezi anayajua yanayo ficha
vifua vyao na wanayo yatangaza. 74

75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo
katika Kitabu kinacho bainisha. 75

76. Hakika Qur'ani hii inawasimulia Wana wa Israili
mengi wanayo khitalifiana nayo. 76

77. Nayo hakika ni Uwongofu na Rehema kwa Waumini. 77

78. Hakika Mola wako Mlezi atawahukumu kwa hukumu yake,
naye ni Mwenye nguvu Mjuzi. 78

79. . Basi mtegemee Mweneyezi Mungu; hakika wewe uko
juu ya Haki iliyo wazi. 79

80. Kwa hakika wewe huwezi kuwafanya maiti wasikie,
wala kuwafanya viziwi wasikie wito, wanapo kwisha geuka kwenda zao. 80

81. Wala huwezi kuwaongoa vipofu waache upotovu wao.
Huwezi kuwafanya wasikie isipo kuwa wenye kuziamini Ishara zetu; na hao ndio
wat'iifu. 81

82. Na itapo waangukia kauli juu yao, tutawatolea
mnyama katika ardhi atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana na yakini na
Ishara zetu. 82

83. Na Siku tutapo kusanya kutoka kila umma kundi
katika wanao kadhibisha Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu. 83

84. Hata watakapo fika, atasema (Mwenyezi Mungu): Je!
Nyinyi si mlizikanusha Ishara zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya
nini? 84

85. Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyo
dhulumu. Basi hao hawatasema lolote. 85

86. Je! Hawaoni kwamba sisi tumeufanya usiku ili
watulie, na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
amini. 86

87. Na Siku litapo pulizwa baragumu, watahangaika
waliomo mbinguni na katika ardhi, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote
watamfikia nao ni wanyonge. 87

88. Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo
inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye
tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo. 88

89. Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo.
Nao watasalimika na mahangaiko ya Siku hiyo. 89

90. Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso
zao Motoni. Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda? 90

91. Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji
huu aliye ufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa
niwe miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea. 91

92. Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi
ameongoka kwa faida ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni
miongoni mwa waonyaji. 92

93. Na sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za
Mwenyezi Mungu. Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako Mlezi
si mwenye kughafilika na myatendayo. 93
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani