Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

0. KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE
KUREHEMU. 0

1. Amri ya Mwenyezi Mungu itafika tu. Basi msiihimize.
Ametakasika na Ametukuka na wanayo mshirikisha nayo. 1

2.
Huwateremsha Malaika na Roho kwa amri yake juu ya
amtakaye katika waja wake ili nyinyi muonye kwamba hapana mungu ila Mimi, basi
nicheni Mimi. 2

3. Ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Ametukuka na
wanayo shirikisha. 3

4. Amemuumba mtu kwa tone la manii. Naye mara amekuwa
mshindani dhaahiri. 4

5. Na nyama hoa amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya
kutia joto,na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala. 5

6. Na wanakupeni furaha pale mnapo warudisha jioni na
mnapo wapeleka malishoni asubuhi.6

7. Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyo
weza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na
Mwenye kurehemu. 7

8. Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na
kuwa ni pambo.Na ataumba msivyo vijua. 8

9. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuelekeza Njia. Na zipo
njia za upotovu.Na angeli penda angeli kuongoeni nyote. 9

.10 Yeye ndiye anaye kuteremshieni maji kutoka
mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia. 10

11. Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na
mizaituni,na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya
zipo ishara kwa watu wanao fikiri. 11

12. Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na
mwezi,na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa
watu wenye akili. 12

13. Na hivi alivyo vieneza katika ardhi vya rangi mbali
mbali. Hakika katika hayo ipo ishara kwa watu wanao waidhika. 13

14. Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili
kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na
unaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate
kushukuru. 14
15 
15. Na kaweka katika ardhi milima ili ardhi isiyumbe
yumbe nanyi.Na mito, na njia ili mpate kuongoka. 15

16. Na alama nyengine. Na kwa nyota wao wanajiongoza. 16

17. Ati anaye umba ni kama asiye umba? Basi hebu,
hamkumbuki? 17

18. Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi
kuzidhibiti.Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu. 18

19. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha na mnayo
yatangaza. 19

20. Na wale wanao waomba wasio kuwa Mwenyezi Mungu
hawaumbi kitu,bali wao wameumbwa. 20

21. Ni wafu si wahai, na wala hawajui watafufuliwa
lini. 21

22. Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Lakini wasio iamini
Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wanajivuna. 22

23. Hapana shaka kuwa hakika Mwenyezi Mungu anayajua
wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Kwa hakika Yeye hawapendi wanao jivuna. 23

24. Na wanapo ambiwa: Kateremsha nini Mola wenu Mlezi?
Husema: Hadithi za kubuni za watu wa kale! 24

25. Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama,
na sehemu ya mizigo ya wale wanao wapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno
hayo wanayo yabeba! 25

26.
Walipanga vitimbi walio kuwa kabla yao, Mwenyezi
Mungu akayasukua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao, na
adhabu ikawajia kutoka wasipo kujua. 26

27. Kisha Siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako
wapi hao washirika wangu ambao kwao mkiwakutisha (Manabii) mashaka? Watasema
walio pewa ilimu:Hakika leo ndiyo hizaya na adhabu itawashukia makafiri, 27

28. Ambao Malaika waliwafisha nao wamejidhulumu nafsi
zao! Basi watasalimu amri, waseme: Hatukuwa tukifanya uovu wowote. (Wataambiwa):
Kwani! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyo kuwa mkiyatenda. 28

29. Basi ingieni milango ya Jahannamu, humo mdumu. Ni
maovu mno makaazi ya wafanyao kiburi! 29

30. Na wataambiwa walio mcha Mungu: Mola wenu Mlezi
kateremsha nini? Watasema: Kheri. Walio fanya wema katika dunia hii watapata
wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi, na njema mno nyumba ya wachamngu. 30

31. Bustani za milele wataziingia; iwe inapita kati
yake mito. Humo watapata watakacho. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye
kumcha. 31

32. Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema,
wanawaambia:Amani iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyo kuwa
mkiyatenda. 32

33.
Wanangojea jengine hawa ila Malaika wawafikie, au
iwafikie amri ya Mola wako Mlezi? Kama hivyo walitenda walio kuwa kabla yao. Na
MwenyeziMungu hakuwadhulumu, lakini walijidhulumu wenyewe. 33

34. Basi ukawafikia uovu wa waliyo yatenda, na waliyo
kuwa wakiyakejeli yakawazunguka. 34

35. Na washirikina wanasema: Mwenyezi Mungu angeli taka
tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeli
harimisha chochote bila ya Yeye. Kama hivyo walifanya walio kuwa kabla yao. Basi
lipo lolote juu ya Mitume isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi? 35

36. Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume
kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio
waongoa MwenyeziMungu. Na kati yao wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi
tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha. 36

37. Hata ukiwa na pupa ya kutaka kuwaongoa, lakini
Mwenyezi Mungu hamwongoi yule anaye shikilia kupotea. Wala hawatapata wa
kuwanusuru. 37

38. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao
kwamba MwenyeziMungu hatomfufua aliye kufa. Kwani! Ni ahadi iliyo juu yake
kikweli; lakini watu wengi hawajui. 38

39. Ili kuwabainishia yale waliyo khitalifiana, na ili
wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa ni waongo. 39

40. Kauli yetu kwa kitu tunacho kitaka kiwe, ni
kukiambia: Kuwa!Basi kinakuwa. 40

41. Na wale walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
baada ya kudhulumiwa,bila ya shaka tutawaweka duniani kwa wema; na ujira wa
Akhera ni mkubwa zaidi; laiti kuwa wanajua! 41

42. Wale wanao subiri na wakamtegemea Mola wao Mlezi. 42

43. Nasi hatukuwatuma kabla yako ila watu wanaume tulio
wapa Wahyi(Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. 43

44. Kwa Ishara wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia
wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyo teremshwa kwao, wapate kufikiri. 44

45. Je! Wameaminisha wanao fanya vitimbi vya uovu
kwamba MwenyeziMungu hatawadidimiza katika ardhi, na haitawafika adhabu kutoka
wasipopajua? 45

46. Au hatawashika katika nyendo zao, na wala
hawataponyoka? 46

47. Au hatawashika kwa kitisho na kuwapunguza kidogo
kidogo? Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.47

48. Je! Hawavioni vitu alivyo viumba Mwenyezi Mungu -
vivuli vyao vinaelekea kushotoni na kuliani, kumsujudia Mwenyezi Mungu na
vikinyenyekea? 48

49. Na vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi,
tangu wanyama mpaka Malaika, vinamsujuidia Mwenyezi Mungu, na wala havitakabari.
49

50.
Vinamkhofu Mola wao Mlezi aliye juu yao, na
vinafanya vinavyoamrishwa. 
51. Na Mwenyezi Mungu amesema: Msiwe na miungu wawili!
Hakika Yeye ni Mungu Mmoja. Basi niogopeni Mimi tu! 51

52. Na ni vyake Yeye viliomo katika mbingu na ardhi. Na
Dini ni yake Yeye daima. Je! Mtamcha mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu? 52

53. Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi
Mungu. Kisha yakikuguseni madhara mnamyayatikia Yeye. 53

54. Na anapo kuondosheeni madhara mara kundi moja
miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao Mlezi, 54

55.
Wakizikataa neema tulizo wapa. Basi stareheni.
Mtakuja jua! 55

56. Na hao ambao hata hawawajui wanawawekea sehemu ya
tunavyo waruzuku.Wallahi! Bila ya shaka mtasailiwa kwa hayo mliyo kuwa mnayazua!
56

57. Na wanamfanyia Mwenyezi Mungu ati ana mabinti,
Subhanahu, Aliyetakasika! Na wao wenyewe, ati ndio wawe na hayo wanayo yatamani!
57

58. Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake
unasawijika,naye kajaa chuki. 58

59.
Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo
bashiriwa! Je,akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa
wanavyohukumu! 59

60. Hali ya wasio iamini Akhera ni ovu; na Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye sifa tukufu. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 60

61. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu
kwa mujibu wa dhulma zao, basi asingeli mwacha hapa hata mnyama mmoja. Lakini
anawaakhirisha mpaka muda ulio wekwa. Na unapo fika muda wao hawatakawilia hata
saa moja wala hawatatangulia. 61

62. Na wanampa Mwenyezi Mungu wanavyo vichukia wao, na
ndimi zao zinasema uwongo kwamba wao watapata mema. Hapana shaka hakika
wamewekewa Moto, nao wataachwa humo. 62

63. Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizo kuwa
kabla yako,lakini Shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye
rafiki yao; nao watapata adhabu chungu. 63

64. Na hatukukuteremshia Kitabu isipo kuwa uwabainishie
yale ambayo wanakhitalifiana, na kiwe Uwongofu na Rehema kwa watu wanao amini. 64

65. Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni
na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Kwa hakika katika hayo imo
Ishara kwa watu wanao sikia. 65

66. Na hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio.
Tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na
damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao. 66

67. Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu
mnatengeneza ulevi na riziki nzuri. Hakika katika hayo ipo Ishara kwa wanao
tumia akili. 67

68. Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee
majumba yako katika milima,na katika miti, na katika wanayo jenga watu. 68

69. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika
njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao
kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa
wanaadamu.Hakika katika haya ipo Ishara kwa watu wanao fikiri. 69

70. Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni; kisha anakufisheni.
Na miongoni mwenu wapo wanao rudishwa kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa
asijue kitu baada ya ujuzi alio kuwa nao. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na
Mweza. 70

71. Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu
kuliko wengine katika riziki. Na wale walio fadhilishwa hawarudishi riziki zao
kwa wale ilio wamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo.
Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu? 71

72. Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi
yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni
vitu vizuri vizuri.Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Mwenyezi
Mungu? 72

73. Na badala ya Mwenyezi Mungu wanawaabudu wasio
wamilikia riziki kutoka mbinguni wala kwenye ardhi, wala hawawezi kitu. 73

74. Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika
Mwenyezi Mungu anajua,na nyinyi hamjui. 74

75. Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye
milikiwa, asiyeweza kitu, na mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka
kwetu,naye akawa anatoa katika riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao
watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu.Lakini
wengi wao hawajui. 75

76. Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili.
Mmoja wao ni bubu, hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake. Popote anapo
muelekeza haleti kheri. Je! Huyo anaweza kuwa sawa na yule anaye amrisha
uadilifu,naye yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka. 76

77. Na siri zote za katika mbingu na ardhi ziko kwa
Mwenyezi Mungu.Wala halikuwa jambo la Saa (ya Kiyama) ila kama kupepesa kwa
jicho, au akali ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. 77

78. Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama
zenu, hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili
mpate kushukuru. 78

79. Je! Hawawaoni ndege walivyo wat'iifu katika anga la
mbingu? Hapana mwenye kuwashika isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya
zipo ishara kwa watu wanao amini. 79

80. Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe
ni maskani yenu, na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo
ziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na
sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia
kwa muda. 80

81. Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni vivuli katika vitu
alivyo viumba,na amekufanyieni maskani milimani, na amekufanyieni nguo za
kukingeni na joto, na nguo za kukingeni katika vita vyenu. Ndio hivyo
anakutimizieni neema zake ili mpate kut'ii. 81

82. Basi wakikengeuka lilio juu yako wewe ni kufikisha
ujumbe waziwazi. 82

83.
Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu, kisha
wanazikanusha; na wengi wao ni makafiri. 83

84. Na siku tutakapo wainua kutokana na kila umma
shahidi, kisha hawataruhusiwa walio kufuru wala hawataachiliwa kutaka radhi. 84

85. Na walio dhulumu watakapo iona adhabu
hawatapunguziwa hiyo adhabu,wala hawatapewa muhula. 85

86. Na walio shirikisha watakapo waona hao walio
washirikisha na Mwenyezi Mungu, watasema: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio
washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaabudu badala yako. Ndipo wale watakapo
watupia kauli:Hakika nyinyi ni waongo! 86

87. Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi
Mungu, na yatapotea waliyo kuwa wakiyazua. 87

88. Wale walio kufuru na kuzuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu tutawazidishia adhabu juu ya adhabu, kwa walivyo kuwa wakifisidi. 88

89. Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika
kila umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe
shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu,
na ni uwongofu,na rehema, na bishara kwa Waislamu. 89

90. Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu,
na hisani,na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma.
Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka. 90

91. Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi,
wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi
Mungu ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo. 91

92. Wala msiwe kama mwanamke anaye uzongoa uzi wake
baada ya kwisha usokota ukawa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya
kudanganyana baina yenu kwa kuwa ati taifa moja lina nguvu zaidi kuliko jengine?
Hakika Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa njia hiyo. Na bila ya shaka
atakubainishieni Siku ya Kiyama mliyo kuwa mkikhitalifiana. 92

93. Na Mwenyezi Mungu angeli taka, kwa yakini angeli
kufanyeni umma mmoja. Lakini anamwachia kupotea anaye mtaka, na anamwongoa
amtakaye. Na hakika mtaulizwa kwa yale mliyo kuwa mkiyafanya. 93

94. Wala msifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana
baina yenu.Usije mguu ukateleza badala ya kuthibiti, na mkaonja maovu kwa sababu
ya kule kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa. 94

95. Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani
ndogo. Hakika kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajua. 95

96. Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi
Mungu ndivyo vitakavyo bakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa walio subiri ujira wao
kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda. 96

97. Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye
akawa ni Muumini,tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya
waliyo kuwa wakiyatenda. 97

98. Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde
na Shetani maluuni. 98

99. Hakika yeye hana madaraka juu ya walio amini na
wakamtegemea Mola wao Mlezi. 99

100.
Hakika madaraka yake ni juu ya wanao mfanya rafiki
yao, na wale wanao fanya ushirika naye. 100

101. Na tunapo badilisha Ishara pahala pa Ishara
nyengine, na MwenyeziMungu anajua anayo teremsha, wao husema: Wewe ni mzushi.
Bali wengi wao hawajui kitu. 101

102. Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na
Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni
uwongofu, na ni bishara kwa Waislamu. 102

103. Na Sisi hakika tunajua kwamba wanasema: Yuko mtu
anaye mfundisha.Lugha ya huyo wanaye muelekezea ni ya kigeni, na hii ni lugha ya
Kiarabu mbayana. 103

104.
Hakika wasio ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu,
Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao watapata adhabu chungu. 104

105. Wanao zua uwongo ni wale tu wasio ziamini Ishara
za MwenyeziMungu. Na hao ndio waongo. 105

106. Anaye mkataa Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake
- isipo kuwa aliye lazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani,
lakini aliye kifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi
Mungu ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa. 106

107. Hayo ni kwa sababu wameyapenda zaidi maisha ya
duniani kuliko ya Akhera, na kwa sababu Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri. 107

108. Hao ndio Mwenyezi Mungu ameziziba nyoyo zao na
masikio yao na macho yao. Na hao ndio walio ghafilika. 108

109.
Hapana shaka ya kwamba hao ndio wenye kukhasiri
Akhera. 109

110. Kisha hakika Mola wako Mlezi, kwa wale walio hama
makwao baada ya kuteswa, kisha wakapigania Dini na wakasubiri, bila ya shaka
Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 110

111. Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, na kila
nafsi italipwa sawa sawa na a'mali ilizo zifanya, nao hawatadhulumiwa. 111

112. Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji ulio kuwa
na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini
ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la
njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyafanya. 112

113. Na alikwisha wajia Mjumbe wa miongoni mwao
wenyewe. Lakini wakamkanusha;basi iliwafika adhabu hali ya kuwa wamedhulumu. 113

114. Basi kuleni katika vile alivyo kupeni Mwenyezi
Mungu, vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema za Mwenyezi Mungu, ikiwa
kweli mnamuabudu Yeye. 114

115.
Amekuharimishieni nyamafu tu, na damu, na nyama ya
nguruwe,na mnyama aliye chinjwa kwa ajili isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu. Lakini
anaye lazimishwa bila ya kuasi, wala kuruka mipaka, basi hakika MwenyeziMungu ni
Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu. 115

116. Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu:
Hichi halali,na hichi haramu - mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanao
mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa. 116

117. Ni starehe ndogo, nao watapata adhabu chungu. 117

118. Na Mayahudi tuliwaharimishia yale tuliyo
kuhadithia zamani.Na Sisi hatukuwadhulumu, bali walikuwa wakijudhulumu wenyewe. 118

119. Kisha hakika Mola wako Mlezi kwa walio tenda uovu
kwa ujinga,kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila ya shaka Mola
wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu. 119

120.
Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu
kwa MwenyeziMungu, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina. 120

121.
Mwenye kuzishukuru neema zake, Mwenyezi Mungu.
Yeye kamteuwa,na akamwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. 121

122. Na tukampa wema duniani, na hakika Akhera atakuwa
miongoni mwa watu wema. 122

123. Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya
Ibrahim, mwongofu,wala hakuwa miongoni mwa washirikina. 123

124.
Hakika siku ya Sabato (Jumaamosi) waliwekewa wale
walio khitalifiana kwa ajili yake. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka
atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana. 124

125. Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa
hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola
wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye
wajua zaidi walio ongoka. 125

126. Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo
adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri. 126

127. Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu
ya MwenyeziMungu tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila
wanazozifanya. 127

128.
Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha,
na watendao mema. . 128
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani