Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni
kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza
kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi
Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwaangalieni. 1

2. Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe
kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni
jukumu kubwa. 2

3. Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima
uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na
mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu
ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.
3

4. Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni
kipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni
kiwashuke kwa raha. 4

5. Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo
Mwenyezi Mungu ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na
muwavike, na mseme nao maneno mazuri. 5

6. Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa.
Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa
watakuja kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri
basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu. 6

7. Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na
jamaa walio karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na
jamaa walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa.
7

8. Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na
mayatima na masikini, wapeni katika hayo mali ya urithi, na semeni nao maneno
mema. 8

9. Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha
nyuma yao watoto wanyonge wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na
waseme maneno yaliyo sawa. 9

10. Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma,
hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni. 10

11. Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu:
Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya
wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto
mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja
wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na
wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi
moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya
kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni
nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka
kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
11

12. Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa
hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya
wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha,
ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha,
baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye
rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila
mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi
watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio
kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi na Mpole. 12

13. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake,
wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa. 13

14. Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata
adhabu ya kudhalilisha. 14

15. Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake
wenu, washuhudizieni watu wane katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni
majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine.
15

16. Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na
wakitubia wakatengenea basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea
toba, Mwenye kurehemu. 16

17. Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya
wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi
Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima.
17

18. Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka
yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala
wale wanao kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.
18

19. Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake
kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa
wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi
huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.
19

20. Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali
mmoja wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je,
mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi? 20

21. Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi
kwa nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti? 21

22. Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo
kwisha pita. Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya. 22

23. Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada
zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa
dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa
wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake
zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia
mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa
pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 23

24. NA WANAWAKE wenye waume, isipo kuwa walio milikiwa
na mikono yenu ya kulia. Ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na
mmehalilishiwa wasio kuwa hao, mtafute kwa mali yenu kwa kuowa pasina kuzini.
Kama mnavyo starehe nao, basi wapeni mahari yao kwa kuwa ni waajibu. Wala hapana
lawama juu yenu kwa mtakacho kubaliana baada ya kutimiza waajibu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua na Mwenye hikima. 24

25. Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea
wanawake wa kiungwana Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki
mikono yenu ya kulia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa imani yenu. Nyinyi mmetokana
wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao
kama ada, wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapo olewa
kisha wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyo wekewa
waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni mwenu anaye ogopa kuingia katika zina. Na
mkisubiri ndio bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye
kurehemu. 25

26. Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na
kukuongozeni nyendo za walio kuwa kabla yenu, na akurejezeni kwenye ut'iifu
wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima. 26

27. Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye
ut'iifu wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko
makubwa.
27

28. Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na
mwanaadamu ameumbwa dhaifu. 28

29. Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma,
isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuwarehemuni. 29

30. Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhaalimu, basi
huyo tutamwingiza Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu. 30

31. Mkiyaepuka makubwa mnayo katazwa, tutakufutieni
makosa yenu madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu. 31

32. Wala msitamani alicho wafadhili Mwenyezi Mungu
baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake
wana fungu katika walio vichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. 32

33. Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyo
yaacha wazazi wawili na jamaa. Na mlio fungamana nao ahadi wapeni fungu lao.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu. 33

34. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa
na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa. Basi
wanawake wema ni wale wenye kut'ii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa
Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu
wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia
ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu. 34

35. Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na
mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na
jamaa za mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi Mwenye khabari. 35

36. Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na
chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na
jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na
walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye
kiburi wanao jifakhiri, 36

37. Ambao wanafanya ubakhili na wanaamrisha watu
ubakhili, na wanaficha fadhila alizo wapa Mwenyezi Mungu. Na tumewaandalia
makafiri adhabu ya fedheha, 37

38. Na ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu, wala
hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho; na yule ambaye Shet'ani amekuwa
ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya mno. 38

39. Na ingeli wadhuru nini wao lau wangeli muamini
Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wakatoa katika aliyo waruzuku Mwenyezi
Mungu? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua vyema. 39

40. Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu hata uzito wa chembe
moja. Na ikiwa ni jambo jema basi Yeye hulizidisha na hutoa kutoka kwake malipo
makubwa. 40

41. Basi itakuwaje pindi tukiwaletea kutoka kila umma
shahidi, na tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa? 41

42. Siku hiyo walio kufuru na wakamuasi Mtume watatamani
ardhi isawazishwe juu yao. Wala hawataweza kumficha Mwenyezi Mungu neno lolote.
42

43. Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa,
mpaka myajue mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini -
mpaka mkoge. Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni,
au mmewagusa wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake
nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye
kughufiria. 43

44. Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa,
mpaka myajue mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini -
mpaka mkoge. Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni,
au mmewagusa wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake
nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye
kughufiria. 44

45. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema maadui zenu. Na
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Mlinzi, na anatosha kuwa ni Mwenye kukunusuruni.
45

46. Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno
kuyatoa mahala pake, na husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya
kusikilizwa. Na husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao ili kuitukana Dini.
Na lau kama wangeli sema: Tumesikia na tumet'ii, na usikie na "Undhurna"
(Utuangalie), ingeli kuwa ni kheri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu
amewalaani kwa kufuru yao; basi hawaamini ila wachache tu. 46

47. Enyi mlio pewa Kitabu! Aminini tuliyo yateremsha
yenye kusadikisha yale mliyo nayo, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka
kisogoni, au tukawalaani kama tulivyo walaani watu wa Sabato (Jumaamosi). Na
amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima ifanyike 47

48. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na
husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu
basi hakika amezua dhambi kubwa 48

49. Jee huwaoni wale wanao dai kuwa ati wametakasika?
Bali Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kadiri ya
kijiuzi kilichomo ndani ya uwazi wa kokwa ya tende 49

50. Tazama vipi wanavyo mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na
haya yatosha kuwa dhambi iliyo dhaahiri. 50

51. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini
masanamu na Shet'ani! Na wanawasema walio kufuru, kuwa hao wameongoka zaidi
katika njia kuliko Walio amini. 51

52. Hao ndio Mwenyezi Mungu amewalaani. Na ambaye
Mwenyezi Mungu amemlaani basi hutamwona kuwa na mwenye kumnusuru 52

53. Au wanayo sehemu ya utawala? Basi hapo wasingewapa
watu hata tundu ya kokwa ya tende. 53

54. Au wanawahusudu watu kwa yale aliyo wapa Mwenyezi
Mungu kwa fadhila yake? Basi tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hikima na
tukawapa utawala mkubwa. 54

55. Basi wapo miongoni mwao waliyo yaamini, na wapo
walio yakataa. Na Jahannamu yatosha kuwa ni moto wa kuwateketeza 55

56. Hakika wale walio zikataa Ishara zetu tutawaingiza
Motoni. Kila zitapo wiva ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyengine ili waionje
hiyo adhabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 56

57. Na wale walio amini na wakatenda mema tutawaingiza
katika Pepo zipitazo mito kati yake kwa kudumu humo milele. Huko watakuwa na
wake walio takasika, na tutawaingiza katika vivuli vizuri kweli. 57

58. Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe
amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika
haya anayo kuwaidhini Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye kusikia, Mwenye kuona. 58

59. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini
Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi
lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku
ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema. 59

60. Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo
teremshwa kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia
ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea
mbali 60

61. Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo
yateremsha Mwenyezi Mungu, na njooni kwa Mtume; utawaona wanaafiki wanakukwepa
kwa upinzani 61

62. Basi inakuwaje unapo wasibu msiba kwa sababu ya yale
iliyo tanguliza mikono yao? Hapo tena hukujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu
wakisema: Hatukutaka ila wema na mapatano 62

63. Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo
ndani ya nyoyo zao. Basi waachilie mbali, uwape mawaidha na uwaambie maneno ya
kuathiri na kuingia katika nafsi zao. 63

64. Na hatukumtuma Mtume yeyote ila at'iiwe kwa idhini
ya Mwenyezi Mungu. Na lau pale walipo jidhulumu nafsi zao wangeli kujia,
wakamwomba Mwenyezi Mungu msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka
wangeli mkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu. 64

65. La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka
wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione
uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa. 65

66. Na lau kuwa tumewaamrisha: Jiueni, au tokeni
majumbani kwenu, wasingeli fanya hayo ila wachache tu miongoni mwao. Na lau kama
wangeli fanya walio waidhiwa ingeli kuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu
zaidi.

67. Na hapo tunge wapa malipo makubwa kutoka kwetu
67

68. Na tungeli waongoa Njia iliyo nyooka. 68

69. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa
pamoja na wale alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na
Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!
69

70. Hiyo ni fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kutosha. 70

71. Enyi mlio amini! Chukueni hadhari yenu! Na mtoke kwa
vikosi au tokeni nyote pamoja! 71

72. Na yupo kati yenu anaye bakia nyuma; na ukikusibuni
msiba husema: Mwenyezi Mungu kanifanyia kheri sikuwa nao. 72

73. Na ikikufikieni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema - kama kwamba hapakuwa mapenzi baina yenu naye: Laiti ningeli kuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio makubwa. 73

74. Basi nawapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu wale
ambao wanao uza uhai wa dunia kwa Akhera. Na anaye pigana katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kisha akauliwa au akashinda basi tutakuja mpa ujira mkubwa.
74

75. Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu
na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi
wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na
mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako
75

76. Walio amini wanapigana katika Njia ya Mwenyezi
Mungu, na walio kufuru wanapiana katika njia ya upotofu. Basi piganeni na
marafiki wa Shet'ani. Hakika hila za Shet'ani ni dhaifu 76

77. Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu,
na mshike Sala na mtoe Zaka. Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati
yao liliwaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi. Na
wakasema: Mola Mlezi wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge
tuakhirishia kiasi ya muda kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na
Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa
ya tende. 77

78. Popote mlipo mauti yatakufikieni, na hata mkiwa
katika ngome zilizo na nguvu. Na likiwafikilia jema wanasema: Hili limetoka kwa
Mwenyezi Mungu. Na likiwafikilia ovu wanasema: Hili limetoka kwako wewe. Sema:
Yote yanatokana na Mwenyezi Mungu. Basi wana nini watu hawa hata hawakaribii
kufahamu maneno? 78

79. Jema lilio kufikia limetokana na Mwenyezi Mungu. Na
ovu lilio kusibu linatokana na nafsi yako. Nasi tumekutuma kwa watu uwe ni
Mtume. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kutosha. 79

80. Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi
Mungu. Na anaye kengeuka, basi Sisi hatukukutuma wewe uwe ni mlinzi wao 80

81. Na wanasema: Tunat'ii. Lakini wanapo toka kwako
kundi moja miongoni mwao hupanga njama usiku kinyume na unayo yasema. Na
Mwenyezi Mungu anayaandika yote hayo wanayo yapangia njama za usiku. Basi
waachilie mbali, na umtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa
kutosha. 81

82. Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka
kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu
nyingi 82

83. Na linapo wafikia jambo lolote lilio khusu amani au
la kitisho wao hulitangaza. Na lau kuwa wangeli lipeleka kwa Mtume na kwa wenye
mamlaka kati yao, wale wanao chunguza wangeli lijua. Na lau kuwa si fadhila ya
Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngeli mfuata Shet'ani ila wachache wenu
tu. 83

84. Basi pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu.
Hukalifishwi ila nafsi yako tu. Na wahimize Waumini. Huenda Mwenyezi Mungu
akayazuia mashambulio ya walio kufuru. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mkali zaidi wa
kushambulia na Mkali zaidi wa kuadhibu. 84

85. Mwenye kusaidia msaada mwema ana fungu lake katika
hayo, na mwenye kusaidia msaada mwovu naye ana sehemu yake katika hayo. Na
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza na ujuzi juu ya kila kitu.. 85

86. Na mnapo amkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi
itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuhisabu kila kitu. 86

87. Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Kwa
yakini atakukusanyeni Siku ya Kiyama. Halina shaka hilo. Na ni nani msema kweli
kuliko Mwenyezi Mungu? 87

88. Mmekuwaje kuwa makundi mawili kwa khabari ya
wanaafiki, na hali Mwenyezi Mungu amewageuza kwa sababu ya yale waliyo yachuma?
Je! Mnataka kumwona mwongofu ambaye Mwenyezi Mungu amemhukumu kuwa kapotea? Na
aliye mhukumu Mwenyezi Mungu kuwa amekwisha potea wewe hutampatia njia 88

89. Wanapenda lau kuwa nanyi mnge kufuru kama walivyo
kufuru wao, ili muwe sawa sawa. Basi msiwafanye marafiki miongoni mwao mpaka
wahame kwa ajili ya Dini ya Mwenyezi Mungu. Na wakikengeuka basi wakamateni na
wauweni popote mnapo wapata. Wala msimfanye rafiki katika wao wala msaidizi
89

90. Isipokuwa wale walio fungamana na watu ambao mna
ahadi baina yenu na wao, au wanakujieni na vifua vyao vina dhiki kupigana nanyi,
au kupigana na watu wao. Na lau angeli penda Mwenyezi Mungu angeli wasaliti juu
yenu wakapigana nanyi. Basi wakijitenga nanyi, wasipigane nanyi, na
wakakuleteeni amani, basi Mwenyezi Mungu hakukupeni njia kupigana nao 90

91. Mtawakuta wengine wanataka wapate salama kwenu na
salama kwa watu wao. Kila wakirudishwa kwenye fitna hudidimizwa humo. Ikiwa
hawajitengi nanyi, na wakakuleteeni salama, na wakazuia mikono yao, basi
wakamateni na wauweni popote mnapo wakuta. Na juu ya hao ndio tumekupeni hoja
zilizo wazi 91

92. Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na
mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe
diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa
ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye
Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi
wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge
miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi na Mwenye hikima. 92

93. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo
yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani,
na amemuandalia adhabu kubwa. 93

94. Enyi mlio amini! Mnapo safiri katika Njia ya
Mwenyezi Mungu basi hakikisheni, wala msimwambie anaye kutoleeni salamu: Wewe si
Muumini; kwa kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi
Mungu zipo ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyo kuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi
Mungu akakuneemesheni. Basi chunguzeni sawa sawa. Hakika Mwenyezi Mungu anazo
khabari za mnayo yatenda 94

95. Hawawi sawa Waumini wanao kaa tu wala hawanadharura,
na wale wanao pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao.
Mwenyezi Mungu amewatukuza cheo wale wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao
kuliko wale wanao kaa tu. Ingawa Mwenyezi Mungu amewaahidi wote mashukio mema,
lakini Mwenyezi Mungu amewafadhili wanao pigana kwa ujira mkubwa kuliko wanao
kaa tu. 95

96. Ni vyeo hivyo vinavyo toka kwake, na maghfira na
rehema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye kurehemu. 96

97. Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha
nao wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa.
Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo?
Basi hao makaazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa. 97

98. Isipo kuwa wale walio kuwa wanyonge miongoni mwa
wanaume na wanawake na watoto wasio na uweza wa hila ya kuongoza njia ya kuhama.
98

99. Basi hao huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa maghfira 99

100. Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu
atapata pengi duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anaye toka nyumbani
kwake kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti
njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu 100

101. Na mnapo safiri katika nchi si vibaya kwenu kama
mkifupisha Sala, iwapo mnachelea wasije wale walio kufuru wakakuleteeni maudhi.
Hakika makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi. 101

102. Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi
moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo
maliza sijida zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo
halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio
kufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio
wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au
mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi
Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha. 102

103. Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu
mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni
Sala kama dasturi. Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati
maalumu 103

104. Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui.
Ikiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji
kwa Mwenyezi Mungu wasio yataraji wao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na
Mwenye hikima 104

105. Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki
ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyo kuonyesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe
mtetezi wa makhaaini. 105

106. Na muombe maghfira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu. 106

107. Wala usiwatetee wanao khini nafsi zao. Hakika
Mwenyezi Mungu hampendi aliye khaaini, mwenye dhambi. 107

108. Wanataka kujificha kwa watu, wala hawataki
kujificha kwa Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao pale wanapo panga njama usiku
kwa maneno asiyo yapenda. Na Mwenyezi Mungu anayajua vyema wanayo yatenda.
108

109. Hivyo nyinyi mmewatetea hawa katika uhai huu wa
duniani. Basi nani atakaye watetea kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama? Au ni nani
atakuwa wakili wao wa kumtegemea? 109

110. Na anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake,
kisha akaomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
maghfira, Mwenye kurehemu. 110

111. Na anaye chuma dhambi, basi ameichumia nafsi yake
mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima. 111

112. Na atendaye kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye
na kosa, basi amejitwika dhulma na dhambi iliyo wazi. 112

113. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako
na rehema yake, kundi moja kati yao linge dhamiria kukupoteza. Wala hawapotezi
ila nafsi zao, wala hawawezi kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu
amekuteremshia Kitabu na hikima na amekufundisha uliyo kuwa huyajui. Na fadhila
za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa. 113

114. Hakuna kheri katika mengi ya wanayo shauriana kwa
siri, isipo kuwa kwa yule anaye amrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au
kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi
Mungu, basi tutakuja mpa ujira mkubwa 114

115. Na anaye mpinga Mtume baada ya kumdhihirikia
uwongofu, na akafuata njia isiyo kuwa ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na
tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu. 115

116. Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na
kitu. Lakini Yeye husamehe yasiyo kuwa hayo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha
Mwenyezi Mungu basi huyo amepotea upotovu wa mbali. 116

117. Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala
hawamuombi ila Shet'ani aliye asi. 117

118. Mwenyezi Mungu amemlaani. Naye Shet'ani alisema:
Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako. 118

119. Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na
nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi
watabadili aliyo umba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni mlinzi
wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri. 119

120. Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shet'ani hawaahidi
ila udanganyifu. 120

121. Hao makao yao ni Jahannamu, na wala hawapati
makimbilio kutoka humo. 121

122. Na wale walio amini na wakatenda mema, tutawaingiza
katika Bustani zipitayo mito kati yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya
Mwenyezi Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu
122

123. Si kwa matamanio yenu, wala matamanio ya Watu wa
Kitabu! Anaye fanya ubaya atalipwa kwalo, wala hatajipatia mlinzi wala wa
kumnusuru, isipo kuwa Mwenyezi Mungu. 123

124. Na anaye fanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke,
naye ni Muumini - basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya
tundu ya kokwa ya tende. 124

125. Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliye
usilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa mwema, na anafuata mila ya
Ibrahim mwongofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwendani.
125

126. Ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni
na vilivyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuvizunguka vitu vyote.
126

127. Wanakuuliza nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi
Mungu ana kutoleeni fatwa juu yao, na mnayo somewa humu Kitabuni kukhusu
mayatima wanawake ambao hamwapi walicho andikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu
wanyonge katika watoto, na kwamba mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na kheri
yoyote mnayo fanya Mwenyezi Mungu anaijua. 127

128. Na mwanamke akichelea kutupwa au kutojaliwa na
mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi
zimewekewa machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamngu basi
hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda. 128

129. Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake, hata
mkikakamia. Kwa hivyo msimili moja kwa moja mkamwacha (mmojapo) kama aliye
tundikwa. Na mkisikizana na mkamchamngu basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
maghfira na Mwenye kurehemu. 129

130. Na wakitengana Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila
mmoja katika wao kwa ukunjufu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu Mwenye hikima.
130

131. Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote viliomo katik
mbingu na viliomo katika dunia. Na kwa hakika tuliwausia walio pewa Kitabu kabla
yenu, na nyinyi pia, kwamba mumche Mwenyezi Mungu. Na mkikataa, basi ni vya
Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi,
anajitosha, na Msifiwa. 131

132. Na ni vya Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na
viliomo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi. 132

133. Akitaka atakuondoeni, enyi watu! Na awalete
wengineo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa hayo 133

134. Anaye taka malipo ya dunia, basi kwa Mwenyezi Mungu
yapo malipo ya dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye
kuona. 134

135. Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu,
mtowao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa ni juu ya nafsi zenu, au
wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu
anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na
mkiupotoa au mkajitenga nao basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayo yatenda.
135

136. Enyi mlio amini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume
wake, na Kitabu alicho kiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alicho kiteremsha
kabla yake. Na anaye mkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na
Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi huyo amekwisha potelea mbali. 136

137. Hakika walio amini, kisha wakakufuru, kisha
wakaamini, kisha wakazidi ukafiri, Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaghufiria wala wa
kuwaongoa njia. 137

138. Wabashirie wanaafiki kwamba watapata adhabu chungu,
138

139. Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki
badala ya Waumini. Je! Wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni
wa Mwenyezi Mungu. 139

140. Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya
kwamba mnapo sikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli,
basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa
nanyi mfano wao hao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanaafiki na makafiri
wote pamoja katika Jahannamu. 140

141. Wale ambao wanakungojeeni, mkipata ushindi unao
toka kwa Mwenyezi Mungu wao husema: Si tulikuwa pamoja nanyi vile? Na ikiwa ni
sehemu ya makafiri kushinda wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kukushindeni,
nasi tukakukingeni na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu
Siku ya Kiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda
Waumini. 141

142. Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na
hali ni Yeye ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa
unyong'onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila
kidogo tu. 142

143. Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako
na huko hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompatia
njia. 143

144. Enyi mlio amini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio
marafiki badala ya Waumini. Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyo wazi
juu yenu? 144

145. Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini
kabisa Motoni, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru. 145

146. Isipo kuwa wale walio tubu, na wakatengeneza na
wakashikamana na Mwenyezi Mungu, na wakamtakasia Dini yao Mwenyezi Mungu. Basi
hao ni pamoja na Waumini. Na Mwenyezi Mungu atakuja wapa Waumini ujira mkubwa.
146

147. Mwenyezi Mungu hakuadhibuni mkimshukuru na
mkamuamini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea shukrani na ndiye Mwenye
kujua. 147

148. MWENYEZI MUNGU hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila
kwa mwenye kudhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
148

149. Mkidhihirisha wema au mkiuficha, au mkiyasamehe
maovu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Muweza. 149

150. Hakika wale wanao mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume
wake, na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, kwa
kusema: Wengine tunawaamini na wengine tunawakataa. Na wanataka kushika njia
iliyo kati kati ya haya. 150

151. Hao ndio makafiri kweli. Na tumewaandalia makafiri
adhabu ya kudhalilisha. 151

152. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake,
wala wasimfarikishe yeyote kati yao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwingi wa maghfira, na Mwenye kurehemu 152

153. Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshia kitabu
kutoka mbinguni. Na kwa hakika walikwisha mtaka Musa makubwa kuliko hayo.
Walisema: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi. Wakapigwa na radi kwa hiyo dhulma
yao. Kisha wakamchukua ndama kumuabudu, baada ya kwisha wajia hoja zilizo wazi.
Nasi tukasamehe hayo, na tukampa Musa nguvu zilizo dhaahiri. 153

154. Na tukanyanyua mlima juu yao kwa kufanya agano nao.
Na tukawaambia: Ingilieni mlangoni kwa unyenyekevu. Na tukawaambia: Msiivunje
Siku ya Sabato (Jumaa mosi). Na tukachukua kwao ahadi iliyo madhubuti. 154

155. Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi zao, na
kuzikataa kwao ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa kwao Manabii bila ya haki,
na kusema kwao: Nyoyo zetu zimefumbwa; bali Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri kwa
kufuru zao, basi hawaamini ila kidogo tu 155

156. Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu
uwongo mkubwa. 156

157. Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa,
mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu,
bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika
shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala
hawakumuuwa kwa yakini 157

158. Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 158

159. Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini
yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao 159

160. Basi kwa dhulma yao Mayahudi tuliwaharimishia vitu
vizuri walivyo halalishiwa. Na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na Njia
ya Mwenyezi Mungu. 160

161. Na kuchukua kwao riba, nao wamekatazwa, na kula
kwao mali ya watu kwa dhulma. Basi tumewaandalia makafiri katika wao adhabu
yenye uchungu. 161

162. Lakini walio bobea katika ilimu miongoni mwao, na
Waumini, wanayaamini uliyo teremshiwa wewe, na yaliyo teremshwa kabla yako. Na
wanao shika Sala, na wakatoa Zaka, na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho - hao tutawapa malipo makubwa. 162

163. Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo
wapelekea wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi
Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus
na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi. 163

164. Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na
Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno.
164

165. Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu
wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 165

166. Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyo
kuteremshia wewe. Ameyateremsha kwa kujua kwake - na Malaika pia wanashuhudia.
Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi. 166

167. Hakika walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu, wamekwisha potelea mbali. 167

168. Hakika wale walio kufuru na wakadhulumu hawi
Mwenyezi Mungu kuwasamehe wala kuwaongoa njia. 168

169. Isipo kuwa njia ya Jahannamu. Humo watadumu milele.
Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. 169

170. Enyi Watu! Amekwisha kujieni Mtume huyu na haki
itokayo kwa Mola wenu Mlezi. Basi aminini, ndiyo kheri yenu. Na mkikakanusha
basi hakika viliomo mbinguni na duniani ni vya Mwenyezi Mungu tu. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima 170

171. Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini
yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa mwana
wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu,
na ni roho iliyo toka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala
msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu
mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliomo katika
mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha 171

172. Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi
Mungu, wala Malaika walio karibishwa. Na watakao ona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi
Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake. 172

173. Na ama walio amini na wakatenda mema atawalipa
ujira wao sawa sawa, na atawazidishia kwa fadhila yake. Na ama wale walio ona
uvunjifu na wakafanya kiburi, basi atawaadhibu adhabu iliyo chungu. Wala
hawatopata mlinzi wala wa kuwanusuru asiye kuwa Mwenyezi Mungu. 173

174. Enyi watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola
wenu Mlezi. Na tumekuteremshieni Nuru iliyo wazi. 174

175. Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu, na
wakashikamana naye, basi atawatia katika rehema yake na fadhila, na atawaongoa
kwenye Njia Iliyo Nyooka. 175

176. Wanakuomba uhukumu, sema: Mwenyezi Mungu anakupeni
hukumu juu ya mkiwa. Ikiwa mtu amekufa, naye hana mtoto, lakini anaye ndugu wa
kike, basi huyo atapata nusu alicho acha maiti. Na mwanamume atamrithi ndugu wa
kike ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni ndugu wa kike wawili, basi watapata
thuluthi mbili za alicho acha maiti. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi
mwanamume atapata sehemu iliyo sawa na ya wanawake wawili. Mwenyezi Mungu
anakubainishieni ili msipotee; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. 176
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright © 22
August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani