Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. T'A SIN MIM 1

2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. 2

3.
Tunakusomea khabari za Musa na Firauni kwa Haki kwa
ajili ya watu wanao amini. 3

4. Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa
wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao,
akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye
alikuwa katika mafisadi. 4

5. Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi
hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi. 5

6. . Na kuwapa nguvu katika nchi, na kutokana na wao
kuwaonyesha kina Firauni na Hamana na majeshi yao mambo yale waliyo kuwa
wakiyaogopa. 6

7.
Tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia:
Mnyonyeshe. Na utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike.
Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume. 7

8. Basi wakamwokota watu wa Firauni, aje kuwa adui kwao
na huzuni. Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa. 8

9. Na mkewe Firauni alisema: Atakuwa kiburudisho cha
macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mwenetu. Wala
wao hawakutambua. 9

10. . Na moyo wa mama yake Musa ukawa mtupu. Alikuwa
karibu kumdhihirisha, ingeli kuwa hatukumtia nguvu moyo wake ili awe miongoni
mwa Waumini. 10

11. . Naye akamwambia dada yake Musa: Mfuatie. Basi
naye akawa anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua. 11

12. Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu
mwanzo, mpaka dada yake akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea
kwa ajili yenu, nao pia watakuwa wema kwake? 12

13. Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake
yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya
kweli, lakini wengi wao hawajui. 13

14. Na Musa alipo fika utu-uzima baraabara, tulimpa
akili na ilimu. Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema. 14

15. Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji
wake, na akakuta humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na
mwengine katika maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake.
Musa akampiga ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet'ani; hakika
yeye ni adui, mpotezaji dhaahiri. 16

16.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi
nimejidhulumu nafsi yangu; basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu. 16

17.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Kwa ulivyo nineemesha,
basi mimi sitakuwa kabisa msaidizi wa wakosefu. 18

18.
Akapambazukiwa mjini asubuhi naye ana khofu,
akiangalia huku na huku. Mara yule yule aliye mtaka msaada jana akawa anampigia
kelele amsaidie. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mgomvi kweli kweli. 18

19. Basi alipo taka kumshika kwa nguvu yule aliye adui
wao wote wawili, akasema: Ewe Musa! Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana?
Wewe hutaki ila kuwa jabari katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wenye
maslaha.. 19

20. Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akipiga mbio,
akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanashauriana kukuuwa. Basi toka! Hakika mimi ni
katika wanao kupa nasaha. 20

21. . Basi akatoka, naye ana khofu, akiangalia huku na
huku. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niokoe na watu madhaalimu. 21

22. Na alipo elekea upande wa Madyana alisema: Asaa
Mola wangu Mlezi akaniongoa njia iliyo sawa. 22

23. Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa
watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia
wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao
wachunga. Na baba yetu ni mzee sana. 23

24. Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na
akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayo niteremshia. 24

25. Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia,
naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea.
Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwisha okoka
kwenye watu madhaalimu. 25

26. Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu!
Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu. 26

27.
Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti
zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako;
lakini mimi sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema. 27

28. Musa akasema: Hayo yamekwisha kuwa baina yangu na
wewe. Muda mmojapo nikiumaliza sitiwi ubayani. Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu
ya haya tunayo yasema. 28

29. Basi alipo timiza muda wake na akasafiri na ahali
zake, aliona moto upande wa Mlima T'uri. Akawaambia ahali zake: Ngojeni! Mimi
nimeona moto, labda nitakuleteeni kutoka huko khabari au kijinga cha moto ili
mpate kuota moto. 29

30. Basi alipo ufikia aliitwa kutoka ng'ambo ya bonde
la kuliani katika eneo lilio barikiwa kutoka kwenye mti: Ewe Musa! Hakika Mimi
ni Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. 30

31. Na tupa chini fimbo yako. Basi alipo iona
ikitikisika kama nyoka, akarudi nyuma wala hakutazama. (Akaambiwa): Ewe Musa!
Njoo mbele wala usiogope. Hakika wewe ni miongoni mwa walio salimika. 
32. Ingiza mkono wako kwenye mfuko wako, utatoka mweupe
pasipo na ubaya. Na jiambatishe mkono wako ukihisi khofu. Basi hizi ni dalili
mbili zitokazo kwa Mola wako Mlezi kumpelekea Firauni na wakuu wa umma wake.
Hakika hao walikuwa watu mafaasiki. 
33. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nilimuuwa
mtu katika wao, kwa hivyo naogopa wataniuwa. 
34. Na ndugu yangu Harun ni fasihi zaidi ulimi wake
kuliko mimi. Basi mtume ende nami kunisaidia, ili anisadikishe. Hakika mimi nina
khofu watanikadhibisha. 
35. (Mwenyezi Mungu) akasema: Tutautia nguvu mkono wako
kwa nduguyo, na tutakupeni madaraka, hata wasikufikilieni. Kwa sababu ya Ishara
zetu nyinyi na watakao kufuateni mtashinda. 
36. Basi alipo wafikia Musa na Ishara zetu, walisema:
Haya si chochote ila ni uchawi ulio zuliwa. Na hatukuyasikia haya kwa baba zetu
wa zamani. 
37. Na Musa akasema: Mola wangu Mlezi ni Mwenye kujua
kabisa nani anaye kuja na uwongofu unao toka kwake, na nani atakaye kuwa na
mwisho mwema wa makaazi. Hakika wenye kudhulumu hawatafanikiwa. 
38. Na Firauni akasema: Enyi waheshimiwa! Sijui kama
mnaye mungu asiye kuwa mimi. Ewe Haman! Niwashie moto unichomee udongo,
unijengee mnara nipate kumchungulia mungu wa Musa. Na hakika mimi namwona yeye
ni katika waongo. 
39. Na alipanda kiburi yeye na majeshi yake katika nchi
bila ya haki, na wakadhania kuwa hawatarudishwa kwetu. 
40. Basi tukamshika yeye na majeshi yake, na tukawatupa
baharini. Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa wenye kudhulumu? 
41. . Na tuliwafanya ni waongozi waitao kwenye Moto. Na
Siku ya Kiyama hawatanusuriwa. 41

42. Na tukawafuatishia laana katika dunia hii, na Siku
ya Kiyama watakuwa miongoni mwa wanao chusha. 42

43. Na hakika bila ya shaka tulimpa Musa Kitabu baada
ya kwisha ziangamiza kaumu za mwanzo, ili kiwafumbue macho watu, na kiwe
uwongofu, na rehema, ili wapate kukumbuka. 43

44. . Wala wewe hukuwa upande wa magharibi tulipo mpa
Musa amri, wala hukuwa katika walio hudhuria. 44

45. Lakini Sisi tuliziumba kaumu, na ukawa mrefu umri
juu yao. Wala hukuwa mkaazi na watu wa Madyana ukiwasomea Aya zetu. Lakini ni
Sisi tulio kuwa tukiwatuma Mitume. 45

46. Wala hukuwa kando ya mlima tulipo nadi. Lakini ni
rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio pata kufikiwa na
mwonyaji kabla yako, huenda wakakumbuka. 46

47. Na usije kuwasibu msiba kwa iliyo yatanguliza
mikono yao, wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Mbona hukututumia Mtume nasi,
tukafuata Ishara zako, na tukawa miongoni mwa Waumini? 47

48. Ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema: Mbona
hakupewa kama aliyo pewa Musa? Je! Kwani wao hawakuyakataa aliyo pewa Musa
zamani? Walisema: Ni wachawi wawili wanasaidiana. Na wakasema: Hakika sisi
tunawakataa wote. 48

49. Sema: Basi leteni Kitabu kinacho toka kwa Mwenyezi
Mungu chenye kuongoka zaidi kuliko hivi viwili tukifuate, kama nyinyi mnasema
kweli. 49

50. Na ikiwa hawakuitikii, basi jua kuwa wanafuata
pumbao lao tu. Na nani aliye potea zaidi kumshinda anaye fuata pumbao lake bila
ya uwongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
wenye kudhulumu. 50

51. Na sasa kwa yakini tumewafikishia Neno ili wapate
kukumbuka. 51

52. Wale tulio wapa Kitabu kabla yake wanakiamini hiki.
52

53. Na wanapo somewa wanasema: Tunaiamini. Hakika hii
ni Haki inayo toka kwa Mola wetu Mlezi. Hakika sisi kabla yake tulikuwa ni
Waislamu, tulio nyenyekea. 53

54. . Basi hao watapewa ujira wao mara mbili kwa
walivyo vumilia, na wakaondoa ubaya kwa wema, na wakatoa katika tuliyo waruzuku.
54

55. Na wanapo sikia upuuzi hujitenga nao na husema:
Sisi tuna vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu. Salamun Alaikum, Amani juu
yenu! Sisi hatutaki kujibizana na wajinga. 55

56. Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye, lakini
Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na Yeye ndiye anawajua zaidi waongokao. 56

57. Na wakasema: Tukiufuata uwongofu huu pamoja nawe
tutanyakuliwa kutoka nchi yetu. Je! Kwani Sisi hatukuwaweka imara katika pahala
patakatifu, penye amani, ambapo huletewa matunda ya kila aina kuwa ni riziki
itokayo kwetu? Lakini wengi wao hawajui. 57

58. Na miji mingapi iliyo jifakharisha tumeiangamiza!
Na hayo maskani yao hayakukaliwa tena baada yao, ila kwa uchache tu. Na Sisi
ndio tumekuwa warithi wao. 58

59. . Na Mola wako Mlezi haangamizi miji mpaka ampeleke
Mtume katika miji yake mikuu awasomee Ishara zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka
watu wake wawe madhaalimu. 59

60. .. Na chochote mlicho pewa ni matumizi ya maisha ya
dunia na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayo baki
zaidi. Basi je, hamfahamu? 60

61. Je! Yule tuliye muahidi ahadi nzuri, tena naye
akayapata, ni kama tuliye mstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani, na kisha
Siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanao hudhurishwa? 
62. Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi mlio
kuwa mkidai kuwa ni washirika wangu? 
63. Watasema wale iliyo thibiti juu yao kauli: Mola
wetu Mlezi! Hawa ndio tulio wapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyo potea sisi.
Tunajitenga nao mbele yako. Hawakuwa wakituabudu sisi. 
64. . Na itasemwa: Waiteni hao miungu wa kishirikina
wenu! Basi watawaita, lakini hawatawaitikia, na wataiona adhabu; laiti wangeli
kuwa wameongoka! 
65. Na siku atapo waita na akasema: Mliwajibu nini
Mitume? 
66. Basi zitawapotea khabari siku hiyo, nao
hawataulizana. 
67. Ama mwenye kutubu na akaamini na akatenda mema,
huyo atakuwa miongoni mwa wenye kufanikiwa. 
68. Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo.
Viumbe hawana khiari. Mwenyezi Mungu ametukuka na ametakasika na hao wanao
washirikisha naye. 
69. Na Mola wako Mlezi anayajua yaliyo ficha vifua
vyao, na wanayo yatangaza. 
70. . Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo
kuwa Yeye. Sifa zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake
Yeye. Na kwake Yeye mtarejeshwa. 
71. Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku
umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi
Mungu atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii? 71

72. Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana
umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi
Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni? 72

73. Na ni katika rehema zake amekufanyieni usiku na
mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru. 73

74. Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi hao
mlio kuwa mkidai kuwa ni washirika wangu? 74

75. Na tutatoa shahidi katika kila umma, na tutasema:
Leteni hoja zenu! Hapo watajua kwamba hakika kweli ni ya Mwenyezi Mungu, na
yatawapotea yale waliyo kuwa wakiyazua. 75

76. Hakika Qaruni alikuwa katika watu wa Musa, lakini
aliwafanyia dhulma. Na tulimpa khazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu
wenye nguvu kuzichukua. Walipo mwambia watu wake: Usijigambe! Hakika Mwenyezi
Mungu hawapendi wanao jigamba. 76

77. Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi
ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi
Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi.
Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi. 77

78. . Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya
ilimu niliyo nayo. Je! Hakujua kwamba Mwenyezi Mungu kesha waangamiza, katika
vizazi vya walio kabla yake, watu walio kuwa wenye ngubvu zaidi kuliko yeye, na
wenye makundi makubwa zaidi kuliko yake. Na wakosefu hawataulizwa khabari ya
dhambi zao. 78

79. Basi akawatokea watu wake katika pambo lake.
Wakasema wale walio kuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungeli kuwa tunayo
kama aliyo pewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa. 79

80. Na wakasema wale walio pewa ilimu: Ole wenu! Malipo
ya Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Wala hawatapewa
hayo isipo kuwa wenye subira. 80

81. Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake katika
ardhi; wala halikuwepo kundi lolote la kumnusuru kwa Mwenyezi Mungu, wala hakuwa
miongoni mwa wanao jitetea. 81

82. Na wale walio tamani kuwa pahala pake jana, wakawa
wanasema: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na
humdhikisha amtakaye. Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutufanyia hisani angeli
tudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi! 82

83. Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale
wasio taka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu. 83

84. Atakaye tenda wema atapata malipo bora kuliko huo
wema alio utenda. Na atakaye tenda uovu, hawalipwi watendao uovu ila waliyo kuwa
wakiyatenda. 84

85. Hakika aliye kulazimisha kuifuata Qur'ani hapana
shaka atakurudisha pahala pa marejeo. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye mjua
zaidi mwenye kuja na uwongofu, na nani aliyomo katika upotofu ulio dhaahiri. 85

86. Nawe hukuwa unataraji kuletewa Kitabu; lakini ni
rehema tu ya Mola wako Mlezi. Basi usiwe msaidizi wa makafiri. 86

87. Wala wasikuzuie kuzifuata Aya za Mwenyezi Mungu
baada ya kuteremshiwa wewe. Na lingania kwa Mola wako Mlezi, wala usiwe miongoni
mwa washirikina. 87

88. Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu
mwenginewe. Hapana mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipo kuwa Yeye. Hukumu
iko kwake, na kwake mtarejezwa. 88
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani