Tarjuma ya Quran Tukufu kwa
kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1. Ewe uliye jifunika! 1

2. Kesha usiku kucha, ila kidogo tu! 2

3. Nusu yake, au ipunguze kidogo. 3

4. Au izidishe - na soma Qur'ani kwa utaratibu na
utungo. 4

5. ka Hakika Sisi tutakuteremshia uli nzito. 5

6. Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo, na
maneno yake yanatua zaidi. 6

7. Kwani hakika mchana una shughuli nyingi. 7

8. Na lidhukuru jina la Mola wako Mlezi, na ujitolee
kwake kwa ukamilifu. 8

9. Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, hapana mungu
isipo kuwa Yeye, basi mfanye kuwa Mtegemewa wako. 9

10. Na vumilia hayo wayasemayo, na jitenge nao kwa
vizuri. 10

11. Na niache Mimi na hao wanao kanusha, walio neemeka;
na wape muhula kidogo! 11

12.
Hakika Sisi tunazo pingu nzito na Moto unao waka
kwa ukali kabisa! 12

13. Na chakula kinacho kwama kooni, na adhabu inayo
umiza. 13

14. Siku ambayo ardhi itatikiswa na milima pia, na
milima itakuwa kama tifutifu la mchanga. 14

15.
Hakika Sisi tumemtuma kwenu Mtume aliye shahidi juu
yenu, kama tulivyo mtuma Mtume kwa Firauni. 15

16.
Lakini Firauni alimuasi huyo Mtume, basi tukamshika
mshiko wa mateso. 16

17. Basi nyinyi mkikufuru, mtawezaje kujikinga na Siku
ambayo itawafanya watoto wadogo waote mvi? 17

18. Hapo mbingu zitapasuka! Ahadi yake itakuwa
imetekelezwa. 18

19. Kwa hakika hili ni kumbusho. Mwenye kutaka atashika
njia ya kwendea kwa Mola wake Mlezi. 19


20. Hakika Mola wako Mlezi anajua ya kuwa hakika wewe
unakesha karibu na thuluthi mbili za usiku, na nusu yake, na thuluthi yake. Na
baadhi ya watu walio pamoja nawe kadhaalika. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye
ukadiria usiku na mchana. Anajua kuwa hamwezi kuweka hisabu, basi amekusameheni.
Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani. Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa
wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi
Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo someni
kilicho chepesi humo, na mshike Sala, na toeni Zaka, na mkopesheni Mwenyezi
Mungu mkopo mwema. Na kheri yoyote mnayo itanguliza kwa ajili ya nafsi zenu
mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana. Na
mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu. 20
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani