Tarjuma ya Quran Tukufu kwa
kiswahili

KWA JINA
LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1.
Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa
wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa
Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni
waongo. 1

2.
Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia
kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa
wakiyafanya. 2

3. Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha
wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu
lolote. 3

4. Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema,
unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania
kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi
Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki? 4

5. Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu
akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa
kiburi. 5

6. Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia
maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
wapotovu. 6

7. Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya
walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu
ndiye Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu. 7

8.
Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila
ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu -
Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui. 8

9. Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala
watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio
khasiri. 9

10. Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia
mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo
nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema? 10

11.
Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote
inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
11
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani