Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
0

1.
MWENYEZI MUNGU amekwisha sikia usemi wa mwanamke
anaye jadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia,
Mwenye kuona. 1

2. Wale miongoni mwenu wanao watenga wake zao, hao si
mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale walio wazaa. Na hakika hao wanasema neno
linalo chusha, na la uwongo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye
kusamehe. 2

3. Na wale wanao jitenga na wake zao, kisha wakarudia
katika yale waliyo yasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa
maonyo kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu anayajua yote mnayo yatenda. 3

4. Na asiye pata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi
miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiye weza hayo basi awalishe masikini
sitini. Hayo ni hivyo ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ndiyo
mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na kwa makafiri iko adhabu chungu. 4

5.
Hakika wanao pinzana na Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, watadhalilishwa kama walivyo dhalilishwa wale walio kuwa kabla yao. Na
tulikwisha teremsha Ishara zilizo wazi. Na makafiri watapata adhabu ya
kufedhehesha. 5

6. Siku atapo wafufua Mwenyezi Mungu, na awaambie yale
waliyo yatenda. Mwenyezi Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau! Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu. 6

7. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo
katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye
huwa ni wane wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache
kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo.
Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
wa kila kitu. 7

8. Kwani huwaoni wale walio katazwa kunong'onezana
kisha wakayarudia yale yale waliyo katazwa, na wakanong'ona juu ya mambo ya
dhambi, na ya uadui, na ya kumuasi Mtume? Na wakikujia hukuamkia sivyo anavyo
kuamkia Mwenyezi Mungu. Na husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi hatuadhibu
kwa haya tuyasemayo? Basi Jahannamu itawatosha; wataingia humo! Na hayo ndiyo
marejeo maovu yaliyoje! 8

9. Enyi mlio amini! Mnapo nong'ona msinong'one kwa
sababu ya mambo ya madhambi, na uadui, na kumuasi Mtume. Bali nong'onezane kwa
kutenda mema na kuacha maovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa
nyote. 9

10.
Kwa hakika minong'ono hiyo inatokana na Shetani ili
awahuzunishe walio amini, na wala haitawadhuru chochote ila kwa idhini ya
Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu tu ndio wategemee Waumini. 10

11.
Enyi mlio amini! Mkiambiwa: Fanyeni nafasi katika
mabaraza, basi fanyeni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi. Na
mkiambiwa: Ondokeni, basi ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua walio amini
miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo
khabari za mnayo yatenda. 11

12.
Enyi mlio amini! Mnapo sema siri na Mtume, basi
tangulizeni sadaka kabla ya kusemezana kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi
zaidi. Na ikiwa hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu. 12

13.
Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya
kusemezana kwenu? Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu,
basi shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. 13

14.
Huwaoni wale walio fanya urafiki na watu ambao
Mwenyezi Mungu amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na
huapa kwa uwongo, na hali kuwa wanajua. 14

15.
Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika
waliyo kuwa wakiyatenda ni maovu kabisa. 15

16.
Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya
Mwenyezi Mungu. Basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha. 16

17.
Hayatawafaa kitu mali yao wala watoto wao mbele ya
Mwenyezi Mungu. Hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu milele. 17

18.
Siku atakayo wafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuwapie
kama wanavyo kuwapieni nyinyi. Na watadhani kuwa wamepata kitu! Kwa hakika hao
ndio waongo. 18

19.
Shetani amewatawala na akawasahaulisha kumkumbuka
Mwenyezi Mungu. Hao ndio kundi la Shetani. Kweli hakika kundi la Shetani ndilo
lenye kukhasirika. 19

20.
Hakika wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
hao ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho. 20

21.
Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na
Mtume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.
21

22.
Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku
ya Mwisho kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata
wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika
katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza
katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe
radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi la Mwenyezi Mungu.
Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa. 22
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii [email protected]
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani