Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Alif Lam Mim 1

2. Hizi ni Aya za Kitabu chenye hikima. 1

3. Kuwa ni Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema, 3

4. Wanao shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na
Akhera. 4

5. Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi,
na hao ndio wenye kufanikiwa. 5

6. Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya
upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na
wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha. 6

7. Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo
kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi.
Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu. 7

8. Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa nazo
Bustani za neema. 8

9. Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli.
Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 9

10.
Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na
ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila
namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika
ardhi mimea mizuri ya kila namna. 10

11. Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni
wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo
dhaahiri. 11

12. Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru
Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi
yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa. 12

13. Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha:
Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya
shaka ni dhulma iliyo kubwa. 13

14. Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake
ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya
miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo
marudio. 14

15. Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna
ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya
anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni
mliyo kuwa mkiyatenda. 15

16. Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya
khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi
Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika,
Mwenye khabari za yote. 16

17. Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza
maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. 17

18. Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa
maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha. 18

19. Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako.
Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda. 19

20. Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya
vikutumikieni viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za
dhaahiri na za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi
Mungu pasipo ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru. 20

21. Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa
Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao? 21

22. Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu,
naye akawa anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio
madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu. 22

23. Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu
ndio marudio yao, na hapo tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi wa yaliyomo vifuani. 23

24.
Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma
kwenye adhabu ngumu. 24

25. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi?
Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema
zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui. 25

26. Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na
katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa. 26

27. Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni
kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba,
maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
nguvu, Mwenye hikima. 27

28.
Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni
kama nafsi moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona. 28

29. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku
katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi?
Vyote hivyo vinakwenda mpaka wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari
za mnayo yatenda. 29

30. Hivi ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa
kweli, na hakika wanacho kiomba ni cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu
ndiye Mtukufu na ndiye Mkubwa. 30

31. Kwani huoni kwamba marikebu hupita baharini
zikichukua neema za Mwenyezi Mungu, ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake?
Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri, mwenye kushukuru. 31

32. Na wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba
Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo
baadhi yao huenda mwendo wa sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini
kafiri mkubwa. 32

33. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku
ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi
ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala
asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu mdanganyifu. 33

34. Hakika kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi
Mungu. Na Yeye ndiye anaye iteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo
ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui
itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari. 34
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani