Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU
MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi vinamtakasa
Mwenyezi Mungu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 1

2. Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua
kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa
kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri. 2

3. Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye
ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 3

4. Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayo mpa
amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa. 4

5. Mfano wa walio bebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni
mfano wa punda anaye beba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu walio
kadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu. 5

6. Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa
ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu pasipo kuwa watu wengine, basi yatamanini mauti,
ikiwa mnasema kweli. 6

7. Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyo
kwisha yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua walio dhulumu.
7

8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia, bila ya shaka
yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo
onekana. Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda. 8

9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa,
nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora
kwenu, lau kama mnajua. 9

10. Na itakapo kwisha Sala, tawanyikeni katika nchi
mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili
mpate kufanikiwa. 10

11. Na wanapo iona biashara au pumbao wanayakimbilia
hayo na wakakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko
pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki. 11
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani