Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la
majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu!
1

2. Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini,
wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi. 2

3. Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka
kabisa; hana mke wala mwana. 3

4. Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa
wakisema uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu. 4

5. Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo
Mwenyezi Mungu. 5

6. Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa
wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi.
6

7. Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani
nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume. 7

8. Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi
wenye nguvu na vimondo. 8

9. Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya
makao ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo
kinamvizia! 9

10. Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa
kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu. 10

11. Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine
wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali. 11

12. Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu
duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia. 12

13. Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye
kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa. 13

14. Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati
yetu wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu.
14

15. Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za
Jahannamu. 15

16. Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia
tungeli wanywesha maji kwa wingi, 16

17. Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka
Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu. 17

18. Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi
msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu. 18

19. Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama
kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga! 19

20. Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala
simshirikishi Yeye na yeyote. 20

21. Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala
kukuongozeni. 21

22. Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na
Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu. 22

23. Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na
risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao
watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele. 23

24. Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo
jua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi. 24

25. Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au
Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu. 25

26. Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala
hamdhihirishii yeyote siri yake, 26

27. Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo
humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake. 27

28. Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola
wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila
kitu. 28
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani