Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. H'a Mim 1

2.
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye
nguvu, Mwenye hikima. 2

3. Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini.
3

4. Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya
zimo Ishara kwa watu wenye yakini. 4

5. Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo
iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa
kwake, na mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili. 5

6. Hizi Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi
hadithi gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake? 6

7. Ole wake kila mzushi mwenye dhambi! 7

8. Anaye sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha
anashikilia yale yale aliyo katazwa, na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi
mbashirie adhabu chungu! 8

9. Na anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia
mzaha. Watu hao ndio watakao kuwa na adhabu ya kufedhehesha. 9

10. Na nyuma yao ipo Jahannamu. Na walio yachuma
hayatawafaa hata kidogo, wala walinzi walio washika badala ya Mwenyezi Mungu. Na
watapata adhabu kubwa. 10

11. Huu ni uwongofu. Na wale wale walio zikataa Ishara za
Mola wao Mlezi watapata adhabu inayo tokana na ghadhabu iliyo chungu. 11

12.
Mwenyezi Mungu ndiye aliye ifanya bahari
ikutumikieni, ili humo zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila
yake, na mpate kushukuru. 12

13. Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na
vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa
watu wanao fikiri. 13

14.
Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji
siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma. 14

15.
Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake,
na mwenye kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu
Mlezi. 15

16. Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu
na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko
walimwengu wote. 16

17. Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi
hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa
baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika
mambo waliyo kuwa wakikhitalifiana. 17

18. Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi
ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu. 18

19. Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni
rafiki wa wamchao. 19

20. Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni
uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha. 20

21. Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama
walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya
wanayo ihukumu! 21

22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki,
na ili kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa. 22

23. Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye
mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na
akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni
mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki? 23

24. Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani -
twafa na twaishi, na hapana kinacho tuhiliki isipo kuwa dahari. Lakini wao
hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu. 24

25. Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila
kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasemao kweli. 25

26. Sema: Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha
anakufisheni, kisha anakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu
wengi hawajui. 26

27. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na
ardhi. Na siku itapo simama Saa ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye
kushikamana na upotovu. 27

28. Na utauona kila umma umepiga magoti, na kila umma
utaitwa kwenda soma kitabu chake: Leo mtalipwa mliyo kuwa mkiyatenda. 28

29. Hichi kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki.
Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyo kuwa mkiyatenda. 29

30. Ama walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi
atawatia katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi. 30

31. Na ama walio kufuru, wataambiwa: Kwani hamkuwa
mkisomewa Aya zangu nanyi mkapanda kichwa, na mkawa watu wakosefu? 31

32. Na ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni
kweli, na Saa haina shaka, nyinyi mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana
tu, wala hatuna yakini. 32

33. Basi ubaya wa waliyo yatenda utawadhihirikia, na
yatawazunguka waliyo yafanyia maskhara. 33

34. Na itasemwa: Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyo
sahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa
kukunusuruni. 34

35. Hayo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za
Mwenyezi Mungu; na maisha ya dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo
wala hao hawatakubaliwa udhuru wao. 35

36. Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola
Mlezi wa mbingu, na Mola Mlezi wa ardhi, na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
36

37. Na ukubwa ni wake Yeye tu, mbinguni na katika ardhi,
naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 37
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani