Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili
17.Surat Al-Israai (Bani
Israil) |

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku
mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo
uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia
na Mwenye kuona. 1

2. Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa
Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi! 2

3. Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika
yeye alikuwa mja mwenye shukrani. 3

4. Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu
kwamba: Hakika nyinyi mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini
mtapanda kiburi, kiburi kikubwa.4

5. Basi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni
waja wetu wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa
ahadi iliyo timizwa. 5

6. Kisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na
tukakusaidieni kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi.6

7. Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na
mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu
nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu
kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa.7

8. Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na
Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri. 8

9. Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka
kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo
makubwa. 9

10. Na yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia
adhabu chungu. 10

11. Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo
kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa. 11

12. Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili.
Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza
ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka
na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi. 12

13. Na kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake.
Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa.13

14.
Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha
leo kukuhisabu. 14

15. Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi
yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi
mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume.15

16. Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale
wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo
kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.16

17. Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na
Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja
wake. 17

18. Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka
kumletea hapa hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu;
ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa. 18

19. Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali
zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa.19

20. Wote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika
neema za Mola wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki.20

21. Angalia vipi tulivyo wafadhili baadhi yao kuliko
wenginewe. Na hakika Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi. 21

22.
Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu,
usije ukawa wa kulaumiwa uliye tupika. 22

23. Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu
yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee,
naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na
sema nao kwa msemo wa hishima.23

24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea
huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.24

25. Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa
nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake. 25

26. Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na
msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo. 26

27.
Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru
Mola wake Mlezi. 27

28. Na ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta rehema
ya Mola wako Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini. 28

29.
Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala usiukunjue
wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi.29

30. Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye,
na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona. 30

31.
Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na
nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa.31

32. Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na
njia mbaya.32

33.
Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na
aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite
mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa. 33

34. Wala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa kwa
njia iliyo bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi
itasailiwa.34

35.
Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema
kwenu na khatimaye ndio bora. 35

36. Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika
masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa. 36

37.
Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi
wala kufikia urefu wa milima. 37

38 Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola
wako Mlezi. 38

39.
Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja
na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na
kufurushwa. 39

40. Je! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana, na Yeye
akawafanya Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi mkubwa.40

41.
Na tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii ili wapate kukumbuka. Lakini
haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo.41

42.
Sema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo, basi
wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi. 42

43.
Subhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka juu
kabisa na hayo wanayo yasema. 43

44.
Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana
kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake.
Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira. 44

45. Na unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako na wale
wasio iamini Akhera pazia linalo wafunika. 45

46.
Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka kwenye
masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi
wao hugeuka nyuma wakenda zao.46

47.
Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo kusikiliza, na
wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati isipo kuwa mtu
aliye rogwa.47

48.
Tazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea. Kwa hivyo hawawezi
kuipata njia. 48

49. Na walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande
yaliyo vurugika, tutafufuliwa kwa umbo jipya?49

50.
Sema: Kuweni hata mawe na chuma.50

51. Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua
vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni
mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa
yakawa karibu! 51

52.
iku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia kwa kumshukuru, na mkadhani kuwa
hamkukaa ila muda mdogo tu.52

53. Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana
Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa
mwanaadamu.53

54.
Mola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda atakurehemuni, na akipenda
atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao. 54

55. Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo
mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko
wengine; na Daudi tulimpa Zaburi.55

56.
Sema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake Yeye. Hawawezi kukuondoleeni
madhara, wala kuyaweka pengine.56

57. Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya
kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji
rehema zake na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa
kutahadhari nayo. 57

58.
Na hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza kabla ya Siku ya Kiyama, au
tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa katika Kitabu. 58

59. Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni
kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni
Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa
ajili ya kuhadharisha. 59

60.
Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka hao watu. Na
hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa
katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa. 60

61.
Na pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam. Wakamsujudia isipo kuwa
Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba kwa udongo? 61

62.
Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza
juu yangu. Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza
dhuriya zake wasipo kuwa wachache tu. 62

63.
Akasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali! Atakaye kufuata katika wao, basi
Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo ya kutimia. 63

64. Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na
wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao
katika mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu. 64

65.
Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa
ni wa kutegemewa. 65

66. Mola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni marikebu
katika bahari ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye
kukurehemuni nyinyi. 66

67.
Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipo
kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni
mwingi wa kukanusha. 67

68. Je! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni upande
wowote katika nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto? Kisha msipate
wa kumtegemea. 68

69.
Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na kukupelekeeni
kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha msipate wa
kukunusuruni nasi. 69

70. Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya
kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na
tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba. 70

71.
Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi
atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao
wala hawatadhulumiwa hata chembe. 71

72. Na aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu
Akhera, na atakuwa aliye ipotea zaidi Njia. 72

73.
Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili utuzulie
mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki.73

74. Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia
kuwaelekea kidogo. 74

75.
Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya uhai, na adhabu
mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu wa kukunusuru nasi. 75

76. Na walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na hapo wao
wasingeli bakia humo ila kwa muda mchache tu. 76

77.
Huo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla yako. Wala hupati mabadiliko
katika mwendo wetu77

78. Shika Sala jua linapo pinduka mpaka giza la usiku,
na Qur'ani ya al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa daima.78

79.
Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe. Huenda Mola
wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika.79

80. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema,
na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie.80

81.
Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke! 81

82. Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu
na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara.82

83.
Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga kando. Na inapo mgusa
shari hukata tamaa.83

84. Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga
kando. Na inapo mgusa shari hukata tamaa. 84

85.
Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu
Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu.85

86. Na tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia.
Kisha usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya.86

87.
Isipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika fadhila yake kwako
ni kubwa.87

88. Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete
mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.88

89.
Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano. Lakini watu
wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu.89

90.
Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika ardhi hii.90

91. Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na
utupitishie mito kati yake ikimiminika. 91

92.
Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi
Mungu na Malaika uso kwa uso. 92

93. Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala
hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi,
Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na
Mtume?93

94.
Na nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo wajia uwongofu isipo kuwa
walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu kuwa ni Mtume? 94

95. Sema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea
kwa utulivu wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni Mtume
wao. 95

96.
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika
Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona. 96

97. Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye
hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya
Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na
viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi
kuuchochea uwake kwa nguvu.97

98.
Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na wakasema: Hivyo
tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa umbo jipya? 98

99. Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba
mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio
na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri. 99

100.
Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola wangu Mlezi,
basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu
tangu hapo tabia yake ni mchoyo! 100

101. Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo
wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi
nakuona wewe Musa umerogwa! 101

102.
Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha ila Mola
Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila
ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia. 102

103. Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa
hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote. 103

104.
Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi. Itapo kuja
ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja. 104

105. Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka.
Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji.105

106.
Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na
tumeiteremsha kidogo kidogo.106

107.
Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanapo
somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu 107

108. Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola
wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe! 108

109.
Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu. 109

110.
Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni
Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina
mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa
sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo. 110

111.
Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye hana mwana,
wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa kumsaidia kwa sababu ya
udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa. 111
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani