Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Laam Miim.

2. Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye Aliye Hai,
Msimamizi wa yote milele.

3.
Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinacho sadikisha
yaliyo kuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili

4. Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha
Furqani (Upambanuo). Hakika walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa na
adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa.

5. Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki chochote kwake,
duniani wala mbinguni.

6. Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi
kwa namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

7. Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake
zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko
nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za
mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana
yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema:
Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo
isipo kuwa wenye akili.

8. (Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo
zetu baada ya kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye
Mpaji.

9. Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye Mkusanyaji wa watu kwa
Siku isiyo na shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.

10. Kwa hakika wale walio kufuru hazitowafaa kitu kwa
Mwenyezi Mungu mali zao, wala watoto wao; nao hao ndio kuni za Motoni.

11. Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio
kuwa kabla yao. Walikanusha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa
madhambi yao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

12. Waambie walio kufuru: Karibuni mtashindwa na
mtakusanywa, mtiwe kwenye Jahannam; nako huko ni makao mabaya kabisa.

13. Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi
mawili yalipo pambana. Jeshi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na
jingine kafiri likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na
Mwenyezi Mungu humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo
mazingatio kwa wenye macho.

14. Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na
wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba.
Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo
mema.

15. Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa
wachamngu ziko Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na
wake walio takaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuwaona waja wake.

16. Ambao husema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi
tumeamini, basi tufutie madhambi yetu, na tuepushe na adhabu ya Moto,

17. Wanao subiri, wanao sema kweli, na wat'iifu, na
wanao toa sadaka, na wanao omba maghafira kabla ya alfajiri.

18. Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu,
wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha
uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

19. Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni
Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa
sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu
basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

20. Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha
uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie
walio pewa Kitabu na wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka.
Na wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuwaona waja wake.

21. Hakika wanao zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na
wakawauwa Manabii pasipo haki, na wakawauwa watu waamrishao Haki wabashirie
adhabu kali.

22. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika duniani na
Akhera. Nao hawatapata wa kuwanusuru.

23. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaitwa
kukiendea Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao; kisha baadhi yao
wanageuka wanakikataa.

24. Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa Moto isipo
kuwa kwa siku chache tu. Na yakawadanganya katika dini yao yale ambayo wenyewe
waliyo kuwa wakiyazua.

25. Basi itakuwaje tutakapo wakusanya Siku ambayo haina
shaka kuja kwake? Na kila nafsi italipwa kama ilivyo chuma, bila ya kudhulumiwa.

26. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote!
Wewe humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza
umtakaye, na humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni
Muweza wa kila kitu.

27. Wewe huingiza usiku katika mchana, na huuingiza
mchana katika usiku. Na humtoa hai kutokana na maiti, na humtoa maiti kutokana
na aliye hai. Na unamruzuku umtakaye bila ya hisabu.

28. Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala
ya Waumini. Na anaye fanya hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi
Mungu. Ila ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu
anakuhadharisheni naye. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

29. Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyafichua
Mwenyezi Mungu anayajua; na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo duniani. Na
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

30. Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya
yamehudhurishwa, na pia ubaya ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako masafa
marefu baina ya ubaya huo na yeye. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na
Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.

31. Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi
nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.

32. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka
basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.

33. Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo
wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.

34. Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia na Mwenye kujua.

35. Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi!
Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika
Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

36. Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa
mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa - Na mwanamume si sawa na
mwanamke. Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake,
uwalinde na Shet'ani aliye laaniwa.

37. Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na
akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya
alipo ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu!
Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi
Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

38. Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi,
akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia
maombi.

39. Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika
kamnadia: Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria Yahya, ataye kuwa mwenye
kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa
watu wema.

40. Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata
mwana na hali ukongwe umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo
hivyo, Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.

41. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema:
Alama yako ni kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu.
Na mdhukuru Mola Mlezi wako kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi.

42. Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu!
Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko
wanawake wote.

43. Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu
na uiname pamoja na wainamao.

44. Hizi ni khabari za ghaibu tunazo kufunulia; nawe
hukuwa nao walipo kuwa wakitupa kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa
nao walipo kuwa wakishindana.

45. Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika
Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni
Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni
mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).

46. Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika
utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema.

47. Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata
mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo,
Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa.

48. Na atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na
Injili.

49. Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi
nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa
udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti
kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba
katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye
kuamini.

50. Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika
Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni
na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na
nit'iini mimi.

51. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola
wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

52. Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema:
Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni
wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi
hakika ni Waislamu.

53. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyo yateremsha, na
tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.

54. Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu
akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.

55. Pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi
nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na
nitawaweka wale walio kufuata juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama.
Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa
mkikhitalifiana.

56. Ama wale walio kufuru, nitawaadhibu adhabu kali
katika dunia na Akhera, wala hawatapata wa kuwanusuru.

57. Na ama wale walio amini na wakatenda mema basi
Mwenyezi Mungu atawalipa ujira wao kaamili. Na Mwenyezi Mungu hawapendi
madhaalimu.

58. Haya tunayo kusomea ni katika Aya na Ukumbusho wenye
hikima.

59. Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano
wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa.

60. Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe
miongoni mwa wanao fanya shaka.

61. Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia
ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na
wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu
tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo.

62. Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu
ila Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye
hikima.

63. Na kama wakigeuka basi Mwenyezi Mungu anawajua
waharibifu.

64. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio
sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala
tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi
badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi
ni Waislamu.

65. Enyi Watu wa Kitabu! Mbona mnabishana juu ya
Ibrahim, na hali Taurati na Injili hazikuteremshwa ila baada yake? Basi
hamzingatii?

66.
Angalieni! Nyinyi mlibishana katika yale mliyo
yajua. Mbona sasa mnabishana katika yale msiyo yajua? Na Mwenyezi Mungu ndiye
ajuaye, na nyinyi hamjui.

67. Ibrahim hakuwa Yahudi wala Mkristo, lakini alikuwa
mwongofu Muislamu, wala hakuwa katika washirikina.

68. Watu wanao mkaribia zaidi Ibrahim ni wale walio
mfuata yeye na Nabii huyu na walio amini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa
Waumini.

69. Kipo kikundi katika Watu wa Kitabu wanao penda
kukupotezeni; lakini hawapotezi ila nafsi zao, nao wenyewe hawatambui.

70. Enyi Watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa Ishara za
Mwenyezi Mungu ilhali nyinyi mnashuhudia?

71. Enyi Watu wa Kitabu! Mbona kweli mnaivisha uwongo,
na kweli mnaificha na hali mnajua?

72. Na kikundi katika Watu wa Kitabu walisema: Yaaminini
yale waliyo teremshiwa wenye kuamini mwanzo wa mchana, na yakataeni mwisho wake;
huenda wakarejea.

73. Wala msimuamini ila anaye fuata dini yenu. Sema:
Hakika uwongofu ni uwongofu wa Mwenyezi Mungu, kuwa apewe mtu mfano wa mlio pewa
nyinyi au wakuhojini mbele ya Mola wenu Mlezi. Sema: Hakika fadhila zimo
mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa
na Mjuzi.

74. Yeye humchagua kumpa rehema zake amtakaye; na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kubwa.

75. Na miongoni mwa Watu wa Kitabu yupo ambaye ukimpa
amana ya mrundi wa mali atakurudishia, na miongoni mwao yupo ambaye ukimpa amana
ya dinari moja hakurudishii isipo kuwa ukimsimamia kumdai. Haya ni kwa kuwa
wakisema: Hatuna lawama kwa ajili ya hawa wasio jua kusoma. Na wanamzulia uwongo
Mwenyezi Mungu, hali nao wanajua.

76. Sivyo hivyo, bali anaye timiza ahadi yake na
akamchamngu basi Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu.

77. Hakika wanao uza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo
vyao thamani ndogo, hao hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala
Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa,
nao watapata adhabu chungu.

78. Na wapo baadhi yao wanao pindua ndimi zao katika
kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki
Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa
Mwenyezi Mungu. Na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na wao wanajua.

79. Haiwezi kuwa mtu aliye pewa na Mwenyezi Mungu Kitabu
na hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya
Mwenyezi Mungu. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe
vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma.

80.Wala hatakuamrisheni kuwafanya Malaika na Manabii
kuwa ni miungu. Je, atakuamrisheni ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?

81. Na pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa
Manabii: Nikisha kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye
kusadikisha mliyo nayo, ni juu yenu mumuamini na mumsaidie. Akasema: Je, mmekiri
na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema:
Basi shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia.

82. Watakao geuka baada ya haya basi hao ndio wapotovu.

83. Je, wanataka dini isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu, na
hali kila kilichomo mbinguni na katika ardhi kimesilimu kwa kumt'ii Yeye
kikipenda kisipende, na kwake Yeye watarejeshwa?

84. Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyo
teremshiwa sisi, na aliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na
wajukuu zao, na aliyo pewa Musa na Isa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao
Mlezi. Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake.

85. Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu
haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.

86. Mwenyezi Mungu atawaongoaje watu walio kufuru baada
ya kuamini kwao, na wakashuhudia ya kuwa Mtume huyu ni wa haki, na zikawafikia
hoja zilizo wazi? Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.

87. Hao malipo yao ni kuwa ipo juu yao laana ya Mwenyezi
Mungu na ya Malaika na ya watu wote.

88. Humo watadumu. Hawatapunguziwa adhabu wala
hawatapewa nafasi.

89. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na
wakatengenea; kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.

90. Hakika wale walio kufuru baada ya kuamini kwao,
kisha wakazidi kukufuru, toba yao haitakubaliwa, na hao ndio walio potea.

91. Hakika wale walio kufuru, na wakafa hali ni makafiri
haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau
wangeli itoa. Hao watapata adhabu chungu, wala hawatakuwa na wa kuwanusuru.

92. KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo
vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.

93. Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israili
isipo kuwa alicho jizuilia Israili mwenyewe kabla haijateremshwa Taurati. Sema:
Leteni Taurati muisome ikiwa nyinyi ni wasema kweli.

94. Na wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo,
basi hao ndio madhaalimu.

95. Sema: Mwenyezi Mungu amesema kweli. Basi fuateni
mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.

96. Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada
ni ile iliyoko Bakka, iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote.

97. Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya
Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya
kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu.

98. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha
ishara za Mwenyezi Mungu, na ilhali kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi kwa yote
mnayo yatenda?

99. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia aliye
amini Njia ya Mwenyezi Mungu mkiitafutia kosa, na hali nyinyi mnashuhudia? Na
Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda.

100. Enyi mlio amini! Mkiwat'ii baadhi ya walio pewa
Kitabu watakurudisheni kuwa makafiri baada ya Imani yenu.

101. Na vipi mkufuru hali nyinyi mnasomewa Aya za
Mwenyezi Mungu na Mtume yuko kati yenu? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu
basi huyo ameongozwa kwenye Njia Iliyo Nyooka.

102. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama
ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.

103. Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote
pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu:
vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa
neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni
nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.

104. Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri
na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa.

105. Wala msiwe kama wale walio farikiana na
kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na
adhabu kubwa.

106. Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zitasawijika.
Ama hao ambao nyuso zao zitasawijika wataambiwa: Je! Mlikufuru baada ya kuamini
kwenu? Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mnakufuru.

107. Ama wale ambao nyuso zao zitanawiri watakuwa katika
rehema ya Mwenyezi Mungu. Wao humo watadumu.

108. Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki.
Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu walimwengu.

109. Na kila kilichomo mbinguni na kilichomo ardhini ni
cha Mwenyezi Mungu; na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu.

110. Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa
kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau
kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao
waumini, lakini wengi wao wapotovu.

111. Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na
wakipigana nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa.

112.
Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo
kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu. Na wakastahiki ghadhabu
ya Mwenyezi Mungu, na wamepigwa na unyonge. Hayo ni kwa sababu walikuwa
wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasina haki; hayo ni
kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka.

113. Wote hao si sawa sawa. Miongoni mwa Watu wa Kitabu
wamo watu walio simama baraabara, wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za
usiku, na pia wanasujudu.

114.
Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na
wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanakimbilia katika mambo ya kheri. Na
hao ndio miongoni mwa watenda mema.

115. Na kheri yoyote wanayo ifanya hawatanyimwa malipwa
yake. Na Mwenyezi Mungu anawajua wachamngu.

116. Hakika wale walio kufuru hazitawafaa kitu mali zao
wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio watu wa Motoni - humo
watadumu.

117. Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa
duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la
watu walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu,
bali wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao.

118. Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio
kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo kudhuruni.
Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni
makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia akilini.

119. Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala
wao hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema:
Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni
kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani.

120.
Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari
wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.

121. Na pale ulipo toka asubuhi, ukaacha ahali zako
uwapange Waumini kwenye vituo kwa ajili ya vita - na Mwenyezi Mungu anasikia na
anajua.

122.
Makundi mawili miongoni mwenu yakaingiwa na woga
kuwa watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao; na Waumini
wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.

123. Na Mwenyezi Mungu alikwisha kunusuruni katika Badri
nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.

124. Ulipo waambia Waumini: Je, haitakutosheni ikiwa
Mola wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tatu walio teremshwa?

125. Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata
maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa
Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu.

126. Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni
bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa
Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

127. Haya ni kwa ajili awakate sehemu katika walio
kufuru, au awahizi wapate kurejea nyuma nao wamepwelewa.

128. Wewe huna lako jambo katika haya - ama atawahurumia
au atawaadhibu, kwani wao ni madhaalimu.

129. Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika
mbingu na vilivyomo katika ardhi. Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye. Na
Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye kurehemu.

130. Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu,
na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.

131. Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya
makafiri.

132. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate
kurehemewa.

133. Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na
Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu,

134. Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na
dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu
huwapenda wafanyao wema;

135. Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu
nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na
nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na
waliyo yafanya na hali wanajua.

136. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na
Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao.

137. Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni
katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanao kanusha.

138. Hii ni bayana kwa watu wote, na ni uwongofu, na
mawaidha kwa wachamngu.

139. Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio
wa juu mkiwa ni Waumini.

140. Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu
wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu
kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu
mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu;

141. Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na
awafutilie mbali makafiri.

142. Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu
hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio
subiri?

143. Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana
nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama.

144. Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita
kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye
geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
atawalipa wanao mshukuru.

145. Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya
Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya
duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye
kushukuru.

146. Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini
wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi
Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda
wanao subiri.

147. Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu
Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na
isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri.

148. Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na
bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.

149. Enyi mlio amini! Ikiwa mtawat'ii walio kufuru
watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri.

150. Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye
bora wa wasaidizi.

151.
Tutazitia khofu nyoyo za walio kufuru kwa vile
walivyo mshirikisha Mwenyezi Mungu na washirika ambao hakuwateremshia hoja
yoyote. Na makaazi yao ni Motoni; na maovu yaliyoje maskani ya wenye kudhulumu!

152. Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile
mlivyo kuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipo legea na mkazozana juu ya
amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu
wanao taka dunia, na wapo miongoni mwenu wanao taka Akhera. Kisha akakutengeni
nao (maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwisha kusameheni. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye fadhila juu ya Waumini.

153. Pale mlipo kuwa mkikimbia mbio wala hamumsikilizi
yeyote, na Mtume anakuiteni, yuko nyuma yenu. Mwenyezi Mungu akakupeni dhiki juu
ya dhiki, ili msisikitike kwa yaliyo kukoseeni wala kwa yaliyo kusibuni. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.

154. Kisha baada ya dhiki alikuteremshieni utulivu -
usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jengine nafsi zao
ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyo kuwa ya haki,
dhana ya kijinga. Wakisema: Hivyo tuna lolote sisi katika jambo hili? Sema:
Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyo kubainishia.
Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusinge uliwa hapa. Sema:
Hata mngeli kuwa majumbani mwenu, basi wangeli toka walio andikiwa kufa, wakenda
mahali pao pa kuangukia wafe.(Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu
yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu
anayajua yaliyomo vifuani.

155. Hakika wale walio rudi nyuma miongoni mwenu siku
yalipo pambana majeshi mawili, Shet'ani ndiye aliye watelezesha kwa sababu ya
baadhi ya makosa waliyo yafanya; na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.

156. Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio kufuru na
wakawasema ndugu zao walipo safiri katika nchi au walipo kuwa vitani: Wangeli
kuwa kwetu wasingeli kufa na wasingeli uwawa. Ili Mwenyezi Mungu afanye hayo
kuwa ni majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.

157. Na pindi mkiuliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au
mkifa, hakika maghfira na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yote
wanayo yakusanya.

158. Na mkifa au mkiuliwa ni kwa Mwenyezi Mungu ndio
mtakusanywa.

159. Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi
Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila
ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao
katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika
Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea.

160.
Akikunusuruni Mwenyezi Mungu hapana wa
kukushindeni, na akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye ataye kunusuruni? Na
Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.

161. Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na
atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha
kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.

162. Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni
kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa
Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea.

163. Hao wana vyeo mbali mbali kwa Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote wayatendayo.

164. Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa
Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya
zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo
walikuwa katika upotovu ulio wazi.

165. Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi
mmekwisha watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo
umetoka kwenu wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

166. Na yaliyo kusibuni siku yalipo pambana majeshi
mawili yalikuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ili awajue Waumini.

167. Na ili awapambanue walio kuwa wanaafiki,
wakaambiwa: Njooni mpigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu au lindeni. Wakasema:
Tungeli jua kuna kupigana bila ya shaka tungeli kufuateni. Wao siku ile walikuwa
karibu na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao yasiyo kuwamo nyoyoni
mwao. Na Mwenyezi Mungu anajua kabisa wanayo yaficha.

168. Hao ndio walio waambia ndugu zao na wao wenyewe
wakakaa kitako: Lau wengeli tut'ii wasingeli uliwa. Sema: Ziondoleeni nafsi zenu
mauti kama mnasema kweli.

169. Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao
Mlezi.

170.
Wanafurahia aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila
yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya
kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

171.
Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu,
na ya kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa Waumini.

172. Walio mwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya
kwisha patwa na majaraha - kwa walio fanya wema miongoni mwao na wakamchamngu
utakuwa ujira mkubwa.

173. Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni,
waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye
ni mbora wa kutegemewa.

174. Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi
Mungu. Hapana baya lilio wagusa, na wakafuata yanayo mridhi Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.

175. Hakika huyo ni Shet'ani anawatia khofu marafiki
zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini.

176. Wala wasikuhuzunishe wale wanao kimbilia ukafirini.
Hakika hao hawamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee
sehemu yoyote katika Akhera, na yao wao adhabu kubwa.

177. Hakika wale walio nunua ukafiri kwa Imani
hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na yao wao ni adhabu chungu.

178. Wala wasidhani wale wanao kufuru kwamba huu muhula
tunao wapa ni kheri yao. Hakika tunawapa muhula wazidi madhambi. Na yao wao ni
adhabu ya kuwadhalilisha.

179. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha Waumini katika
hali mliyo nayo mpaka apambanue wabaya na wema. Wala haiwi kwa Mwenyezi Mungu
kukujuulisheni mambo ya ghaibu. Lakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume wake
amtakaye. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake. Na mkiamini na
mkamchamngu mtakuwa na ujira mkubwa.

180. Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika
aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni
shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili Siku ya Kiyama.
Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anazo
khabari za yote myatendayo.

181.
Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya walio sema:
Mwenyezi Mungu ni masikini, na sisi ni matajiri. Tumeyaandika waliyo yasema, na
pia kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni
adhabu ya kuungua.

182.
kuwadhuluHaya ni kwa sababu ya iliyo tanguliza
mikono yenu, na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye mu waja.

183. Walio sema: Mwenyezi Mungu ametuahidi tusimuamini
Mtume yeyote mpaka atuletee kafara inayo teketezwa na moto. Waambie: Walikujieni
Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa hayo mnayo sema, basi kwa nini
mkawauwa ikiwa mlikuwa wakweli?.

184. Na wakikukanusha basi walikanushwa Mitume wengine
kabla yako walio kuja na hoja waziwazi na Vitabu vyenye hikima, na Kitabu chenye
nuru.

185. Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa
ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi
basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu.

186. Hapana shaka yoyote mtapata misukosuko katika mali
zenu na nafsi zenu, na bila ya shaka yoyote mtasikia udhia mwingi kutokana na
walio pewa Kitabu kabla yenu na wale walio shiriki. Na ikiwa mtasubiri na
mkamchamngu basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia.

187. Na pale Mwenyezi Mungu alipo fungamana na walio
pewa Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa
nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho
walicho nunua.

188.
Usiwadhanie kabisa wale wanao furahia waliyo
yafanya, na wakapenda kusifiwa kwa wasiyo yatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika
na adhabu. Yao wao ni adhabu chungu.

189. Na Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu;
na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu

190. Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na
kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili.

191. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na
wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola
wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu
ya Moto.

192. Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi;
na walio dhulumu hawana wasaidizi.

193. Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye
kuita akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi
tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu
wema.

194. Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume
wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi.

195. Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu:
Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke,
kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na
wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi
nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita
mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu kwake yapo malipo mema kabisa.

196. Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa
walio kufuru katika nchi.

197. Hiyo ni starehe ndogo. Kisha makaazi yao yatakuwa
Jahannamu. Na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia.

198. Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata Mabustani
yanayo pita mito kati yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa
Mwenyezi Mungu. Na vilioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema.

199. Hakika miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na
yaliyo teremshwa kwenu na yaliyo teremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu.
Hawabadili Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani duni. Hao wana ujira wao kwa Mola
wao Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

200. Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri,
na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa.
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii
qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani