Tarjuma ya Quran Tukufu kwa
kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Enyi mlio amini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia, Mwenye kujua. 1

2. Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti
ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyo semezana nyinyi kwa nyinyi,
visije vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui. 2

3. Kwa hakika wanao teremsha sauti zao mbele ya Mtume wa
Mwenyezi Mungu, hao ndio Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Hao
watakuwa na maghfira na ujira mkubwa. 3

4. Hakika hao wanao kuita nawe uko nyuma ya vyumba,
wengi wao hawana akili. 4

5. Na lau wao wangeli ngojea mpaka uwatokee ingeli kuwa
kheri kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu. 5

6. Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari
yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye
kujuta kwa mliyo yatenda. 6

7. Na jueni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nanyi. Lau
angeli kut'iini katika mambo mengi, bila ya shaka mngeli taabika. Lakini
Mwenyezi Mungu amekupendezeeni Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na
amekufanyeni muuchukie ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walio ongoka,
7

8. Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. 8

9. Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana,
basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni
linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi
yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu
anawapenda wanao hukumu kwa haki. 9

10.
Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya
ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe. 10

11. Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume
wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora
kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni
uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye
kudhulumu. 11

12. Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani
baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa
nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa?
Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kupokea toba, Mwenye kurehemu. 12

13. Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na
mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane.
Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu
zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.
13

14.
Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini,
lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii
Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 14

15.
Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli. 15

16.
Sema: Ati ndio mnamfundisha Mwenyezi Mungu Dini
yenu, na hali Mwenyezi Mungu anayajua ya katika mbingu na ardhi, na Mwenyezi
Mungu anajua kila kitu? 16

17.
Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie
kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyieni hisani kwa
kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli. 17

18.
Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na
ardhi. Na Mwenyezi Mungu anayaona myatendayo. 18
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani