Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE
KUREHEMU. 0

15. Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na
Qur'ani inayo bainisha. 1

2. HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa
Waislamu. 2

3. Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa.
Watakuja jua. 3

4. Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na
muda wake maalumu. 4

5. Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala
kuchelewa. 5

6. Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika
wewe ni mwendawazimu. 6

7. Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa
wasemao kweli? 7

8. Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki,
na hapo hawatapewa muhula. 8

9. Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na
hakika Sisi ndio tutao ulinda. 9

10. Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya
mwanzo. 10

11. Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli. 11

12. Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za
wakosefu. 12

13.
Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia
mfano wa watu wa kale. 13

14. Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa
wanapanda, 14

15. Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi
wenyewe tumerogwa. 15

16. Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari,
na tumezipamba kwa wenye kuangalia. 16

17. Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye. 17

18. Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye
hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana. 18

19. Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na
tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. 19

20. Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya
hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. 20

21. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na
Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu. 21

22. Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na
tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si
nyinyi mnayo yaweka. 22

23. Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi
ndio Warithi. 23

24. Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na
tunawajua waliotaakhari. 24

25. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya.
Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi. 25

26. Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao
tokana na matope yaliyo tiwa sura. 26

27. Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.
27

28. Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika
Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa
sura. 28

29. Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho
yangu, basi mumwangukie kumsujudia. 29

30. Basi Malaika wote pamoja walimsujudia, 30

31. Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na
walio sujudu. 31

32.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata
hukuwa pamoja na walio sujudu? 32

33. Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa
udongo unaotoa sauti, unao tokana na matope yenye sura. 33

34.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani
hakika wewe ni maluuni! 34

35. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo. 35

36. Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula
mpaka siku watapofufuliwa. 36

37.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika
walio pewa muhula 37

38. Mpaka siku ya wakati maalumu. 38

39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia
makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote, 39

40. Ila waja wako walio safika. 40

41. Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka. 41

42. Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu
yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata. 42

43. Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo
ahidiwa wote. 43

44. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu
walio tengewa. 44

45. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na
chemchem. 45

46.
(Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani. 46

47. Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe
ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana. 47

48. Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo. 48

49. Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu. 49

50. Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu! 50

51. Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim. 51

52. Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye
akasema: Hakika sisi tunakuogopeni. 52

53.
Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana
mwenye ujuzi. 53

54. Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi
kwa njia gani mnanibashiria? 54

55.
Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe
miongoni mwa wanaokata tamaa. 55

56. Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola
wake Mlezi ila wale walio potea? 56

57. Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe? 57

58.
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya
wakosefu! 58

59. Isipo kuwa walio mfuata Luut'i. Bila ya shaka sisi
tutawaokoa hao wote. 59

60. Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao
bakia nyuma. 60

61. Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut'i, 61

62. Alisema (Luut'i): Hakika nyinyi ni watu msio
juulikana. 62

63.
Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa
wakiyafanyia shaka. 63

64. Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema
kweli. 64

65. Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe
ufuate nyuma yao,wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa.
65

66. Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa
mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali. 66

67. Na wakaja watu wa mji ule nao furahani. 67

68. Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi
msinifedheheshe. 68

69. Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi. 69

70.
Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote?
70

71. Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni
watendaji. 71

72. Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika
ulevi wao, wakihangaika ovyo. 72

73. Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa. 73

74. Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua
ya mawe ya udongo wa Motoni. 74

75. Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi. 75

76. Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa. 76

77. Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini. 77

78. Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini. 78

79. Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko
kwenye njia iliowazi. 79

80. Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha
Mitume. 80

81. Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza. 81

82. Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa
amani. 82

83. Basi ukelele ukawatwaa asubuhi. 83

84.
Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma. 84

85. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani
yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha
mzuri. 85

86. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi. 86

87. Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na
Qur'ani Tukufu. 87

88.
Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha
makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la
huruma) Waumini. 88

89. Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.
89

90. Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa, 90

91. Ambao wakaifanya Qur'ani vipande vipande. 91

92. Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote. 92

93. Kwa waliyo kuwa wakiyatenda. 93

94. Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na
washirikina. 94

95. Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli. 95

96. Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo
mungu mwingine.Basi, watakuja jua! 96

97. Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako
kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo. 97

98. Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe
miongoni wanaomsujudia. 98

99. Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie
Yakini. 99
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani