Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko
la Saa (ya Kiyama) ni jambo kuu. 1

2. Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau
amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu
wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali. 2

3. Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya
Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet'ani aliye asi.

4. Ameandikiwa kwamba anaye
mfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya
Moto mkali. 4

5. Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi
kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha
kutokana na kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama
chenye umbo na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika
matumbo ya uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa
hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao
kufa, na wapo katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata
mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya,
lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila
namna ya mimea mizuri. 5

6. Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki,
na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni
Muweza wa kila kitu. 6

7. Na kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo,
na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini. 7

8. Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi
Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru. 8

9. Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache
Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha
adhabu ya kuungua. 9

10.
(Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza
mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja. 10

11. Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu
kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso
wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi. 11

12. Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho
mdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotolea mbali! 12

13. Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo
karibu zaidi kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki
muovu. 13

14. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na
wakatenda mema katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu
hutenda atakayo. 14

15. Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru
(Mtume) katika dunia na Akhera na afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame
je hila yake itaondoa hayo yaliyo mkasirisha? 16

16. Na namna hivi tumeiteremsha (Qur'ani) kuwa ni Aya
zilizo wazi, na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye.16

17. Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai
na Wakristo na Majusi na wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu
atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila
kitu. 18

18. Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu
viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima,
na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu.
Na anaye fedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu
hutenda apendayo. 18

19. Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola
wao Mlezi. Basi walio kufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya
vichwa vyao maji yanayo chemka. 19

20. Kwa maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao,
na ngozi zao pia. 20

21. Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma. 21

22. Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu
watarudishwa humo humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuungua! 22

23. Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na
wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa
mapambo ya mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri.. 23

24. Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa
kwenye Njia ya Msifiwa. 24

25. Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya
Mwenyezi Mungu na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote
sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo
kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu. 25

26. Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba
tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya
wanao izunguka kwa kut'ufu, na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na
wanao sujudu. 26

27. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu
ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali. 27

28. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la
Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni
katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri. 28

29. Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao,
na waizunguke Nyumba ya Kale. 29

30. Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya
Mwenyezi Mungu basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na
mmehalalishiwa nyama hoa ila wale mlio somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa
masanamu, na jiepusheni na usemi wa uwongo. 30

31. Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya
kumshirikisha. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka
kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali. 
32. Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu,
basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo. 
33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu.
Kisha pahala pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale. 
34. Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia
mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo
ruzukiwa katika wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu.
Jisalimishieni kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu. 
35. Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao
hutetemeka, na wanao vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa
katika tulivyo waruzuku. 
36. Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni
kudhihirisha matukuzo kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi
litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo
ubavu kuleni katika hao na walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio
kama hivi tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru. 
37. Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao,
lakini unamfikia uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze
Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema. 
38. Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika
Mwenyezi Mungu hampendi kila khaini mwingi wa kukanya mema. 
39. Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa
sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia . 
40. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki,
ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi
Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za
wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la
Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia
yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. 
41. Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi
husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na
kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote. 41

42. Na wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao
watu wa Nuhu, na kina A'ad na kina Thamud, 42

43. Na watu wa Ibrahim na watu wa Lut'i 43

44. Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa.
Nikawapa muda makafiri, kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu! 44

45. Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu,
ikawa imebaki magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti?
45

46. Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na
nyoyo zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo
pofuka, lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani. 46

47. Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu
hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi
ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi. 47

48. Na miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa
imedhulumu, na kisha nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndio marudio yote. 48

49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu
niliye dhaahiri. 49

50. Basi walio amini na wakatenda mema watapata
maghfira na riziki za ukarimu. 50

51. Na wanao jitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu
wa Motoni. 51

52. Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila
anapo soma, Shet'ani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu
huyaondoa anayo yatia Shet'ani; kisha Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. 52

53. Hayo ni ili alifanye lile analo litia Shet'ani liwe
ni fitna kwa wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni
ngumu. Na hakika madhaalimu wamo katika mfarakano wa mbali. 
54. Na ili walio pewa ilimu wajue kuwa hayo ni Haki
itokayo kwa Mola wako Mlezi na waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika
Mwenyezi Mungu ndiye anaye waongoa wenye kuamini kwenye Njia Iliyo Nyooka. 54

55. Na walio kufuru hawatoacha kuwa katika wasiwasi kwa
hilo mpaka Saa iwafikie ghafla, au iwafikie adhabu ya Siku Tasa. 55

56. Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu.
Atahukumu baina yao. Basi walio amini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani
zenye neema. 56

57. Na walio kufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi
hao watapata adhabu ya kufedhehesha. 57

58. Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha
wakauwawa au wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na
hakika Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao ruzuku. 58

59. BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapo paridhia.
Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole. 59

60. Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo
adhibiwa, kisha akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye maghfira. 60

61. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku
katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusikia Mwenye kuona. 61

62. Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na
kwamba wale wanao waomba badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu
ndiye Aliye Juu na ndiye Mkubwa. 62

63. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji
kutoka mbinguni, na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mpole na Mwenye kujua. 63

64. Ni vyake viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi.
Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Mwenye kusifiwa. 64

65. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha
kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na
amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu. 65

66. Na Yeye ndiye aliye kuhuisheni kisha akakufisheni,
na kisha atakufufueni. Hakika mwanaadamu hana fadhila. 66

67. Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika.
Basi wasizozane nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako
Mlezi. Hakika wewe uko kwenye Uwongofu Ulio Nyooka. 67

68. Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua
zaidi mnayo yatenda. 68

69. Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama
katika hayo mnayo khitalifiana. 69

70. Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo
mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi
Mungu ni mepesi. 70

71. Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo
hakuviteremshia ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhaalimu
hawatakuwa na wa kuwasaidia. 71

72. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki
katika nyuso za walio kufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya
zetu. Sema: Je! Nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi
Mungu amewaahidi walio kufuru, na ni marudio mabaya hayo. 72

73. Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika
wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa
watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake.
Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa. 73

74.
Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki
kuadhimishwa. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda. 74

75. Mwenyezi Mungu huteuwa Wajumbe miongoni mwa Malaika
na miongoni mwa watu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. 75

76. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Na
kwa Mwenyezi Mungu yatarejeshwa mambo yote. 76

77. Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni
Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe. 77

78. Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama
inavyo stahiki jihadi yake. Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo
mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu)
alikuiteni Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume
shahidi juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni
Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora
kabisa, na Msaidizi bora kabisa. 78
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani