Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili
awe mwonyaji kwa walimwengu wote. 1

2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala
hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na
akakikadiria kwa kipimo. 2

3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi
chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala
haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka. 3

4. Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni
uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na
dhulma na uwongo. 4

5. Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo
viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni. 5

6. Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika
mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. 6

7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula,
na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye? 7

8. Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na
bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye
rogwa. 8

9. Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea,
wala hawataiweza Njia. 9

10.
Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora
kuliko hayo,nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya
fakhari. 10

11. Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi
tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa.. 11

12. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia
hasira yakena mngurumo wake. 12

13. Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali
wamefungwa, wataombawafe. 13

14.
Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi! 14

15. Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo
wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo? 16

16.
Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni
ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa. 16

17. Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu,
na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe
walipotea njia? 18

18.
Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu!
Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha
wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia. 18

19. Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo
hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu
tutamwonjesha adhabu kubwa. 19

20. Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa
hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia
baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni
Mwenye kuona. 20

21. NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona
sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa
wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno! 21

22. Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku
hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali! 22

23. Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo
vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika. 23

24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi
bora na mahali penye starehe nzuri. 24

25. Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na
wateremshwe Malaika kwa wingi, 25

26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman,
Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri. 26

27. Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono
yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! 27

28. Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa
rafiki! 28

29.
Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha
nijia, na kweli Shet'ani ni khaini kwa mwanaadamu. 29

30. Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi!
Hakika watu wangu wameifanya hii Qur'ani ni kihame. 30

31. Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni
mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye
kunusuru. 31

32. Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa
Qur'ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio
tumeisoma kwa mafungu. 32

33. Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi
tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora. 33

34. Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi
mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana
njia. 34

35. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja
naye nduguye, Harun, kuwa waziri. 35

36. . Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha
Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa. 36

37. Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume,
tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye
kudhulumu adhabu chungu. 37

38. Na tuliwaangamiza kina A'di na Thamudi na watu wa
Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao. 3

39. Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza
kabisa kabisa. 39

40. Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio
teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji
kufufuliwa. 40

41. Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na
(wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume? 41

42. Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu
yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua,
watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia. 42

43. Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio
mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake? 43

44. Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au
wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.
44

45. Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza
kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa
ni kiongozi wake. 45

46. Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo. 46

47. Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na
usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka. 47

48. Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema
kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi. 48

49. Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na
tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba. 49

50. Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate
kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru. 50

51. Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji
Mwonyaji. 51

52. Basi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa
Jihadi kubwa. 52

53. Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu
mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho. 53

54. Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na
maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza. 54

55. Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo
wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake
Mlezi. 55

56. Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji.
56

57. Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na
ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi. 57

58. Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa
sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake. 58

59. . Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo
ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa
Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye. 59

60. Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema:
Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki.
60

61.
Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na
akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara. 61

62. Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana
kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru. 62

63. Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao
tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama! 63

64. Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa
kusujudu na kusimama. 64

65. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee
adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi. 65

66. Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya. 66

67. Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala
hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo. 67

68. Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na
Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa
haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara, 68

69.
Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo
kwa kufedheheka. 69

70. Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda
vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 70

71. Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo
ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu. 71

72. Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi
wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao. 72

73. Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao
Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu. 73

74. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika
wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa
wachamngu. 74

75. Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa
walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu. 75

76. Wadumu humo - kituo na makao mazuri kabisa. 76

77. Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si
kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe. 77
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani