Tarjuma ya Quran Tukufu
kwa kiswahi li

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Hakika tumekufungulia Ushindi wa dhaahiri 1

2. Ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyo
tangulia na yajayo, na akutimizie neema zake, na akuongoe katika Njia Iliyo
Nyooka, 2

3. Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu
3

4. Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za
Waumini ili wazidi Imani juu ya Imani yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye
majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima
4

5. Ili awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake
katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo, na awafutie makosa yao. Na
huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. 5

6. Na awape adhabu wanaafiki wanaume na wanaafiki
wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake, wanao mdhania Mwenyezi
Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na
awalaani, na awaandalie Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa. 6

7. Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 7

8. Hakika tumekutuma wewe uwe Shahidi, na Mbashiri, na
Mwonyaji, 8

9. Ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
mumsaidie, na mumhishimu, na mumtakase asubuhi na jioni. 9

10. Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika
wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao.
Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza
aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa. 10

11.
Watakuambia mabedui walio baki nyuma:
Yametushughulisha mali yetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha. Wanasema kwa
ndimi zao yasiyo kuwamo katika nyoyo zao. Sema: Ni nani awezaye kukusaidieni
chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka Yeye kukudhuruni au akitaka kukunufaisheni?
Bali Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. 11

12. Lakini mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarudi
kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu, na mkadhania dhana
mbaya, na mkawa watu wanao angamia. 12

13. Na asiye muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi
kwa hakika Sisi tumewaandalia makafiri Moto mkali. 13

14. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye ufalme wa mbingu na
ardhi. Humsamehe amtakaye, na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu. 14

15. Walio baki nyuma watasema: Mtapo kwenda kuchukua
ngawira, tuacheni tukufuateni! Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu.
Sema: Hamtatufuata kabisa. Mwenyezi Mungu alikwisha sema kama hivi zamani. Hapo
watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu. Siyo, bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.
15

16.
Waambie walio achwa nyuma katika mabedui: Mtakuja
itwa kwenda pigana na watu wakali kwa vita, mpigane nao au wasalimu amri. Basi
mkimt'ii, Mwenyezi Mungu atakupeni ujira mzuri. Na mkigeuka kama mlivyo geuka
kwanza, atakuadhibuni kwa adhabu iliyo chungu. 16

17. Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala
mgonjwa hana lawama. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza
katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Na atakaye geuka upande atamuadhibu
kwa adhabu chungu. 17

18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini
walipo fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi
akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu. 18

19. Na ngawira nyingi watakazo zichukua. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 19

20.
Mwenyezi Mungu anakuahidini ngawira nyingi mtakazo
zichukua, basi amekutangulizieni hizi kwanza, na akaizuia mikono ya watu
isikufikieni, na ili hayo yawe ni Ishara kwa Waumini, na akakuongozeni Njia
Iliyo Nyooka. 20

21. Na mengine hamwezi kuyapata bado, Mwenyezi Mungu
amekwisha yazingia. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. 21

22. Na lau makafiri wangeli pigana nanyi basi bila ya
shaka wangeli geuza migongo, kisha wasingeli pata mlinzi wala msaidizi.
22

23. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kwisha pita
zamani, wala hutapata mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu. 23

24. Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono
yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kukupeni Ushindi juu yao. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo. 24

25. Hao ndio walio kufuru na wakakuzuieni msiingie
Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao. Na lau si wanaume
Waumini na wanawake Waumini msio wajua mkawasaga na mkaingia makosani kutokana
nao bila ya kujua ...Mwenyezi Mungu (amefanya haya) ili amuingize amtakaye
katika rehema yake. Lau wangeli tengana bila ya shaka tungeli waadhibu walio
kufuru kwa adhabu chungu. 25

26. Pale walio kufuru walipo tia katika nyoyo zao
hasira, hasira za kijinga, Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake
na juu ya Waumini, na akawalazimisha neno la kuchamngu. Na wao walikuwa ndio
wenye haki nalo na wenye kustahili. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
26

27. Hakika Mwenyezi Mungu amemtimizia Mtume wake ndoto
ya haki. Bila ya shaka nyinyi mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani,
na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza nywele. Hamtakuwa na khofu. Yeye
anajua msiyo yajua. Basi atakupeni kabla ya haya Ushindi karibuni. 27

28. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na
Dini ya Haki, ili aitukuze juu ya dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa
Shahidi. 28

29.
Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja
naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona
wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao
zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati.
Na mfano wao katika Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia
nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima,
ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini
na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa. 29
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una
ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii [email protected]
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani