Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Lam Mim.

2. Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni
uwongofu kwa wachamungu,

3. Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa
katika tuliyo wapa.

4. Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na
yaliyo teremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.

5. Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi,
na hao ndio walio fanikiwa.

6. Hakika wale walio kufuru ni sawa kwao ukiwaonya au
usiwaonye, hawaamini.

7. Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu
ya masikio yao, na juu ya macho yao pana kifuniko. Basi watapata adhabu
kubwa.

8. Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi
Mungu na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini.

9. Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio
amini, lakini hawadanganyi ila nafsi zao; nao hawatambui.

10. Nyoyoni mwao mna maradhi, na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi. Basi
watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

11. Na wanapo ambiwa:Msifanye uharibifu ulimwenguni.
Husema: Bali sisi ni watengenezaji.

12. Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.

13. Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini watu.
Husema: Tuamini kama walivyo amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini
hawajui tu.

14. Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini.
Na wanapo kuwa peke yao na mashet'ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi.
Hakika sisi tunawadhihaki tu. 14

15. Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawawacha katika
upotofu wao wakitangatanga ovyo.

16. Hao ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu; lakini
biashara yao haikupata tija, wala hawakuwa wenye kuongoka.

17. Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto, na ulipo
tanda mwangaza wake kote kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha
katika giza, hawaoni.

18. Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.

19. Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na
radi na umeme; wakawa wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo,
kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.

20.
Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea
mwangaza huenda, na unapo wafanyia giza husimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu
angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila
kitu.

21. Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni
nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.

22. Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa
kama tandiko, na mbingu kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo
akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na
hali nyinyi mnajua.

23. Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja
wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya
Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.

24. Na mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi
uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha.

25. Na wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba
watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo,
watasema: Haya ndiyo kama tuliyo pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo
fanana; na humo watakuwa na wake walio takasika; na wao humo watadumu.

26. Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa
mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki
iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo
kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na
huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu,

27. Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha
ifunga, na wakayakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya
uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara.

28. Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu
akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?.

29. Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika
ardhi. Tena akazielekea mbingu, na akazifanya mbingu saba. Naye ndiye Mjuzi wa
kila kitu.

30. Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi
nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya
uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na
tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua.

31. Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha
akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema
kweli.

32. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi
isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.

33. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo
waambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni
na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?

34. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam,
wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika
makafiri.

35. Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika
Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu
tu; mkawa katika wale walio dhulumu.

36. Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili na
akawatoa katika waliyo kuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa
nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.

37. Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na
Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba
na Mwenye kurehemu.

38. Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni
uwongofu utokao kwangu, basi watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa khofu
juu yao wala hawatahuzunika.

39. Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu, hao
ndio watakao kuwa watu wa Motoni, humo watadumu.

40. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo
kuneemesheni, na timizeni ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na
niogopeni Mimi tu.

41. Na aminini niliyo yateremsha ambayo yanasadikisha
mliyo nayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa thamani
ndogo. Na niogopeni Mimi tu.

42. Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha kweli
nanyi mnajua.

43. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na
wanao inama.

44. Je! Mnawaamrisha watu mema na mnajisahau nafsi zenu,
na hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je, hamzingatii?

45. Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na
kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu,

46. Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao
Mlezi na ya kuwa hakika watarejea kwake.

47. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni zile neema zangu
nilizo kuneemesheni, na nikakuteuweni kuliko wote wengineo.

48. Na iogopeni Siku ambayo mtu hatomfaa mtu kwa lolote,
wala hayatakubaliwa kwake maombezi, wala hakitapokewa kikomboleo kwake; wala
hawatanusuriwa.

49. Na vile tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio
kupeni adhabu mbaya, wakiwachinja wana wenu wa kiume na wakawawacha hai
wanawake; na katika hayo ulikuwa ni mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola wenu
Mlezi.

50. Na tulipo ipasua bahari kwa ajili yenu na
tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa Firauni, na huku mnatazama.

51. Na tulipo muahidi Musa masiku arubaini, kisha
mkachukua ndama (mkamuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.

52. Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate
kushukuru.

53. Na tulipo mpa Musa Kitabu na pambanuo ili mpate
kuongoka.

54. Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu!
Hakika nyinyi mmezidhulumu nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi
tubuni kwa Muumba wenu na ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba
wenu. Naye akapokea toba yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba na Mwenye
kurehemu.

55. Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone
Mwenyezi Mungu waziwazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia.

56. Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate
kushukuru.

57. Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na
tukakuteremshieni Manna na Salwa; tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyo
kuruzukuni. Nao hawakutudhulumu Sisi lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao.

58. Na tulipo sema: Ingieni mji huu, na humo mle
mpendapo maridhawa, na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni:
Tusamehe! Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.

59. Lakini walio dhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa
waliyo ambiwa. Kwa hivyo tukaiteremsha juu ya wale walio dhulumu adhabu kutoka
mbinguni kwa sababu ya walivyo kuwa wamepotoka.

60. Na Musa alipo omba maji kwa ajili ya watu wake,
tulimwambia: Lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatimbuka chemchem kumi na
mbili; kila kabila ikajua mahali pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe
riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.

61. Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula
cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea
katika ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na
vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini,
huko mtapata mlivyo viomba. Na wakapigwa na unyonge,na umasikini, na wakastahili
ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya
Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na
wakapindukia mipaka.

62. Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo, na
Wasabai; yeyote atakaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda
mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao,
wala hawatahuzunika.

63. Na tulipo chukua ahadi yenu, na tukaunyanyua mlima
juu yenu (tukakwambieni): Shikeni kwa nguvu haya tuliyo kupeni, na yakumbukeni
yaliyomo ndani yake ili mpate kujilinda.

64. Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa si fadhila
za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema zake, mngeli kuwa miongoni mwa wenye
kukhasirika.

65. Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni mwenu
walio ivunja Sabato,(siku ya mapumziko, Jumaa Mosi) na tukawaambia: Kuweni
manyani wadhalilifu.

66. Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale walio
kuwa katika zama zao na walio kuja baada yao, na mawaidha kwa wachamngu.

67. Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi
Mungu anakuamrisheni mchinje ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema:
Audhubil lahi! Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.

68. Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie
ni ng'ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng'ombe huyo si mpevu, wala
si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.

69. Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini
rangi yake? Akasema: Yeye anasema, kuwa ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi
yake imekoza, huwapendeza wanao mtazama.

70. Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie
ni yupi? Hakika tunaona ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi
Mungu akipenda, tutaongoka.

71. Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni ng'ombe asiye
tiwa kazini kulima ardhi wala kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema:
Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.

72. Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na
Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha.

73. Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng'ombe).
Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili
mpate kufahamu.

74. Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, hata
zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani kuna mawe yanayo timbuka mito, na kuna
mengine yanayo pasuka yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa
sababu ya khofu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na
mnayo yafanya.

75. Mnatumai watakuaminini na hali baadhi yao walikuwa
wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha wakayabadili baada ya kuwa
wameyafahamu, na hali wanajua?

76. Na wanapo kutana na wale walio amini husema:
Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao, wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyo
kufunulieni Mwenyezi Mungu ili wapate kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi? Basi
hamfahamu nyinyi?

77. Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayo
yaficha na wanayo yatangaza?

78. Na wako miongoni mwao wasio jua kusoma; hawakijui
Kitabu isipo kuwa uwongo wanao utamani, nao hawana ila ni kudhania tu. 78

79. Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao,
kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo.
Basi ole wao kwa yale iliyo andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo
yachuma.

80. Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache
tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda
kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua?

81. Naam, anaye chuma ubaya - na makosa yake
yakamzunguka hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.

82. Na wale walio amini na wakatenda mema, hao ndio watu
wa Peponi, humo watadumu.

83. Na tulipo funga agano na Wana wa Israili:
Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na
mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni
Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.

84. Na tulipo chukua agano lenu kuwa hamtamwaga damu
zenu, wala hamtatoana majumbani mwenu; nanyi mkakubali nanyi
mnashuhudia.

85. Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi
yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka
mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na
mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila
hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu
kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda.

86. Hao ndio walio nunua uhai wa dunia kwa (uhai wa)
Akhera; kwa hivyo hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.

87. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada
yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na
tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale
ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine
mkawauwa.

88. Na walisema: Nyoyo zetu zimefunikwa. Bali Mwenyezi
Mungu amewalaani kwa kufuru zao: kwa hivyo ni kidogo tu wanayo yaamini.

89. Na kilipo wajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu
kinacho thibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi kuwashinda
makafiri - yalipo wajia yale waliyo kuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya
Mwenyezi Mungu juu ya wakanushao!

90. Kiovu kweli walicho jiuzia nafsi zao, nacho ni kule
kukataa kwao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kuona maya kwa kuwa
Mwenyezi Mungu humteremshia fadhila yake amtakaye miongoni mwa waja wake. Basi
wamejiletea wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu. Na makafiri watapata mateso ya
kudhalilisha.

91. Na wanapo ambiwa: Yaaminini aliyo yateremsha
Mwenyezi Mungu. Wao husema: Tunaamini tuliyo teremshiwa sisi. Na huyakataa
yasiyo kuwa hayo. Na hali ya kuwa hii ndiyo Haki inayo thibitisha yale waliyo
nayo wao. Sema: Mbona mliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani ikiwa kweli
mlikuwa Waumini?

92. Na alikufikieni Musa na hoja zilizo waziwazi, kisha
mkamchukua ndama (kumuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.

93. Na tulipo chukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu
yenu (tukakwambieni): Kamateni kwa nguvu haya tuliyo kupeni na sikieni.
Wakasema: Tumesikia na tumekataa! Na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya) ndama
kwa kufuru yao. Sema: Ni uovu mno iliyo kuamrisheni imani yenu ikiwa ni wenye
kuamini.

94. Sema: Ikiwa nyumba ya Akhera iliyoko kwa Mwenyezi
Mungu ni yenu tu bila ya watu wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi mnasema
kweli.

95. Wala hawatayatamani kamwe kwa sababu ya yale yaliyo
tangulizwa na mikono yao; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema wanao
dhulumu.

96. Na hakika utawaona ni wenye kuwashinda watu wote kwa
pupa ya kuishi, na kuliko washirikina. Kila mmoja wao anatamani lau angeli pewa
umri wa miaka elfu. Wala hayo ya kuzidishiwa umri hayamuondoshei adhabu; na
Mwenyezi Mungu anayaona wanayo yatenda.

97. Sema: Aliye kuwa ni adui wa Jibril, basi huyo ndiye
aliye iteremsha Qur'ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu inayo
thibitisha yaliyo kuwa kabla yake, na ni uwongofu na bishara njema kwa Waumini.

98. Aliye kuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na
Mitume wake na Jibril na Mikail, basi hakika Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.

99. Hakika tumekuteremshia Ishara zilizo wazi na hapana
wanao zikataa ila wapotovu.

100. Je! Ati ndio kila wanapo funga ahadi huwapo kikundi
miongoni mwao kikaivunja? Bali wengi wao hawaamini.

101. Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale walio pewa
Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba
hawajui.

102. Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia
ufalme wa Su leiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio
kufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili,
Haaruta na Maaruta katika Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka
wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili
yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka
Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yatayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika
wanajua kwamba aliye khiari haya hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na
hakika ni kiovu mno walicho jiuzia nafsi zao laiti wangelijua.

103. Na lau kuwa wangeamini na wakaogopa, bila ya shaka
malipo yatokayo kwa Mwenyezi Mungu yange kuwa bora. Laiti wangeli kuwa wanajua!

104. Enyi mlio amini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni:
"Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.

105. Walio kufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na
washirikina hawapendi mteremshiwe kheri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na
Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi Mungu ni
mwenye fadhila kubwa.

106. Ishara yoyote tunayo ifuta au tunayo isahaulisha
tunailetea iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi
Mungu ni Muweza wa kila kitu?

107. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na
ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.

108. Au mnataka kumwomba Mtume wenu kama alivyo ombwa
Musa zamani? Na anaye badilisha Imani kwa ukafiri bila ya shaka huyo ameipotea
njia iliyo sawa.

109. Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau
wange kurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya
uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia Haki. Basi
sameheni na wachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atapo leta amri yake. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

110. Na shikeni Sala na toeni Zaka; na kheri mtakazo
jitangulizia nafsi zenu mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu
anayaona mnayo yafanya.

111. Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Yahudi
au Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni
wasema kweli.

112. Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa
Mwenyezi Mungu naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi,
wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

113. Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo. Na
Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo. Na ilhali wote wanasoma Kitabu hicho
hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasio jua kitu mfano wa kauli yao
hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo
kuwa wakikhitilafiana.

114. Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye zuia
misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake na akajitahidi
kuiharibu? Watu hao haitawafalia kuingia humo ila nao wanaogopa. Duniani
watapata hizaya na Akhera watapata adhabu kubwa.

115. Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu.
Basi kokote mnako elekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni
mwenye wasaa na Mjuzi.

116. Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana.
Subhanahu! Ametakasika na hayo. Bali vyote viliomo mbinguni na duniani ni vyake.
Vyote vinamt'ii Yeye.

117. Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza;
na anapo taka jambo basi huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.

118. Na walisema wale wasio jua kitu: Mbona Mwenyezi
Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale walio kuwa
kabla yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka
wazi Ishara kwa watu wenye yakini.

119. Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri, na
mwonyaji. Na wala hutaulizwa juu ya watu wa Motoni.

120. Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka
ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama
ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala
msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.

121. Wale tulio wapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo
kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini. Na wanao kikataa basi hao ndio wenye
kukhasiri.

122. Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo
kuneemesheni, na hakika Mimi nikakufadhilisheni kuliko wengineo wote. 122

123. Na iogopeni siku ambayo hatamfaa mtu mwenziwe kwa
lolote, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo, wala maombezi hayatamfaa, wala
hawatanusuriwa.

124. Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa kumpa
amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi
wa watu. Akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu
haitawafikia wenye kudhulumu.

125. Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba)
iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipo kuwa akisimama
Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni
Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu na wanao jitenga huko kwa
ibada, na wanao inama na kusujudu.

126. Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye
huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini
Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia
nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo ni
pahala pabaya mno pa kurejea.

127. Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua
misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe
ndiye Msikizi Mjuzi.

128. Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye
kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na
utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.

129. Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye tokana na
wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika
Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. 129

130. Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipo kuwa
anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini Sisi tulimteuwa yeye katika
dunia; na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.

131. Na Mola wake Mlezi alipo mwambia: Silimu,
Nyenyekea! Alinena: Nimesilimu, nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu wote.

132. Na Ibrahim akawausia wanawe, na pia Yaaqub: Enyi
wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteulieni Dini hii; basi msife ila nanyi
mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.

133. Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti,
akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako
na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is- hak, Mungu Mmoja tu, na sisi
tunasilimu kwake.

134. Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata waliyo
yachuma, nanyi mtapata mtakayo yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyo kuwa
wakiyafanya wao.

135. Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio
mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika
washirikina.

136. Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale
tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na
Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii
wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na
sisi tumesilimu kwake.

137. Basi wakiamini kama mnavyo amini nyinyi, itakuwa
kweli wameongoka. Na wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi
Mungu atakutosheni kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye Msikizi, Mjuzi.

138. Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu, na nani
aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu
Yeye tu.

139. Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye
ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna
vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.

140. Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na
Yaakub na wajukuu zao walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua
zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliye
ficha ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye
kughafilika na hayo myafanyayo.

141. Hao ni watu walio kwisha pita. Wao watapata waliyo
yachuma, na nyinyi mt apata mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyo
kuwa wakifanya wao.

142. WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho
wageuza kutoka kibla chao walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na
Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo
nyooka.

143. Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani,
ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na
hatukukifanya kibla ulicho kuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume
na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo
kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye
kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye
kuwarehemu.

144. Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako
mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako
upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande
huo; na hakika wale walio pewa Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa
Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.

145. Na hao walio pewa Kitabu, hata ukiwaletea hoja za
kila namna, hawatafuata Kibla chako; wala wewe hutafuata kibla chao, wala baadhi
yao hawatafuata kibla cha wengineo; na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya
kukufikia ujuzi, hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhullumu.

146. Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo
wajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.

147. Haki inatoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe
miongoni mwa wanao fanya shaka.

148. Na kila mmoja anao upande anao elekea. Basi
shindanieni mema. Popote mlipo Mwenyezi Mungu atakuleteni nyote pamoja. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

149. Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti
Mtakatifu. Na hiyo ndiyo Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si
mwenye kughafilika na mnayo yatenda.

150. Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti
Mtakatifu. Na popote mlipo elekezeni nyuso zenu upande huo ili watu wasiwe na
hoja juu yenu, isipokuwa wale walio dhulumu miongoni mwao Basi msiwaogope wao,
lakini niogopeni Mimi - na ili nikutimizieni neema yangu, na ili mpate kuongoka.

151. Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na
nyinyi, anakusomeeni Aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima
na kukufundisheni mliyo kuwa hamyajui.

152. Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni
wala msinikufuru.

153. Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala.
Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.

154. Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika Njia ya
Mwenyezi Mungu ni maiti; bali hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui.

155. Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na
njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri,

156. Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni
wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.

157. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao
Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.

158. Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za
Mwenyezi Mungu. Basi anaye hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa
kwake kuvizunguka. Na anaye jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi
Mungu ni Mwenye shukrani na Mjuzi.

159. Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha nazo ni
hoja zilizo wazi na uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni -- hao
anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.

160. Ila wale walio tubu na wakatengeneza na
wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na
Mwenye kurehemu.

161. Hakika walio kufuru na wakafa hali ni makafiri, hao
iko juu yao laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.

162. Watadumu humo. Hawata-punguziwa adhabu wala
hawatapewa muda wa kupumzika.

163. Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila
Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

164. Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na
kukhitalifiana usiku na mchana, na marikebu ambazo hupita baharini kwa
viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa
hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya
wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina
ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao zingatia.

165. Na katika watu wapo wanao chukua waungu wasio kuwa
Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walio amini
wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana. Na laiti walio dhulumu wakajua watakapo
iona adhabu kuwa nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali
wa kuadhibu!

166. Walio fuatwa watakapo wakataa wale walio wafuata,
na hali ya kuwa wamekwisha iona adhabu; na yatakatika mafungamano yao.

167. Na watasema wale walio fuata: Laiti tungeweza
kurudi tukawakataa wao kama wanavyo tukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu
atakavyo waonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka
Motoni.

168. Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na
vizuri, wala msifuate nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu aliye
dhaahiri.

169. Yeye anakuamrisheni maovu na machafu, na
mumsingizie Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua.

170. Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa
baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?

171. Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa anaye
mpigia kelele asiye sikia ila wito na sauti tu ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa
hivyo hawaelewi.

172. Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni,
na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.

173. Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya
nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi
Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye
hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

174. Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Mwenyezi
Mungu katika Kitabu, wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao
isipo kuwa moto, wala Mwenyezi Mungu hatawasemeza Siku ya Kiyama, wala
hatawatakasa. Nao watapata adhabu chungu.

175. Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu, na
adhabu badala ya maghfira. Ama wavumilivu wa Moto watu hawa!

176. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha
Kitabu kwa haki. Na wale walio khitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani
ulio mbali na haki.

177. Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa
mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake,
jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na
akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na
wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha,
na hao ndio wajilindao.

178. Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi
katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke
kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa
wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu
Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata
adhabu chungu.

179. Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi
wenye akili, ili msalimike.

180. Mmeandikiwa -- mmoja wenu anapo fikwa na mauti,
kama akiacha mali -- afanye wasia kwa wazazi wake na jamaa zake kwa namna nzuri
inayo pendeza. Ni waajibu haya kwa wachamngu.

181. Na atakaye ubadilisha wasia baada ya kuusikia, basi
dhambi yake ni juu ya wale watakao ubadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia Mwenye kujua.

182. Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo au kupata
dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Msamehevu na Mwenye kurehemu.

183. Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo
andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.

184. (Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye
kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku
nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye
fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama
mnajua.

185. Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani
kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi
ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini,
basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo
mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze
Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.

186. Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu,
waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na
waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.

187. Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake
zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba
mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na
amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi
Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi
wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali
mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie.
Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.

188. Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na kuzipeleka
kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.

189. Wanakuuliza khabarai ya miezi. Sema: Hiyo ni vipimo
vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kuziingia nyumba kwa nyuma.
Bali mwema ni mwenye kuchamngu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni. Na
mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.

190. Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale
wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao
uadui.

191. Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote
walipo kutoeni; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane nao
kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi nanyi pia
wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.

192. Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe Mwenye kurehemu.

193. Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe
ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa wenye
kudhulumu.

194. Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu
vitakatifu vimeekewa kisasi. Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri
alivyo kushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu
yu pamoja na wachamngu.

195. Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala
msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi
Mungu huwapenda wafanyao wema.

196. Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu. Na ikiwa mkizuiwa,basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala
msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa
mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa
kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye
kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye
mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba
mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake
hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi
Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

197. Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya
Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo
vichafu wala asibishane katika Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu
anaijua. Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na
nicheni Mimi, enyi wenye akili!

198. Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola wenu
Mlezi. Na mtakapo miminika kutoka A'rafat mtajeni Mwenyezi Mungu penye Masha'ril
Haram. Na mkumbukeni kama alivyo kuongoeni, ijapo kuwa zamani mlikuwa miongoni
mwa walio potea.

199. Kisha miminikeni kutoka pale wanapo miminika watu,
na muombeni Mwenyezi Mungu msamaha: hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.

200. Na mkisha timiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi
Mungu kama mlivyo kuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya
watu wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika Akhera hana sehemu
yoyote.

201. Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu Mlezi,
tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!

202. Hao ndio watakao pata sehemu yao kwa sababu ya yale
waliyo yachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

203. Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo
hisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea) si dhambi
juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumchamngu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.

204. Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa
maisha ya kidunia hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo
moyoni mwake, na hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu.

205. Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa
kufisidi humo na kuteketeza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.

206. Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na
mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa
mapumziko.

207. Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa
kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.

208. Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa
ukamilifu, wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye
wazi.

209. Na ikiwa mkateleza baada ya kukufikieni hoja zilizo
wazi, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

210. Je wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika
vivuli vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa? Na kwa
Mwenyezi Mungu ndio hurejeshwa mashauri yote.

211. Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara ngapi
zilizo wazi? Na anaye zibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia basi
hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

212. Walio kufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na
wanawafanyia maskhara walio amini. Na wenye kuchamngu watakuwa juu yao Siku ya
Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

213. Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu
akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa
Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala
hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja
zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini
yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na
Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.

214. Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni
kama yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na
wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya
Mwenyezi Mungu itakuja? Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.

215. Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayo itoa ni
kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri
yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua.

216. Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha kwenu.
Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho
ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.

217. Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi
mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu
wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu
wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi
mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha
kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika
nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao
zimeharibika duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.

218. Hakika wale walio amini na wale walio hama na
wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanao taraji rehema za Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.

219. Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika
hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi
kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna
hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri--

220. .--katika mambo ya dunia na mambo ya Akhera. Na
wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika
nao basi ni ndugu zenu; na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na
Mwenyezi Mungu angeli penda angeli kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

221. Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na
mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze
(binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni
bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na
Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye
huzibainisha Aya zake kwa watu ili wapate kukumbuka.

222. Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni
uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka
wat'ahirike. Wakisha t'ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha.

223. Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde
zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi
Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema
Waumini.

224. Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo
vyenu kuwa ni kisingizio cha kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha
baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

225. Mwenyezi Mungu hakushikeni kwa viapo vyenu vya
upuuzi. Bali anakushikeni kwa yanayo chuma nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe na Mpole.

226. Kwa wanao apa kuwa watajitenga na wake zao,
wangojee miezi mine. Wakirejea basi Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye kusamehe na
Mwenye kurehemu.

227. Na wakiazimia kuwapa talaka basi, Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusikia na Mjuzi.

228. Na wanawake walio achwa wangoje peke yao mpaka
t'ahara (au hedhi) tatu zipite. Wala haiwajuzii kuficha alicho umba Mwenyezi
Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na
waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya sulhu.
Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana
daraja zaidi kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

229. T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au
kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake
zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka
ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya
Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo
mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya Mwenyezi
Mungu, hao ndio madhaalimu.

230. Na kama amempa t'alaka (ya tatu) basi si halali
kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya
kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni
mipaka ya Mwenyezi Mungu anayo ibainisha kwa watu wanao jua.

231. Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia
kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala
msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu
nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni
neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima
anacho kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

232. Na mtakapo wapa wanawake t'alaka nao wakamaliza eda
yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema.
Hayo anaonywa nayo yule miongoni mwenu anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua,
lakini nyinyi hamjui.

233. Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka
miwili kaamili kwa anaye taka kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula
cha kina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa
kadiri ya uwezo wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa
ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka
kumwachisha ziwa kwa kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka
kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa
mlicho ahidi kwa mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba
Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayo yatenda.

234. Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake,
hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi. Na wanapo timiza eda yao
basi hapana ubaya kwao kwa wanao jifanyia kwa mujibu wa ada. Na Mwenyezi Mungu
anazo khabari za yote mnayo yatenda.

235. Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa
ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi
Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene
maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni
kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye.
Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.

236. Hapana ubaya kwenu mkiwapa t'alaka wanawake ambao
hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye
wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza kwa mujibu wa
dasturi kuwa ni haki juu ya watendao mema.

237. Na mkiwapa t'alaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha
wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio agana, isipo kuwa
ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi
mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala
msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.

238. Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na
simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).

239. Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu
au mmepanda. Na mtakapo kuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama
alivyo kufunzeni yale mliyo kuwa hamyajui.

240. Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakawacha
wake, na wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi kwa mwaka mmoja bila ya
kuwatoa nyumba. Na wanawake wenyewe wakiondoka, basi hapana ubaya kwenu kwa
waliyo jifanyia wenyewe kwa mujibu wa Sharia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu
na Mwenye hikima.

241. Na wanawake walio achwa wapewe cha kuwaliwaza kwa
mujibu wa Sharia. Haya ni waajibu kwa wachamngu.

242. Namna hivi anakubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake
ili mpate kufahamu.

243. Hukuwaona wale walio toka majumbani kwao kwa maelfu
kwa kuogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha akwahauisha. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.

244. Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni
kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi na Mjuzi.

245. Ni nani atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema
ili amzidishie mzidisho mwingi, na Mwenyezi Mungu hukunja na hukunjua. Na Kwake
Yeye mtarejea.

246. Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya
Musa, walipo mwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya
Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane?
Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa
majumbani kwetu na watoto wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo
kuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.

247. Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu
amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme
juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa
wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia
ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.

248. Na Nabii wao akawaambia: Alama ya ufalme wake ni
kukuleteeni lile sanduku ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho
kwa Mola wenu Mlezi, na mna mabaki ya waliyo yaacha kina Musa na kina Harun,
wanalichukua Malaika. Bila shaka katika hayo zimo dalili kwenu ikiwa nyinyi
mnaamini.

249.Basi Taluti alipo ondoka na majeshi alisema:
Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na
asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono
wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka
mto yeye na wale walio amini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti
(Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi
Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.

250. Na walipo toka kupambana na Jaluti na majeshi yake
walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na
utusaidie tuwashinde watu Makafiri--

251. .--Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na
Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na
akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa
watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya
walimwengu wote.

252. Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki.
Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.

253. MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo.
Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo.
Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho
Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada
yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati
yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu
alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.

254. Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni kabla
haijafika Siku ambayo hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi. Na
makafiri ndio madhaalimu.

255. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai,
Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee
vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila
ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui
chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake
imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye
aliye juu, na ndiye Mkuu.

256. Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu
umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini
Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

257. Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa
gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni Mashet'ani.
Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo
watadumu.

258. Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola
wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola
wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na
kufisha. Ibrahim akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe
lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu madhaalimu.

259. Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha
kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake?
Basi Mwenyezi Mungu alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua.
Akamuuliza: Je umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya
siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na
vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni
Ishara kwa watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha
nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye
uweza juu ya kila kitu.

260. Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe
vipi unavyo fufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha!
Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako,
kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue
kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.

261. Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya
Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika
kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.

262. Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu,
kisha hawafuatishii masimbulizi wala udhia kwa walicho toa, wana ujira wao kwa
Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

263. Kauli njema na usamehevu ni bora kuliko sadaka
inayo fuatiliwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha na Mpole.

264. Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa
masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala
hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa
jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha
tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu makafiri.

265. Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta
radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo
mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama
haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo
yatenda.

266. Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha
mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila
namna, na uzee ukamfikia naye hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga
chenye moto, kikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara
ili mpate kufikiri.

267. Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo
vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa
vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho.
Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.

268. Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na
anakuamrisheni mambo machafu. Na Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila
zitokazo kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.

269. Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima
bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.

270. Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo weka basi
hakika Mwenyezi Mungu anajua. Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.

271. Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha
mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi
ya maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.

272. Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu
humwongoa amtakaye. Na kheri yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu. Wala msitoe ila
kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mtakayo toa mtalipwa kwa
ukamilifu, wala hamtadhulumiwa.

273. Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia za
Mwenyezi Mungu, wasio weza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye wajua
hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua
kwa alama zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa,
basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.

274. Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri
na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao,
wala hawatahuzunika.

275. Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama
aliye zugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama
riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi
aliye fikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake
ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia
basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.

276. Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na
huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae
dhambi.

277. Hakika wale walio amini na wakatenda mema na
wakashika Sala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala
haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.

278. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni
riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini.

279. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu
na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala
msidhulumiwe.

280. Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje
mpaka afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa
mnajua.

281. Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi
Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.


282. Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio
wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala
mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na
mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi.
Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa
au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa
uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana
wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia
kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na
mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa
mpaka muda wake. Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa
zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya
mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini
mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na
mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

283. Na mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, yatosha
kukabidhiwa rahani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe basi aliye aminiwa
airudishe amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala
msifiche ushahidi. Na atakaye ficha basi hakika moyo wake ni wenye kutenda
dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayo yatenda.

284. Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya Mwenyezi
Mungu. Na mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu
atakuhisabuni kwayo. Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

285. Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa
Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na
Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote
katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet'ii. Tunakutaka
maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.

286. Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa
kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma
ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea.
Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla
yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na
uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya
makafiri.
Imetarjumiwa na
Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa
anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August
1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani