Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya
Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina
yenu, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini. 1

2. Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi
Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na
wakamtegemea Mola wao Mlezi. 2

3. Hao ambao wanashika Sala na wanatoa katika yale
tunayo waruzuku. 3

4. Hao kweli ndio Waumini. Wao wana vyeo, na maghfira,
na riziki bora, kwa Mola wao Mlezi. 4

5. Kama Mola wako Mlezi alivyo kutoa nyumbani kwako kwa
Haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia. 5

6.
Wanajadiliana nawe kwa jambo la Haki baada ya kwisha
bainika, kama kwamba wanasukumwa kwenye mauti nao wanaona. 6

7. Na Mwenyezi Mungu alipo kuahidini kuwa moja katika
makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na
Mwenyezi Mungu anapenda ahakikishe Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya
makafiri. 7

8. Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangachukia
wakosefu. 8

9. Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye
akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wanao fuatana
mfululizo. 9

10. Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara
na ili nyoyo zenu zituwe. Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima. 10

11. Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho
kutoka kwake, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo
na kukuondoleeni uchafu wa Shet'ani, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara
miguu yenu. 11

12. Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi
ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za
walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za
vidole. 12

13. Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume
wake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi Mwenyezi Mungu ni
Mkali wa kuadhibu. 13

14. Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri
wana adhabu ya Moto. 14

15. Enyi Mlio amini! Mkikutana na walio kufuru vitani
msiwageuzie mgongo. 15

16. Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo
kuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu
ya Mwenyezi Mungu. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu. 16

17.
Hamkuwauwa nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye
wauwa. Na wewe hukutupa, walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye tupa, ili awajaribu
Waumini majaribio mema yatokayo kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Msikizi na
Mjuzi. 17

18. Ndio hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kudhoofisha vitimbi vya makafiri. 18

19. Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha kujieni.
Na mkiacha itakuwa ndio kheri kwenu. Na mkirejea Sisi pia tutarejea. Na jeshi
lenu halitakufaeni kitu, japo likiwa kubwa. Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na
Waumini. 19

20. Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, wala msijiepushe naye, nanyi mnasikia. 20

21. Wala msiwe kama wale wanao sema: Tumesikia, na kumbe
hawasikii. 21

22. Hakika vinyama viovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni vile
viziwi na bubu visio tumia akili zao. 22

23. Na Mwenyezi Mungu angeli jua wema wowote kwao ange
wasikilizisha, na lau ange wasikilizisha wangeli geuka wakapuuza. 23

24. Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume
anapo kuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu
huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa. 24

25. Na jikingeni na Fitna ambayo haitowasibu walio
dhulumu peke yao kati yenu. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu. 25

26. Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, mkionekana
wanyonge katika nchi, mnaogopa watu wasikunyakueni, naye akakupeni pahala pazuri
pa kukaa, na akakutieni nguvu kwa nusura yake, na akakupeni riziki nzuri ili
mpate kushukuru. 26

27. Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi Mungu na
Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua. 27

28. Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu ni Fitna
(mtihani), na kwamba kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa. 28

29. Enyi mlio amini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atakupeni
kipambanuo, na atakufutieni makosa, na atakusameheni, na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye fadhila kubwa. 29

30. Na walipo kupangia mpango walio kufuru wakufunge, au
wakuuwe, au wakutoe. Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na
Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango. 30

31. Na wanapo somewa Aya zetu, wao husema: Tumesikia. Na
lau tungeli penda tunge sema kama haya. Haya si chochote ila hadithi za watu wa
kale tu. 31

32. Na walipo sema: Ee Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni
kweli itokayo kwako basi tunyeshee mawe kutoka mbinguni, au tuletee adhabu
yoyote iliyo chungu. 32

33. Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu nawe umo
pamoja nao, wala Mwenyezi Mungu si wa kuwaadhibu na hali ya kuwa wanaomba
msamaha. 33

34. Lakini wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu
asiwaadhibu, na hali ya kuwa wanawazuilia watu Msikiti Mtakatifu? Wala wao
hawakuwa ndio walinzi wake, bali walinzi wake hawakuwa ila wacha-Mngu tu. Lakini
wengi katika wao hawajui. 34

35. Na haikuwa ibada yao kwenye hiyo Nyumba (Al Kaaba)
ila ni kupiga miunzi na makofi. Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa
mkikufuru. 35

36. Hakika wale walio kufuru hutoa mali yao ili kuzuilia
Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watayatoa, kisha yatakuwa juu yao majuto, na kisha
watashindwa. Na wale walio kufuru watakusanywa kwenye Jahannam. 36

37. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwa pambanua walio waovu
na walio wema, na kuwaweka waovu juu ya waovu wengine, na kuwarundika wote
pamoja, na kuwatupa katika Jahannam. Hao ndio walio khasirika. 37

38. Waambie wale walio kufuru: Wakikoma watasamehewa
yaliyo kwisha pita. Na wakiyarudia basi imekwisha pita mifano ya wa zamani. 38

39. Na piganeni nao mpaka isiwepo fitna na mateso, na
Dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyezi
Mungu anayaona wanayo yatenda. 39

40. Na kama wakigeuka basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu
ndiye Mola wenu, ni Mola Mwema na Msaidizi Mwema. 40

41. NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi khums
(sehemu moja katika tano) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na
mayatima, na masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu na
tuliyo yateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuo, siku yalipo kutana majeshi
mawili. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. 41

42. Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya
karibu ya bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini
yenu. Na ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini
(mkakutana) ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa
sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa
kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia
Mwenye kujua. 42

43. Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao
ni wachache - na lau angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na
mngeli zozana katika jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu kakuvueni. Hakika Yeye ni
Mwenye kuyajua yalio vifuani. 43

44. Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa
wao ni wachache, na akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi
Mungu atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu.
44

45. Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni
imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa. 45

46. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala
msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi
Mungu yu pamoja na wanao subiri. 46

47. Wala msiwe kama wale walio toka majumbani mwao kwa
fakhari na kujionyesha kwa watu, na wakawazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ameyazunguka yote wanayo yafanya. 47

48. Na pale Shet'ani alipo wapambia vitendo vyao, na
akawaambia: Hapana watu wa kukushindeni hii leo, na hali mimi ni mlinzi wenu.
Yalipo onana majeshi mawili, akarudi nyuma, na akasema: Mimi si pamoja nanyi.
Mimi naona msiyo yaona. Mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni
mkali wa kuadhibu. 48

49. Na walipo sema wanaafiki, na wale wenye ugonjwa
nyoyoni mwao: Watu hawa dini yao imewadanganya. Na Mwenye kumtegemea Mwenyezi
Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Ametukuka, na Mwenye hikima. 49

50. Na laiti ungeli ona Malaika wanapo wafisha wale
walio kufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, na kuwaambia: Ionjeni adhabu
ya Moto! 50

51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyo kwisha tangulizwa
na mikono yenu, na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja. 51

52. Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa kabla yao
- walizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa
sababu ya madhambi yao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mkali wa
kuadhibu. 52

53. Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa
neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao.
Na hakika Mwwnyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. 53

54. Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao -
walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao. Na
tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu. 54

55. Hakika vinyama vilio viovu kabisa mbele ya Mwenyezi
Mungu ni wale wanao kufuru, basi hao hawaamini; 55

56. Wale ambao miongoni mwao umepatana nao ahadi, kisha
wanavunja ahadi yao kila mara, wala hawamchi Mungu. 56

57. Basi ukiwakuta vitani wakimbize walio nyuma yao ili
wapate kukumbuka. 57

58. Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie
ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini. 58

59. Wala wasidhanie wale walio kufuru kwamba wao
wametangulia mbele. La, wao hawatashinda. 59

60. Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi
walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui
zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa
chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi
hamtadhulumiwa. 60

61. Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee
Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. 61

62. Na wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu
atakutosheleza. Kwani Yeye ndiye aliye kuunga mkono kwa nusura yake na kwa
Waumini. 62

63. Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote
viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye
aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 63

64. Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na
Waumini walio kufuata. 64

65. Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani. Wakiwapo
kati yenu ishirini wanao subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo kati yenu
mia watawashinda elfu moja katika walio kufuru. Kwa sababu wao ni watu wasio
fahamu. 65

66. Sasa Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua kuwa
upo udhaifu kwenu. Kwa hivyo wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye kusubiri
watawashinda mia mbili. Na wakiwapo elfu moja watawashinda elfu mbili, kwa
idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri. 66

67. Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe
ameshinda baraabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu
anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima. 67

68. Lau isingeli kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia
kutoka kwa Mwenyezi Mungu ingeli kupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyo chukua. 68

69. Basi kuleni katika mlivyo teka, ni halali na vizuri,
na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye
kurehemu. 69

70. Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu:
Kama Mwenyezi akiona kheri yoyote nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko vilivyo
chukuliwa kwenu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu. 70

71. Ikiwa wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha
mfanyia khiana Mwenyezi Mungu kabla yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima. 71

72. Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania
Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa
kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio
amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka
wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia,
isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu
anayaona mnayo yatenda. 72

73. Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa
wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa. 73

74. Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi katika
Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio
Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema. 74

75. Na watakao amini baadaye na wakahajiri, na
wakapigana Jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa nasaba
wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. 75
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani