Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA
REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1.
IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika
mghafala wanapuuza. 1

2.
Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao
Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo. 2

3.
Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu
hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama
nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona? 3

4. Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo
mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. 4

5. Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo,
bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama
walivyo tumwa wale wa mwanzo. 5

6.
Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza.
Basi, je, wataamini hawa? 6

7. Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio
wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui. 7

8. Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala
hawakuwa wenye kuishi milele. 8

9. Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na
tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka. 9

10. Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani
yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii? 10

11. Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu
tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine. 11

12. Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza
kukimbia. 12

13.
Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe
zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa! 13

14.
Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa
madhaalimu. 14

15.
Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya
kama walio fyekwa, wamezimika. 15

16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina
yao kwa mchezo. 16

17. Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia
Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo. 17

18. Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na
mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua. 18

19. Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo
mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu,
wala hawachoki. 19

20.
Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei. 20

21. Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua? 21

22. Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa
Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika.
Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na
hayo wanayo yazua. 22

23. Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao
hojiwa kwa wayatendayo. 23

24. Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema:
Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa
walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza. 24

25. Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila
tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu. 25

26. Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana!
Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio
tukuzwa. 26

27.
Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake. 27

28.
Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala
hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa
wananyenyekea. 28

29. Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu,
badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo
wenye kudhulumu. 29

30. Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na
ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji
kila kilicho hai? Basi je, hawaamini? 30

31. Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili
isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka. 31

32. Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa,
lakini wanazipuuza Ishara zake. 32

33. Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na
mwezi, vyote katika anga vinaogelea. 33

34. Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako
kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele? 34

35. Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa
mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa. 35

36. Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni
kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na
hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema! 36

37.
Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni
Ishara zangu. Basi msinihimize. 37

38. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi
mnasema kweli? 38

39. Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao
hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa! 39

40. Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala
hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula! 40

41. Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa.
Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia
dhihaka. 41

42. Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na
Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi. 42

43. Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao
hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi! 43

44. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri
ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha
zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda? 44

45. Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi
hawasikii wito wanapo onywa. 45

46. Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu
itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa
wenye kudhulumu. 46

47. Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya
Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe
ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu. 47

48. Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi,
na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu, 48

49. Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na
wanaiogopa Saa ya Kiyama. 49

50. Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo
yateremsha. Basi je! Mnayakataa? 50

51. Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake
zamani, na tulikuwa tunamjua. 51

52. Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya
masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu? 52

53.
Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu. 53

54.
kasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa
katika upotofu ulio dhaahiri. 54

55.
Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe
ni katika wachezao tu? 55

56.
Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa
mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia
hayo. 56

57. Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya
baada ya mkisha geuka kwenda zenu. 57

58. Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili
wao walirudie. 58

59.
Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu?
Hakika huyu ni katika walio dhulumu. 59

60.
Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja.
Anaitwa Ibrahim. 60

61.
Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe
Ibrahim? 61

62.
Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe
Ibrahim? 62

63.
Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi
waulizeni ikiwa wanaweza kutamka. 63

64. Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi
mlikuwa madhaalimu! 64

65. Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao
wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi. 65

66.
Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi
Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni? 66

67. Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya
Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini? 67

68.
Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu,
ikiwa nyinyi ni watendao jambo! 68

69. Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa
Ibrahim! 69

70. Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao
ndio walio khasiri. 70

71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye
nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote. 71

72. Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na
wote tukawajaalia wawe watu wema. 72

73. Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri
yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na
walikuwa wanatuabudu Sisi tu. 73

74. Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na
ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu. 74

75. Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni
miongoni mwa watenda mema. 75

76. Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na
tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa. 76

77. Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu.
Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote. 77

78. Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika
kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye
kushuhudia hukumu yao hiyo. 78

79.
Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa
hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee
na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo. 79

80. Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili
yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru? 80

81. Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga
wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila
kitu. 81

82. Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya
kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao. 82

83. Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema:
Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu. 83

84. Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo
kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo
toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada. 84

85. Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa
miongoni mwa wanao subiri. 85

86. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao
walikuwa katika watu wema. 86

87. Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na
akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana
mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni
mwa wenye kudhulumu. 87

88. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki.
Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini. 88

89. Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu
Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi. 89

90. Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia
katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu. 90

91. Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia
katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu. 91

92. Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni
Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi. 92

93. Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina
yao. Wote watarudi kwetu. 93

94. Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa
juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia. 94

95. Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba
hawatarejea, 95

96. Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa
wanateremka kutoka kila mlima; 96

97. Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo
kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa
tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu. 97

98. Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya
Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu. 98

9. Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote
watadumu humo. 99

100. Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia
(jenginelo). 100

101. Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao
watatenganishwa na hayo. 101

102.
Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika
yale zinayo yatamani nafsi zao. 102

103.
Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na
Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa! 103

104.
Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa
karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni
ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao. 104

105. Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya
Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema. 105

106.
Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao
ibada. 106

107.
Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu
wote. 107

108.
Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika
Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu? 108

109. Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni
sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa. 109

110.
Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua
myafichayo. 110

111.
Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na
starehe mpaka muda kidogo. 111

112.
Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola
wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua; 112
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani