Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba
mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru
wanawafanya wengine sawa na Mola wao Mlezi. 1

2. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha
akakuhukumieni ajali, na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi
mnatia shaka. 2

3. Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini.
Anajua ya ndani yenu na ya nje yenu. Na anajua mnayo yachuma. 3

4. Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za Mola
wao Mlezi ila wao huwa wenye kuipa nyongo. 4

5.
Wameikanusha Haki ilipo wajia. Basi zitawajia khabari
za yale waliyo kuwa wakiyakejeli. 5

6. Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla
yao? Tuliwaweka katika nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi
na tukaifanya mito inapita chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao;
na tukaanzisha baada yao kizazi kingine. 6

7. Na lau tungeli kuteremshia kitabu cha karatasi,
wakakigusa kwa mikono yao, wangeli sema walio kufuru: Haya si chochote ila ni
uchawi dhaahiri. 7

8. Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama
tungeli teremsha Malaika, basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo
wasingeli pewa muhula. 8

9. Na kama tungeli mfanya Malaika bila ya shaka tungeli
mfanya kama binaadamu, na tungeli watilia matatizo yale wanayo yatatiza wao. 9

10. Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa
kejeli, lakini walio wafanyia kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa
wao wanayafanyia kejeli. 10

11. Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje
mwisho wa wanao kanusha. 11

12. Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika
ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu.
Hakika atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri
wenyewe hawaamini. 12

13. Na ni vyake vilio tulia usiku na mchana. Naye ndiye
Mwenye kusikia na Mwenye kujua. 13

14. Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa
Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala
halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala
kabisa usiwe miongoni wa washirikina. 14

15. Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku kubwa hiyo ikiwa
nitamuasi Mola wangu Mlezi. 15

16. Siku hiyo yule atakaye epushwa nayo adhabu hiyo
atakuwa Mwenyezi Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio wazi. 16

17. Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi
hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye
ndiye Mwenye uweza wa kila kitu. 17

18. Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye
Mwenye hikima na Mwenye khabari zote. 18

19. Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema:
Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa
Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi
mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi
sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao
washirikisha. 19

20. Wale Tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo
wajua watoto wao. Wale walio zikhasiri nafsi zao hawaamini. 20

21. Na nani dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo
Mwenyezi Mungu, na akazikanusha Ishara zake? Hakika madhaalimu hawafanikiwi. 21

22. Siku tutapo wakusanya wote pamoja, kisha tuwaambie
walio shirikisha: Wako wapi washirikishwa wenu mlio kuwa mnadai? 22

23. Kisha hautakuwa udhuru wao ila ni kusema: Wallahi!
Mola wetu Mlezi! Hatukuwa washirikina. 23

24. Tazama jinsi wanavyo jisemea uwongo wenyewe. Na
yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua. 24

25. Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza; na tumezitia
pazia nyoyo zao wasije kuyafahamu. Na upo uziwi masikioni mwao, na wakiona kila
Ishara hawaiamini. Hata wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema walio kufuru:
Hizi si chochote ila hadithi za watu wa kale. 25

26. Nao huwazuia watu, na wao wenyewe wanajitenga nayo.
Nao hawaangamizi ila nafsi zao tu, wala wao hawatambui. 26

27. Na unge ona watakapo simamishwa kwenye Moto, wakawa
wanasema: Laiti tungeli rudishwa, wala hatutakanusha tena Ishara za Mola wetu
Mlezi, na tutakuwa miongoni wa Waumini. 27

28. Bali yamewadhihirikia waliyo kuwa wakiyaficha
zamani. Na kama wangeli rudishwa bila ya shaka wange yarejea yale yale waliyo
katazwa. Na hakika hao ni waongo. 28

29. Na walisema: Hakuna mengine ila maisha yetu haya ya
duniani, wala sisi hatutafufuliwa. 29

30. Na lau ungeli ona watavyo simamishwa mbele ya Mola
wao Mlezi, akawaambia: Je, si kweli haya? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa
Mola Mlezi wetu ni kweli. Yeye atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile
mlivyo kuwa mnakataa. 30

31. Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na
Mwenyezi Mungu, mpaka ilipo wajia Saa kwa ghafla, wakasema: Ole wetu kwa tuliyo
yapuuza! Nao watabeba mizigo yao juu ya migongo yao. Ni maovu hayo wanayo
yabeba. 31

32. Na maisha ya dunia si chochte ila ni mchezo na
pumbao tu. Na hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanao mcha Mungu. Basi,
je, hamtii akilini? 32

33. Tunajua ya kwamba yanakuhuzunisha wanayo yasema.
Basi hakika wao hawakukanushi wewe, lakini hao madhaalimu wanazikataa Ishara za
Mwenyezi Mungu. 33

34. Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao
wakavumilia kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na
hapana wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia
baadhi ya khabari za Mitume hao. 34

35. Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi
kama unaweza kutafuta njia ya chini kwa chini ya ardhi, au ngazi kwendea
mbinguni ili uwaletee Ishara -- Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa angeli
wakusanya kwenye uwongofu. Basi usiwe miongoni mwa wasio jua. 35

36. Hakika wanao kubali ni wale wanao sikia. Na ama wafu
Mwenyezi Mungu atawafufua, na kisha kwake Yeye ndio watarejeshwa. 36

37. Hakika wanao kubali ni wale wanao sikia. Na ama wafu
Mwenyezi Mungu atawafufua, na kisha kwake Yeye ndio watarejeshwa. 37

38. Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka
kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu
chochote. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa. 38

39. Na walio kanusha Ishara zetu ni viziwi na mabubu
waliomo gizani. Mwenyezi Mungu humwachia kupotea amtakaye, na humweka katika
Njia iliyo nyooka amtakaye. 39

40. Sema: Mwaonaje ikikujieni adhabu ya Mwenyezi Mungu,
au ikakufikieni hiyo Saa - mtamwomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni
wakweli? 40

41. Bali Yeye ndiye mtakaye mwomba, naye atakuondoleeni
mnacho mwombea akipenda. Na mtasahau hao mnao wafanya washirika wake. 41

42. Na kwa yakini tulipeleka Mitume kwa kaumu zilizo
kuwa kabla yako, kisha tukazitia katika dhiki na mashaka ili zipate kunyenyekea.
42

43. Kwa nini wasinyenyekee ilipo wafika adhabu yetu?
Lakini nyoyo zao zilikuwa ngumu, na Shet'ani akawapambia waliyo kuwa
wakiyafanya. 43

44. Basi walipo sahau walio kumbushwa tuliwafungulia
milango ya kila kitu. Mpaka walipo furahia yale waliyo pewa tuliwashika kwa
ghafla, na mara wakawa wenye kukata tamaa. 44

45. Ikakatwa mizizi ya watu walio dhulumu - na wa
kuhimidiwa ni Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. 45

46. Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu akanyakua kusikia
kwenu, na kuona kwenu, na akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani asiye kuwa
Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni hayo tena? Angalia vipi tunavyo zieleza Ishara,
kisha wao wanapuuza. 46

47. Sema: Mwaonaje, ikikufikieni adhabu ya Mwenyezi
Mungu kwa ghafla, au kwa dhaahiri, jee wataangamizwa isipo kuwa walio dhulumu? 47

48. Na hatuwatumi Mitume ila huwa ni wabashiri na
waonyaji. Na wenye kuamini na wakatenda mema haitakuwa khofu juu yao, wala
hawatahuzunika. 48

49. Na walio kanusha Ishara zetu itawagusa adhabu kwa
walivyo kuwa wakipotoka. 49

50. Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za
Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyo fichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni
Malaika. Mimi sifuati ila yanayo funuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa,
kipofu na mwenye kuona. Basi hamfikiri? 50

51. Na waonye kwayo wanao ogopa kuwa watakusanywa kwa
Mola wao Mlezi, hali kuwa hawana mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye, ili
wapate kuchamngu. 51

52. Wala usiwafukuze wanao mwomba Mola Mlezi wao asubuhi
na jioni kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu
yako si juu yao hata kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye kudhulumu.
52

53. Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili
waseme: Ni hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani
Mwenyezi Mungu hawajui wanao shukuru? 53

54. Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie:
Assalamu alaikum! Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya
kwamba atakaye fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na
akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. 54

55. Na ndio hivi tunavyo zieleza Ishara ili ibainike
njia ya wakosefu. 55

56. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba
badala ya Mwenyezi Mungu. Sema: mimi sifuati matamanio yenu. Hivyo nitakuwa
nimepotea, na sitakuwa miongoni mwa walio ongoka. 56

57. Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa
Mola wangu Mlezi, nanyi mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana
hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa
kuhukumu kuliko wote. 57

58. Sema: Lau kuwa ninacho hicho mnacho kihimiza, ingeli
kwisha katwa shauri baina yangu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu anawashinda wote
kuwajua madhaalimu. 58

59. Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila
Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila
analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo
katika Kitabu kinacho bainisha. 59

60. Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho
fanya mchana. Kisha Yeye hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe.
Kisha kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya. 60

61. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya
waja wake. Na hukupelekeeni waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe
wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri. 61

62. Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa
Haki. Hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu. 62

63. Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi
kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa
na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru. 63

64. Sema: Mwenyezi Mungu hukuokoeni kutoka hayo, na
kutoka kila mashaka, na kisha nyinyi mnamshirikisha! 64

65. Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka
juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na
kuwaonjesha baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili
wapate kufahamu. 65

66. Na watu wako wameikanusha, nayo ni Haki. Sema: Mimi
sikuwakilishwa juu yenu. 66

67. Kila khabari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua. 67

68. Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi
jitenge nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani
akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu. 68

69. Wala wamchao Mungu hawana jukumu lolote kwao, lakini
ni kukumbusha, asaa wapate kujiepusha. 69

70.
Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na
pumbao, na uhai wa dunia ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi
ikaangamizwa kwa sababu ya iliyo yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila
Mwenyezi Mungu. Na ingatoa kila fidia haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa
kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto
kabisa, na adhabu chungu. 70

71. Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae
hatufai wala hatudhuru, na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi?
Tuwe kama ambao mashet'ani wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki
wanao mwita ende kwenye uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika uwongofu
wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola Mlezi wa
viumbe vyote, 71

72. Na mshike Sala, na mcheni Yeye, na kwake Yeye ndiko
mtako kusanywa. 72

73. aye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na
anaposema: Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku
litapo pulizwa barugumu, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye
Mwenye hikima na Mwenye khabari. 73

74. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar:
Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo
katika opotofu ulio wazi. 74

75. Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu
na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini. 75

76. Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu
ni Mola Mlezi wangu. Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua. 76

77. Alipo uona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola
Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa
katika kaumu walio potea. 77

78. Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye
Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu!
Mimi simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina. 78

79. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa
aliye ziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina. 79

80. Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu
ya Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha
naye, ila Mola wangu Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya
kila kitu. Basi je, hamkumbuki? 80

81. Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali
nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho
hakukiteremshia uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi
kupata amani, kama nyinyi mnajua? 81

82. Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao
na dhulma - hao ndio watakao pata amani na wao ndio walio ongoka. 82

83. Na hizo ndizo hoja zetu tulizo mpa Ibrahim kuhojiana
na watu wake. Tunamnyanyua kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye
hikima na Mwenye ujuzi. 83

84. Na tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila
mmoja wao tulimwongoa. Na Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake
tulimwongoa Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo
tunavyo walipa wafanyao wema. 84

85. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas. Wote walikuwa
miongoni mwa watu wema. 85

86. Na Ismail, na Al Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na wote
tuliwafadhilisha juu ya walimwengu wote. 86

87. Na kutokana na baba zao, na vizazi vyao na ndugu
zao. Na tukawateuwa na tukawaongoa kwenye Njia iliyo nyooka. 87

88. Hiyo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo humhidi
amtakaye katika waja wake. Na lau wangeli mshirikisha yangeli waharibikia waliyo
kuwa wakiyatenda. 88

89. Hao ndio tulio wapa Vitabu na hukumu na Unabii.
Ikiwa hawa watayakataa hayo, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasio yakataa.
89

90. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewahidi. Basi fuata
hidaya yao. Sema: Mimi sikuombeni ujira. Haya hayakuwa ila ni mawaidha kwa
walimwengu wote. 90

91. Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri
yake, walipo sema: Mwenyezi Mungu hakumteremshia mwanaadamu chochote. Sema: Nani
aliyo teremsha Kitabu alicho kuja nacho Musa, chenye nuru na uwongofu kwa watu,
mlicho kifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha. Na mkafunzwa
mlio kuwa hamyajui nyinyi wala baba zenu? Sema: Mwenyezi Mungu. Kisha waache
wacheze katika porojo lao. 91

92. Na hiki ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho
barikiwa, chenye kuhakikisha yaliyo tangulia, na ili uuwonye Mama wa Miji na
walio pembezoni mwake. Na wenye kuamini Akhera wanakiamini hichi, nao
wanazihifadhi Sala zao. 92

93. Nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzuliya
uwongo Mwenyezi Mungu, au anaye sema: Mimi nimeletewa wahyi; na hali hakuletewa
wahyi wowote. Na yule anaye sema: Nitateremsha kama alivyo teremsha Mwenyezi
Mungu. Na lau ungeli waona madhaalimu wanavyo kuwa katika mahangaiko ya mauti,
na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa
adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu
yasiyo ya haki, na mlivyo kuwa mkizifanyia kiburi Ishara zake. 93

94. Nanyi mlitujia wapweke kama tulivyo kuumbeni mara ya
kwanza. Na mkayaacha nyuma yenu yote tuliyo kupeni, na wala hatuwaoni hao
waombezi wenu, ambao mlidai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu.
Yamekatika makhusiano baina yenu, na yamekupoteeni mliyo kuwa mkidai. 94

95. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa,
zikachipua. Humtoa aliye hai kutoka maiti, naye ni mtoaji maiti kutokana na
aliye hai. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu. Basi vipi mnageuzwa? 95

96. Ndiye anaye pambazua mwangaza wa asubuhi; na
ameufanya usiku kwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi kwenda kwa hisabu.
Hayo ndiyo makadirio ya Aliye tukuka Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi. 96

97. Na Yeye ndiye aliye kuwekeeni nyota ili mwongoke
kwazo katika kiza cha bara na bahari. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu
wanao jua. 97

98. Na Yeye ndiye aliye kuzalisheni kutokana na nafsi
moja. Pako pahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezichambua Ishara hizi
kwa watu wanao fahamu.98

99. Na Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka mbinguni;
na kwayo tunatoa mimea ya kila kitu. Kutokana na baadhi yao tukatoa mimea ya
majani, tukatoa ndani yake punje zilizo pandana; na kutokana na mitende yakatoka
kwenye makole yake mashada yaliyo inama; na bustani za mizabibu na mizaituni, na
makomamanga, yaliyo fanana na yasiyo fanana. Angalieni matunda yake yanapo zaa
na yakawiva. Hakika katika hayo pana Ishara kwa watu wanao amini. 99

100. Bado wamemfanyia Mwenyezi Mungu majini kuwa
washirika wake, na hali Yeye ndiye aliye waumba. Na wakamzulia, bila ya ujuzi
wowote, kuwa ana wana wa kiume na wa kike. Subhanahu, Ametakasika na ametukuka
juu ya hayo wanayo mbandikiza nayo! 100

101. Yeye ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ya
ruwaza. Itakuwaje awe na mwana naye hakuwa na mke? Naye ndiye aliye umba kila
kitu. Naye ni Mwenye kujua kila kitu. 101

102. Huyo ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu,
hapana mungu ila Yeye, Muumba wa kila kitu. Basi muabuduni Yeye tu. Naye ni
Mtegemewa wa kila kitu. 102

103. Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho.
Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari. 103

104.
Zimekwisha kukujieni hoja wazi kutoka kwa Mola wenu
Mlezi. Basi anaye ona ni kwa faida yake mwenyewe, na anaye pofuka basi ni
khasara yake. Nami si mtunzaji wenu. 104

105. Na namna hivyo tunazisarifu Aya, na wao wakwambie:
Umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanao jua. 105

106. Fuata uliyo funuliwa kutoka kwa Mola wako Mlezi.
Hapana mungu ila Yeye. Na jitenge na washirikina. 106

107. Na lau Mwenyezi Mungu angeli penda, wasingeli
shiriki. Na Sisi hatukukufanya wewe uwe mtunzaji wao. Wala wewe si mlinzi juu
yao. 107

108. Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya
Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya
kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao
yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda. 108

109. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo
vyao, kuwa ikiwafikia Ishara wataiamini. Sema: Ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu.
Na nyinyi hamjui kuwa zitapo kuja hawato amini. 109

110. Nasi twazigeuza nyoyo zao na macho yao. Kama
walivyo kuwa hawakuamini mara ya kwanza, tunawaacha katika maasi yao
wakitangatanga. 110

111. NA LAU kuwa tungeli wateremshia Malaika, na maiti
wakazungumza nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, bado wasingeli amini,
ila Mwenyezi Mungu atake. Lakini wengi wao wamo ujingani. 111

112. Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui
mashet'ani wa kiwatu, na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya
kupamba-pamba, kwa udanganyifu. Na angeli penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya
hayo. Basi waache na wanayo yazua. 112

113. Na ili nyoyo za wasio amini Akhera zielekee hayo,
nao wayaridhie na wayachume wanayo yachuma. 113

114. Je, nimtafute hakimu ghairi ya Mwenyezi Mungu, naye
ndiye aliye kuteremshieni Kitabu kilicho elezwa waziwazi? Na hao tulio wapa
Kitabu wanajua ya kwamba kimeteremshwa na Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi usiwe
katika wanao tia shaka. 114

115. Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na
uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia
na Mwenye kujua. 115

116. Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani
watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa
ila ni wenye kusema uwongo tu. 116

117.
Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote
kuwajua walio potea Njia yake, na ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua walio
hidika. 117

118. Basi kuleni katika walio somewa jina la Mwenyezi
Mungu, ikiwa mnaziamini Aya zake. 118

119. Na kwa nini msile katika walio somewa jina la
Mwenyezi Mungu, naye amekwisha kubainishieni alivyo kuharimishieni, isipo kuwa
vile mnavyo lazimishwa? Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya
kuwa na ilimu. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua wanao
pindukia mipaka. 119

120. Na acheni dhambi zilizo dhaahiri na zilizo
fichikana. Hakika wanao chuma dhambi watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyachuma. 120

121. Wala msile katika wale wasio somewa jina la
Mwenyezi Mungu. Kwani huo ni upotofu. Na kwa yakini mashet'ani wanawafunza
marafiki zao kubishana nanyi. Na mkiwafuata basi hapana shaka nyinyi mtakuwa
washirikina. 121

122. Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na
tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani
akawa hata hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa
wakiyafanya. 122

123.
Kadhaalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa
wakosefu wao wafanye vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa
nafsi zao, nao hawatambui. 123

124. Na inapo wajia Ishara, wao husema: Hatutoamini
mpaka tupewe mfano wa walio pewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye
Mjuzi kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao walio kosa
udhalili na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo
kuwa wakivifanya. 124

125. Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi
humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake
kina dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu
anajaalia uchafu juu ya wasio amini. 125

126. Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka.
Tumezipambanua Aya kwa watu wanao kumbuka. 126

127. Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao.
Naye ndiye Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda. 127

128. Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi
makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na
marafiki zao katika wanaadamu waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na
wao. Na tumefikia ukomo wetu ulio tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto
ndio makaazi yenu, mtadumu humo, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako
Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua. 128

129. Ndio kama hivi tunawaelekeza madhaalimu wapendane
wao kwa wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma. 129

130. Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni
Mitume kutokana na nyinyi wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni
mkutano wa Siku yenu hii. Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na
yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa
makafiri. 130

131. Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa
wa kuiangamiza miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika. 131

132. Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale
waliyo yatenda. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
132

133. Na Mola wako Mlezi ndiye Mkwasi, Mwenye rehema.
Akipenda atakuondoeni na awaweke wengine awapendao badala yenu, kama vile alivyo
kutoeni kutokana na uzazi wa watu wengine. 133

134. Bila ya shaka hayo mnayo ahidiwa yatafika tu, wala
nyinyi hamtaweza kuyaepuka. 134

135. Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni muwezayo, na hakika
mimi nafanya. Mtakuja jua nani atakuwa na makaazi mema mwishoni. Hakika
madhaalimu hawatafanikiwa. 135

136. Na wamemwekea sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea na
wanyama alio umba, nao husema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai yao -
na hii ni ya miungu tunao washirikisha. Basi vile walivyo wakusudia miungu yao
havimfikii Mwenyezi Mungu, na vilivyo kuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia miungu
yao. Ni uovu kabisa hayo wanayo yahukumu. 136

137. Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi
katika washirikina kuwauwa watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo
wanayo yazua. 137

138. Nao husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko.
Hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao tu. Na wanyama hawa imeharimishwa
migongo yao kupandwa. Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu
yao. Wanamzulia uwongo tu Mwenyezi Mungu. Atawalipa kwa hayo wanayo mzulia. 138

139. Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni
kwa ajili ya wanaume wetu tu, na wameharimishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa
nyamafu basi wanashirikiana. Mwenyezi Mungu atawalipa kwa maelezo yao hayo.
Hakika Yeye ni Mwenye hikima, Mwenye kujua. 139

140.
Hakika wamekhasirika wale ambao wamewauwa watoto
wao kwa upumbavu pasipo kujua, na wakaharimisha alivyo waruzuku Mwenyezi Mungu
kwa kumzulia Mwenyezi Mungu. Hakika wamepotea, wala hawakuwa wenye kuongoka. 140

141. Na Yeye ndiye aliye ziumba bustani zenye kutambaa
juu ya chanja, na zisio tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali,
na mizaituni na mikomamanga inayo fanana na isiyo fanana. Kuleni matunda yake
inapo zaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo.
Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo. 141

142. Na katika wanyama amekujaalieni wenye kubeba mizigo
na kutoa matandiko. Kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, wala
msifuate nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu dhaahiri. 142

143.
Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika
kondoo, na wawili katika mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au
majike wawili, au waliomo matumboni mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu
ikiwa nyinyi mnasema kweli 143

144. .Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe.
Sema: Je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni
mwa yote majike? Au, nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya? Basi
ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa
ajili ya kuwapoteza watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi watu
madhaalimu. 144

145. Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu
kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo
mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa
kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila
ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu. 145

146. Na wale walio fuata dini ya Kiyahudi
tumewaharimishia kila mwenye kucha. Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi
tumewaharimishia shahamu yao, isipo kuwa ile iliyo beba migongo yao au matumbo
yao, au iliyo gandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na
bila ya shaka Sisi ndio wasema kweli. 146

147.
Wakikukanusha basi wewe sema: Mola Mlezi wenu ni
Mwenye rehema iliyo enea. Wala haizuiliki adhabu yake kwa watu wakhalifu. 147

148.
Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu
ange taka tusingeli shiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu
chochote. Vivi hivi walikanusha walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu
yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala
hamsemi ila uwongo tu. 148

149. Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya
kukata. Na kama angeli penda angeli kuhidini nyote. 149

150. Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa
Mwenyezi Mungu ameharimisha hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja
nao. Wala usifuate matamanio ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini
Akhera, na ambao wanamlinganisha Mola Mlezi wao na wengine. 150

151. Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola
wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu
wafanyieni wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi
tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayo onekana, na
yanayo fichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa,
ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini. 151

152. Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya
wema kabisa, mpaka afikilie utu-uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa
uadilifu. Sisi hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo
semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni.
Hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka. 152

153. Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka.
Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya
amekuusieni ili mpate kuchamngu. 153

154. Tena tulimpa Musa Kitabu kwa kumtimizia (neema)
aliye fanya wema, na kuwa ni maelezo ya kila kitu, na uwongofu na rehema, ili
wapate kuamini mkutano wao na Mola wao Mlezi. 154

155. Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho
barikiwa. Basi kifuateni, na mchenimngu, ili mrehemewe. 155

156. Msije mkasema: Hakika mataifa mawili kabla yetu
yameteremshiwa Kitabu; na sisi tulikuwa hatuna khabari ya waliyo kuwa
wakiyasoma. 156

157. Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu
tungeli kuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola
wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko
yule anaye kanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa
wanao jitenga na Ishara zetu adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga kwao. 157

158.
Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au
awafikie Mola wako Mlezi, au zifike baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku
zitakapo fika baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu
kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake.
Sema: Ngojeni, nasi pia tunangoja. 158

159.
Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi
makundi, huna ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi
Mungu; kisha atawaambia yale waliyo kuwa wakiyatenda. 159

160.
Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na
afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa. 160

161. Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa
kwenye Njia Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim
aliye kuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina. 161

162. Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai
wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe
vyote. 162

163. Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa,
na mimi ni wa kwanza wa Waislamu. 163

164. Sema: Je nitafute Mola Mlezi asiye kuwa Mwenyezi
Mungu, na hali Yeye ndiye Mola Mlezi wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila
nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa
Mola wenu Mlezi, naye atakuambieni mliyo kuwa mkikhitalifiana. 164

165. Naye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na
amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa
hayo aliyo kupeni. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye
ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. 165
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani