Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. ALIF LAM MYM 'SAAD 1

2. Kitabu kilicho teremshwa kwako - basi isiwe dhiki
kifuani kwako kwa ajili yake, upate kuonya kwacho, na kiwe ni ukumbusho kwa
Waumini. 2

3. Fuateni mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu,
wala msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake. Ni machache mnayo
yakumbuka. 3

4. Na miji mingapi tuliiangamiza, ikaifikia adhabu yetu
usiku au walipo kuwa wamelala adhuhuri. 4

5. Basi hakikuwa kilio chao ilipo wafikia adhabu yetu,
isipo kuwa kusema: Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu. 5

6. Na kwa yakini tutawauliza wale walio pelekewa Ujumbe,
na pia tutawauliza hao Wajumbe. 6

7. Tena tutawasimulia kwa ilimu; wala Sisi hatukuwa
mbali 7

8. Na Siku hiyo kipimo kitakuwa kwa Haki. Basi watakao
kuwa na uzani mzito, hao ndio watakao fanikiwa. 8

9. Na watakao kuwa na uzani khafifu, basi hao ndio walio
zitia khasarani nafsi zao kwa sababu ya kuzipinga Ishara zetu.9

10. Na hakika tumekuwekeni katika ardhi, na
tumekujaalieni humo njia za kupatia maisha. Ni kuchache kushukuru kwenu. 10

11. 11

12. Mwenyezi Mungu akasema: Nini kilicho kuzuia
kumsujudia nilipo kuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa
moto, naye umemuumba kwa udongo12

13. Akasema: Basi teremka kutoka humo! Haikufalii
kufanya kiburi humo. Basi toka! Hakika wewe u miongoni mwa walio duni. 13

14. Akasema: Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa. 14

15. Akasema: Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula 15

16. Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi
nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka.16

17. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani
kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani.17

18. Akasema: Toka humo, nawe umekwisha fedheheka,
umekwisha fukuzwa. Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza
Jahannam kwa nyinyi nyote18

19. Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii,
na kuleni humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio
dhulumu19

20. Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia
tupu zao walizo fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila
msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele. 20

21. Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao
kunasihini. 21

22. Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti,
tupu zao zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao
Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni
adui yenu wa dhaahiri?22

23.
Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu,
na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.23

24. Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi
maadui. Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike
muda. 24

25. Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka
humo mtatolewa 25

26. Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha
tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika
Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka.26

27. Eny wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama
alivyo watoa wazazi wenu Peponi, akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika
yeye na kabila yake wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya
Mashet'ani kuwa ni marafiki wa wasio amini. 27

28. Na wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta
nayo baba zetu, na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu
haamrishi mambo machafu. Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua? 28

29. Sema: Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu, na
mumuelekeze nyuso zenu kila mnapo sujudu, na muombeni Yeye kwa kumsafia Dini.
Kama alivyo kuumbeni mwanzo ndivyo mtavyo rudi,29

30. Hali ya kuwa kundi moja amelihidi, na kundi jengine
limethibitikiwa na upotofu. Kwa hakika hao waliwafanya mashet'ani kuwa ndio
marafiki walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka. 30

31. Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila
pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa
hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu. 31

32. Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi
Mungu alilo watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni
kwa walio amini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu.
Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua. 32

33. Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya
dhaahiri na ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi
Mungu na asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua. 33

34. Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao
basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia. 34

35. Enyi wanaadamu! Watakapo kufikieni Mitume miongoni
mwenu wakakuelezeni Ishara zangu, basi watakao mchamngu na wakatengenea
haitakuwa khofu kwao, wala hawatahuzunika.35

36. Na wale watakao kanusha Ishara zetu na wakazifanyia
kiburi, hao ni watu wa Motoni; humo watadumu.36

37. Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye
mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia
sehemu yao waliyo andikiwa, mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha,
watawaambia: Wako wapi mlio kuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema:
Wametupotea! Na watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri.37

38. Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na
umma zilizo pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma
utawalaani wenzake. Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema
wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya
Motoni marudufu. Atasema: Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
38

39. Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi
nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyo
kuwa mkiyachuma 39

40. Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na
wakazifanyia kiburi hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi
mpaka apite ngamia katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa
wakosefu. 40

41.
Jahannamu itakuwa kitanda chao na juu yao nguo za
moto za kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.41

42. Na wale wanao amini na wakatenda mema -
hatumkalifishi mtu yoyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa
Peponi. Wao watadumu humo. 42

43. Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe
inapita mito. Na watasema: Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu,
ambaye aliye tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli
kuwa Mwenyezi Mungu hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki.
Na watanadiwa kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa
mkiyafanya. 43

44. Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi
tumekuta aliyo tuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta
aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji
atawatangazia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu, 44

45. Wale ambao walikuwa wakizuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu, na wakataka kuipotosha, nao wanaikanusha Akhera. 45

46. Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na
juu ya Mnyanyuko patakuwa watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao
watawaita watu wa Peponi: Assalamu Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado hawajaingia
humo, lakini wanatumai.46

47. Na yanapo geuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni,
watasema: Mola Mlezi wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu walio dhulumu. 47

48. Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao
wajua kwa alama zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho
mlicho kuwa mnafanyia kiburi. 48

49. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi
Mungu hatawafikishia rehema. Ingieni Peponi, hapana khofu kwenu, wala
hamtahuzunika! 49

50. Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi:
Tumimieni maji, au chochote alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema:
Hakika Mwenyezi Mungu ameviharimisha hivyo kwa makafiri,50

51. Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo,
na maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo Sisi tunawasahau kama walivyo usahau
mkutano wa Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu. 51

52. Na hakika tumewaletea Kitabu tulicho kipambanua kwa
ilimu, uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini. 52

53. Je, lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake?
Siku yatapo fika matokeo yake watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola
Mlezi wetu walileta Haki! Je, tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili
tufanye yasiyo kuwa yale tuliyo kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri
nafsi zao, na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua. 53

54. Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye
ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi.
Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota
zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.54

55. Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa
siri. Hakika Yeye hawapendi warukao mipaka.55

56. Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa
imekwisha tengenezwa. Na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya
Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao fanya mema.56

57. Na Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni
bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito
tunayachunga mpaka kwenye nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio
kama hivyo tukatolesha kila aina ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo
wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.57

58. Na ardhi njema, yenye udongo wa rutba, hutoa mimea
yenye kukua vizuri yenye uhai, kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Na ardhi mbaya
haitoi ila mimea michache, isiyo na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo
tunavyo zipambanua Ishara (Aya) kwa watu wanao shukuru.58

59.
Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi
kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi
ninakukhofieni adhabu ya Siku iliyo kuu. 59

60. Wale watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika
sisi tunakuona wewe umo katika upotofu ulio dhaahiri.60

61. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu,
lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. 61

62.
Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na
ninakunasihini; na ninayajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi. 62

63. Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa
Mola Mlezi wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na
ili mumchemngu, na ili mpate kurehemewa?63

64. Basi walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na walio
kuwa pamoja naye katika jahazi. Na tukawazamisha wale walio kanusha Ishara zetu.
Hakika hao walikuwa watu vipofu. 64

65. Na kwa A'adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema:
Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je,
hamumchi? 65

66. Wakasema watukufu wa wale walio kufuru katika kaumu
yake: Sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe
ni katika waongo.66

67. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini
mimi ni Mtume niliye toka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. 67

68.
Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi
kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu. 68

69. Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa
Mola wenu Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni
alivyo kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo.
Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.69

70.
Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu
peke yake, na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo
unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.70

71. Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha
kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu
mliyo yaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha
uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja. 71

72. Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye kwa
rehema zetu, na tukakata mizizi ya wale walio zikanusha Ishara zetu, na hawakuwa
wenye kuamini.72

73. Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema:
Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika
imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni
ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye
ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu. 73

74. Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa
A'adi na akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika
nyanda zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za
Mwenyezi Mungu wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi.74

75.
Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia
wanao onewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa
na Mola Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa. 75

76. Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo
mnayo yaamini. 76

77. Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola
Mlezi wao, na wakasema: Ewe Saleh! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni
mwa Mitume.77

78. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha
wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa.78

79. Basi Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu!
Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi
hamwapendi wenye nasaha.79

80. Na tulimtuma Lut', alipo waambia watu wake: Je,
mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe
vyote! 80

81. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio
mkwawacha wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji! 81

82. Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipo kuwa
kuambizana: Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanao jitakasa. 82

83. Basi tukamwokoa yeye na watu wake, isipo kuwa mkewe,
alikuwa miongoni mwa walio bakia nyuma.83

84. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyo kuwa
mwisho wa wakosefu. 84

85. Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib.
Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo
kuwa Yeye. Imekwisha kufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi
timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala
msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo
bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.85

86. Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na
kuwazuilia na Njia ya Mwenyezi Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia
ipotoke. Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na
tazameni jinsi ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi. 86

87. Na kama liko kundi miongoni mwenu lililo amini haya
niliyo tumwa, na kundi jengine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu
ahukumu baina yetu. Naye ndiye Mbora wa wenye kuhukumu.87

88.
WAHESHIMIWA WALIO TAKABARI katika kaumu yake
wakasema: Ewe Shua'ib! Tutakutoa wewe pamoja na wale walio kuamini katika mji
wetu, au mrejee katika mila yetu. Akasema: Je, ingawa tunaichukia? 88

89. Bila ya shaka itakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi
Mungu tukirudi katika mila yenu baada ya kwisha tuokoa nayo Mwenyezi Mungu. Wala
haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi
wetu. Ujuzi wa Mola Mlezi wetu umeenea katika kila kitu. Kwa Mwenyezi Mungu
tunategemea. Ewe Mola Mlezi wetu! Tuhukumie baina yetu na kaumu yetu kwa haki,
nawe ndiye mbora wa wanao hukumu. 89

90. Na waheshimiwa walio kufuru katika kaumu yake
wakasema: Mkimfuata Shua'ib, basi hakika hapo nyinyi mtakuwa mlio khasiri.90

91. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na wakaamkia
majumbani mwao wamejifudikiza, wamekwisha kufa.91

92. Wale walio mkanusha Shua'ib wakawa kama kwamba
hawakuwako. Walio mkanusha Shua'ib ndio walio kuwa wenye kukhasiri.92

93. Basi akawaachilia mbali na akasema: Enyi kaumu
yangu! Nimekufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na nimekunasihini; basi vipi
niwahuzunikie watu makafiri? 93

94. Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji ila
tuliwapatiliza wakaazi wake kwa taabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.94

95. Kisha Sisi hubadilisha mahala pa ubaya kwa wema,
hata wakazidi, na wakasema: Taabu na raha ziliwafikia baba zetu. Basi kwa ghafla
tukawashika, hali ya kuwa hawajatambua. 95

96. Na lau kuwa watu wa miji wangeli amini na
wakamchamngu, kwa yakini tungeli wafungulia baraka kutoka mbinguni na katika
ardhi. Lakini walikanusha basi tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyo kuwa
wakiyachuma.96

97. Je, watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu
haitawafika usiku, nao wamelala?97

98. Au watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu
haitawafika mchana, nao wanacheza?98

99 . Je, wamejiaminisha na mipango ya Mwenyezi Mungu?
Kwani hawajiaminishi na mipango ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye kukhasiri.99

100. Je, hawahidiki hawa wanao rithi ardhi baada ya wale
wenyewe kwamba tukitaka tutawapatiliza kwa madhambi yao, na tutapiga muhuri juu
ya nyoyo zao, na kwa hivyo hawatasikia? 100

101. Miji hiyo, tunakusimulia baadhi ya khabari zake. Na
hapana shaka Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo waziwazi. Lakini hawakuwa
wenye kuamini waliyo yakanusha zamani. Namna hivi Mwenyezi Mungu anazipiga
muhuri nyoyo za makafiri.101

102. Wala hatukuwaona wengi wao kuwa wanatimiza ahadi;
bali kwa hakika tuliwakuta wengi wao ni wapotofu. 102

103. Kisha baada yao tukamtuma Musa na Ishara zetu kwa
Firauni na waheshimiwa wake. Nao wakazikataa. Basi tazama ulikuwaje mwisho wa
waharibifu. 103

104. Na Musa alisema: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume
nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.104

105.
Inafaa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila lilio la
Haki. Nami hakika nimekujieni na dalili waziwazi kutokana na Mola Mlezi wenu.
Basi waache Wana wa Israili wende nami.105

106.
Akasema Firauni: Ikiwa umekuja na Ishara, basi
ilete ukiwa ni katika wasemao kweli.106

107. Basi akaitupa fimbo yake, na mara ikawa nyoka
dhaahiri. 107

108. Na akatoa mkono wake, mara ukawa mweupe kwa
watazamao. 108

109.
Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Hakika
huyo ni mchawi mjuzi.109

110.
Anataka kukutoeni katika nchi yenu. Basi mnatoa
shauri gani? 110

111.
Wakasema: Mwache kidogo yeye na nduguye, na watume
mijini wakusanyao, 111

112.
Wakuletee kila mchawi mjuzi.112

113.
Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: Hakika
tutapata ujira ikiwa tutashinda.113

114.
Akasema: Naam! Nanyi bila ya shaka mtakuwa katika
wa karibu nami.114

115.
Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe, au tutakuwa
sisi tutao tupa?115

116.
Akasema: Tupeni! Basi walipo tupa waliyazuga macho
ya watu na wakawatia khofu, na wakaleta uchawi mkubwa.116

117. Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako.
Mara ikavimeza vyote vile walivyo vibuni.117

118. Kweli ikathibiti na yakabat'ilika waliyo kuwa
wakiyatenda. 118

119.Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa
wadogo.119

120. Na wachawi wakapoomoka wakisujudu.120

121.
Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa viumbe vyote,121

122. Mola Mlezi wa Musa na Haarun.122

123.
Akasema Firauni: Mmemuamini kabla sijakupeni
idhini? Hizi ni njama mlizo panga mjini mpate kuwatoa wenyewe. Lakini karibu
mtajua! 123

124.
Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu mbali
mbali. Kisha nitakutundikeni misalabani.124

125.
Wakasema: Sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu
Mlezi. 125

126. Nawe hukuudhika nasi ila kwa kuwa tumeziamini
Ishara za Mola Mlezi wetu zilipo tujia. Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie uvumilivu
na utufishe hali ni Waislamu.126

127.
Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Unamuacha
Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na wakuache wewe na miungu yako?
Akasema: Tutawauwa wavulana wao, na tutawaacha hai wanawake wao. Na bila ya
shaka sisi ni wenye nguvu juu yao.127

128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa
Mwenyezi Mungu, na subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Naye humrithisha
amtakaye katika waja wake. Na mwisho ni wa wachamngu.128

129.
Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia, na baada ya
wewe kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamhiliki adui wenu, na
akakufanyeni nyinyi ndio wa kufuatia kushika nchi, ili atazame mtavyo kuja tenda
nyinyi. 129

130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa miyaka
(ya ukame) na kwa upungufu wa mazao, ili wapate kukumbuka.130

131.
Likiwafika jema wakisema: Haya ni haki yetu. Na
likiwafika ovu husema: Musa na walio pamoja naye ni wakorofi. Hakika ukorofi wao
huo unao wafikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui. 131

132. Na wakisema: Hata ukituletea Ishara yoyote kutuzuga
hatuto kuamini. 132

133. Basi tukawapelekea tufani, na nzige, na chawa, na
vyura, na damu, kuwa ni Ishara mbali mbali. Nao wakapanda kiburi, na wakawa watu
wakosefu. 133

134. Na ilipo waangukia adhabu wakasema: Ewe Musa!
Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa aliyo kuahidi. Ukituondolea adhabu hii hapana
shaka tutakuamini, na tutawaachilia Wana wa Israili wende nawe.134

135.
Lakini tukiwaondolea adhabu mpaka muda fulani wao
waufikie, mara wakivunja ahadi yao.135

136. Basi tuliwapatiliza, tuka- wazamisha baharini kwa
sababu walizikanusha Ishara zetu, na wakaghafilika nazo.136

137. Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa
mashariki na magharibi ya ardhi tuliyo ibariki. Na likatimia neno jema la Mola
Mlezi wako juu ya Wana wa Israili, kwa vile walivyo subiri. Na tukayaangamiza
aliyo kuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake, na waliyo kuwa wakiyajenga. 137

138. Na tukawavusha bahari Wana wa Israili, wakafika kwa
watu wanao abudu masanamu yao. Wakasema: Ewe Musa! Hebu tufanyie na sisi miungu
kama hawa walivyo kuwa na miungu. Musa akasema: Hakika nyinyi ni watu msio jua
kitu138

139.
Hakika haya waliyo nayo watu hawa yatakuja angamia,
na hayo waliyo kuwa wakiyafanya yamepotea bure.139

140.
Akasema: Je, nikutafutieni mungu asiye kuwa
Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye kufadhilisheni juu ya viumbe vyote?140

141. Na pale tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio
kupeni adhabu za mwisho wa uovu. Wakiwauwa wavulana wenu, na wakawaacha hai
wanawake wenu. Na katika hayo yalikuwa majaribio makubwa kutokana na Mola wenu
Mlezi. 141

142.
Tulimuahidi Musa masiku thalathini na tukayatimiza
kwa kumi; ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arubaini. Na Musa akamwambia
nduguye Haarun: Shika mahala pangu kwa watu wangu na utengeneze wala usifuate
njia ya waharibifu.142

143. Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake
Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi
Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi
utaniona. Basi alipo jionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike,
na Musa akaanguka chini amezimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka,
Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.143

144.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Musa! Mimi
nimekuteuwa wende kwa watu na Ujumbe wangu na maneno yangu. Basi chukua niliyo
kupa na uwe katika wanao shukuru. 
145. Na tukamuandikia katika mbao kila kitu, mawaidha na
maelezo ya mambo yote. (Tukamwambia): Basi yashike kwa nguvu na uwaamrishe watu
wako wayashike kwa ubora wake. Nami nitakuonyesheni makaazi ya wapotofu. 145

146.
Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi
katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia
ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu
wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na
wameghafilika nazo.146

147. Na walio zikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera
a'mali zao zimeharibika. Kwani watalipwa ila kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda? 147

148. Na baada yake walimfanya ndama kutokana na mapambo
yao (kumuabudu), kiwiliwili tu kilicho kuwa na sauti. Hivyo, hawakuona kuwa
hawasemezi wala hawaongoi njia? Wakamuabudu, na wakawa wenye kudhulumu.148

149. Na walipo juta na wakaona ya kwamba wamekwisha
potea, walisema: Ikiwa Mola wetu Mlezi hakuturehemu na akatusamehe, bila ya
shaka tutakuwa miongoni mwa walio khasiri.149

150. Na alipo rudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika
na kuhuzunika, alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je,
mmeitangulia amri ya Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na
akamkamata kichwa ndugu yake akimvutia kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa
mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi
usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu.150

151.
(Musa) akasema: Mola Mlezi wangu! Nisamehe mimi na
ndugu yangu, na ututie katika rehema yako. Nawe ni Mwenye kurehemu kushinda wote
wenye kurehemu.151

152.
Hakika wale walio muabudu ndama, itawapata ghadhabu
ya Mola wao Mlezi na madhila katika maisha ya dunia. Na hivi ndivyo tunavyo
walipa wazushi.152

153. Na walio tenda maovu, kisha wakatubia baada yake na
wakaamini, hapana shaka kuwa Mola Mlezi wako baada ya hayo ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.153

154. Na Musa ilipo mtulia ghadhabu aliziokota zile mbao.
Na katika maandiko yake mna uwongofu na rehema kwa wanao mwogopa Mola wao Mlezi.
154

155. Na Musa akawateuwa watu sabiini katika kaumu yake
kwa miadi yetu. Na ulipo fika mtetemeko mkubwa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi!
Ungeli taka ungeli wahiliki wao na mimi zamani! Unatuhiliki kwa waliyo yafanya
wajinga katika sisi? Haya si chochote ila ni mtihani wako, umpoteze umtakaye na
umhidi umtakaye. Wewe ndiye Rafiki Mlinzi wetu. Basi tughufirie na uturehemu. Na
Wewe ndiye mbora wa kughufiria.155

156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika
Akhera. Sisi tumerejea kwako. (Mwenyezi Mungu) akasema: Adhabu yangu nitamsibu
nayo nimtakaye. Na rehema yangu imeenea kila kitu. Lakini nitawaandikia khasa
wanao mchamngu, na wanao toa Zaka, na wale ambao wanaziamini Ishara zetu,156

157Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma
wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye
waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana
waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao.
Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata
nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.157

158. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi
nyote, niliye tumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana
mungu ila Yeye anaye huisha na anaye fisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na
maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka. 158

159.Na katika kaumu ya Musa lipo kundi linao waongoa
watu kwa haki na kwa haki wanafanya uadilifu.159

160. Na tuliwagawanya katika makabila kumi na mbili,
mataifa mbali mbali. Na tulimfunulia Musa walipo muomba maji watu wake
kumwambia: Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatibuka humo chemchem kumi
na mbili, na kila watu wakajua mahali pao pa kunywea. Na tukawafunika kivuli kwa
mawingu, na tukawateremshia Manna na Salwa. Tukawaambia: Kuleni vizuri hivi
tulivyo kuruzukuni. Wala hawakutu- dhulumu Sisi, bali wamejidhulumu wenyewe.160

161. Na pale walipo ambiwa: Kaeni katika mji huu, na mle
humo mpendapo, na semeni: Tufutie dhambi zetu. Na ingieni katika mlango wake kwa
unyenyekevu, tupate kukusameheni makosa yenu. Walio wema tutawazidishia.161

162.
Lakini walio dhulumu miongoni mwao walibadilisha
kauli, sio ile waliyo ambiwa. Basi tukawapelekea adhabu kutoka mbinguni kwa vile
walivyo kuwa wakidhulumu 162

163. Na waulize khabari za mji ulio kuwa kando ya
bahari, wakiivunja Sabato (Jumaamosi ya mapumziko). Samaki walikuwa wakiwajia
juu juu siku ya mapumziko yao, na siku zisio kuwa za kupumzika hawakuwa
wakiwajia. Kwa namna hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya upotovu.163

164. Na kikundi kati yao walisema: Kwa nini mnawawaidhi
watu ambao tangu hapo Mwenyezi Mungu atawateketeza au atawaadhibu adhabu kali?
Wakasema: Ili uwe ni udhuru kwa Mola Mlezi wenu, na huenda nao wakamchamngu.164

165. Basi walipo yasahau waliyo kumbushwa, tuliwaokoa
walio kuwa wakikataza maovu, na tukawatesa walio dhulumu kwa adhabu mbaya kwa
vile walivyo kuwa wakifanya upotovu.165

166.
Walipo jifakharisha katika waliyo kanywa
tuliwaambia: Kuweni manyani wa kudharauliwa.166

167. Na pale alipo tangaza Mola wako Mlezi kwamba hapana
shaka atawaletea watu ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya mpaka Siku ya Kiyama.
Hakika Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuadhibu, na bila ya shaka ni Mwenye
maghfira, na Mwenye kurehemu.167

168. Na tuliwafarikisha katika ardhi makundi makundi.
Wako kati yao walio wema, na wengine kinyume cha hivyo. Na tukawajaribu kwa mema
na mabaya ili wapate kurejea.168

169. Na wakafuatia baada yao kizazi kibaya walio rithi
Kitabu. Wakashika anasa za haya maisha duni, na wakasema: Tutasamehewa! Na
ikiwajia tena anasa kama hiyo wataishika pia. Je, hawakufanyiwa agano la Kitabu
kuwa wasiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila Haki tu? Nao wamekwisha soma yaliomo
humo. Na nyumba ya Akhera ni bora kwa wanao jikinga na maasi. Basi je, hamtii
akilini?169

170. Na wale wanao kishikilia Kitabu, na wakashika Sala
- hakika Sisi hatupotezi ujira wa watendao mema.170

171. Na pale tulipo unyanyua mlima juu yao ukawa kama
kwamba ni kiwingu kilicho wafunika, na wakadhani kuwa utawaangukia,
(tukawaambia): Kamateni kwa nguvu tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani
yake ili mpate kumcha Mungu.171

172. Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika
wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi
zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia.
Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.172

173. Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha
kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu
ya waliyo yafanya wapotovu?173

174. Ndio kama hivyo tunavyo zipambanua Ishara, kwa
kutaraji kuwa watarejea.174

175. Na wasomee khabari za yule ambaye tulimpa Ishara
zetu, naye akajivua nazo. Na Shet'ani akamuandama, akawa miongoni walio potea. 175

176. Na tungelitaka tungeli mtukuza kwa hizo Ishara,
lakini yeye aliushikilia ulimwengu na akafuata pumbao lake. Basi mfano wake ni
mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi na ukimwacha pia hupumua na
kutoa ulimi. Huo ni mfano wa kaumu wanao zikanusha Ishara zetu. Basi simulia
hadithi, huenda wakatafakari.176

177. Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanao kanusha
Ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao. .177

178. Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanao kanusha
Ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao.178

179. Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana
nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana
masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu
zaidi. Hao ndio walio ghafilika. 179

180. Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi
muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanao haribu utakatifu wa majina yake. Hao
watakuja lipwa waliyo kuwa wakiyatenda.180

181. Na katika tulio waumba wako watu wanao ongoza kwa
Haki, na kwayo wanafanya uadilifu.181

182. Na wale walio kadhibisha Ishara zetu, tutawapururia
pole pole kwa namna ambayo wenyewe hawaijui182

183. Nami nitawapa muda. Hakika mpango wangu ni
madhubuti. 183

184. Je, hawafikiri? Huyu mwenzao hana wazimu. Hakuwa
yeye ila ni mwonyaji aliye dhaahiri.184

185. Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi, na vitu
alivyo viumba Mwenyezi Mungu, na pengine ajali yao imekwisha karibia? Basi
maneno gani baada ya haya watayaamini? 185

186. Aliye mwacha Mwenyezi Mungu kupotea hana wa
kumwongoa. Atawaacha hao wakitangatanga katika upotofu wao. 186

187.
Wanakuuliza hiyo Saa (ya mwisho) itakuwa lini?
Sema: Kuijua kwake kuko kwa Mola Mlezi wangu. Haidhihirishi hiyo kwa wakati wake
ila Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haikujiini ila kwa ghafla tu.
Wanakuuliza kama kwamba wewe una pupa ya kuijua. Sema: Ujuzi wake uko kwa
Mwenyezi Mungu. Lakini aghlabu ya watu hawajui.187

188. Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara,
ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ninge jizidishia
mema mengi, wala ovu lisinge nigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na
mbashiri kwa watu wanao amini.188

189. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika nafsi moja; na
katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu. Na anapo
muingilia hubeba mzigo mwepesi, akitembea nao. Anapo kuwa mja mzito, wote wawili
humwomba Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wao: Kama ukitupa mwana mwema tutakuwa
katika wanao shukuru.189

190. Basi anapo wapa mwana mwema, wanamfanyia
washirikina Mwenyezi Mungu katika kile kile alicho wapa. Mwenyezi Mungu
ametukuka na huko kushirikisha kwao190

191. Ati wanawafanya viumbe kuwa ni washirika wa
Mwenyezi Mungu, nao hawaumbi, bali wao ndio wanaumbwa?191

192. Wala hawana uwezo wa kuwanusuru wala wenyewe
hawajinusuru. 192

193. Na mkiwaita kwenye uwongofu, hawakufuateni. Ni
mamoja kwenu ikiwa mtawaita au mkinyamaza.193

194.
Hakika hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu ni
waja mfano wenu nyinyi. Hebu waombeni, nao wakuitikieni, kama mnasema kweli. 194

195. Je, wao wanayo miguu ya kwendea? Au wanayo mikono
ya kutetea? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikizia? Sema:
Iiteni hio miungu yenu ya ushirikina. Kisha nifanyieni mimi vitimbi, wala
msinipe muhula.195

196.
Hakika Mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu aliye
teremsha Kitabu. Naye ndiye awalindae walio wema. 196

197. Na hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi hawawezi
kukunusuruni, wala hawajinusuru wenyewe.197

198. Na mkiwaita kwenye uwongofu hawasikii. Na unawaona
wanakutazama, nao hawaoni.198

199.
Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge
na majaahili. 199

200. 200

201. Na uchochezi wa Shet'ani ukikuchochea basi omba
ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Msikizi, Mjuzi.201

202. Na ndugu zao wanawavutia kwenye upotofu, kisha wao
hawaachi. 202

203. Na usipo waletea Ishara waitakayo husema: Kwa nini
hukuibuni? Sema: mimi ninafuata yanayo funuliwa kwangu kutokana na Mola Mlezi
wangu. Hii (Qur'ani) ni hoja zinazo toka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu na
rehema kwa watu wanao amini.203

204. Na isomwapo Qur'ani isikilizeni na mnyamaze ili
mpate kurehemewa. 204

205. Na mkumbuke Mola Mlezi wako nafsini kwako kwa
unyenyekevu na khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni. Wala
usiwe miongoni wa walio ghafilika.205

206.
Hakika wale walioko kwa Mola wako Mlezi hawajivuni
wakaacha kumuabdu, na wanamtakasa na wanamsujudia206
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa una ushauri au maoni juu ya tarjuma
hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al
Barwani