Tarjuma ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye
amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo. 1

2. Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake,
na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri. 1

3. Wakae humo milele. 3

4. Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana.
4

5. Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni
neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu. 5

6. Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao,
kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya! 6

7. Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni
pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi.
7

8. Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi
kuwa kama nchi ilio pigwa na ukame. 8

9. Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na
Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu? 9

10. Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema:
Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo
letu. 10

11.
Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa
muda wa miaka kadhaa wa kadhaa. 11

12. Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi
mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa. 12

13. Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika
wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha
uwongofu. 13

14. Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na
wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita
mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la
kuvuka mpaka. 14

15. Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake
Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye
dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu? 15

16. Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya
Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema
yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu. 16

17. Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani
mwao kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo
katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi
Mungu anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi
hutampatia mlinzi wala mwongozi. 17

18. Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi
tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele
kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe
umejaa khofu. 18

19. Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate
kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema:
Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda
mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame
chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo
hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote. 19

20. Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au
watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa! 20

21. Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua
ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo
kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola
wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka
tutawajengea msikiti juu yao. 21

22.
Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao.
Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na
wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi
ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane
juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa
yeyote yule. 22

23. Wala usisema kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika
nitalifanya hilo kesho 23

24. Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke
Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa
kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu. 24

25. Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na
wakazidisha tisa. 25

26. Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa.
Ni zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana
mlinzi isipo kuwa Yeye, wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake. 26

27. Na soma uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako
Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo
kuwa kwake. 27

28. Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba
Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho
yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye
mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita
mpaka. 28

29. Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi.
Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye
kudhulumu Moto ambao utawazunguka kama khema. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa
kupewa maji kama mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua nyuso zao. Kinywaji hicho
ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno! 29

30. Hakika wale walio amini na wakatenda mema - hakika
Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda mema. 30

31. Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito
kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za
kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo
bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia! 31

32. Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa
vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia
mimea ya nafaka. 32

33. Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala
hapana kitu katika hayo kilicho tindikia. Na ndani yake tukapasua mito.
33

34. Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia
mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu!
34

35. Na akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu
nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika. 35

36. Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kyama) itatokea. Na
ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora
zaidi kuliko haya. 36

37. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je!
Unamkufuru aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii,
kisha akakufanya mtu kaamili? 37

38. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi.
Wala simshirikishi na yeyote. 38

39. Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema:
Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.
Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, 39

40. Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora
kuliko kitalu chako, naye akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho
chako, na kikageuka ardhi tupu inayo teleza. 40

41. Au maji yake yakadidimia wala usiweze kuyagundua.
41

42.
Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua
pindua viganja vyake, kwa vile alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya
chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingeli mshiriki Mola wangu Mlezi na yeyote!
42

43. Wala hakuwa nacho kikundi cha kumsaidia badala ya
Mwenyezi Mungu, wala mwenyewe hakuweza kujisaidia. 43

44. Huko ulinzi ni wa Mwenyezi Mungu wa Haki tu. Yeye
ndiye mbora wa malipo, na mbora wa matokeo. 44

45. Na wapigie mfano wa maisha ya dunia. Hayo ni kama
maji tunayo yateremsha kutoka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha
hiyo mimea ikawa vibuwa vinavyo peperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
uweza juu ya kila kitu. 45

46. Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema
yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini.
46

47. Na siku tutapo iondoa milima na ukaiona ardhi
iwazi, na tukawafufua - wala hatutamwacha hata mmoja kati yao 47

48. Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa
safu (wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai
kwamba hatutakuwekeeni miadi. 48

49. Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo
ogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini!
Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda
yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote. 49

50. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam!
Walimsjudia isipo kuwa Iblisi. Yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja
amri ya Mola wake Mlezi. Je! Mnamshika yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala
yangu, hali wao ni adui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.
50

51.
Sikuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wala
kuumbwa kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni wasaidizi. 51

52. Na siku atakapo sema (Mwenyezi Mungu): Waiteni hao
mlio dai kuwa ni washirika wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi
tutaweka baina yao maangamio. 52

53. Na wakhalifu watauona Moto na watajua ya kwamba wao
lazima wataingia humo; wala hawatapata pa kuuepuka. 53

54. Na bila ya shaka tumewaelezea watu katika hii
Qur'ani kila namna ya mfano. Lakini mwanaadamu amezidi kuliko kila kitu kwa
ubishi. 54

55. Na hapana kilicho wazuia watu kuamini ulipo wajia
uwongofu na wakaomba maghfira kwa Mola wao Mlezi, isipo kuwa yawafikie ya wale
wa zamani, au iwafikie adhabu jahara. 55

56. Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na
waonyaji. Na walio kufuru wanabishana kwa uwongo, ili kwa uwongo huo waivunje
kweli. Na wanazifanya Ishara zangu na yale waliyo onywa kuwa ni mzaha. 56

57. Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye
kumbushwa Ishara za Mola wake Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyo
tangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili
wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao. Na ukiwaita kwenye uwongofu hawakubali
kabisa kuongoka. 57

58. Na Mola wako Mlezi ni Msamehevu Mwenye rehema. Lau
angeli wachukulia kwa mujibu waliyo yachuma, bila ya shaka angeli wafanyia
haraka kuwaadhibu. Lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya
kuepukana nayo. 58

59. Na miji hiyo tuliwaangamiza watu wake walipo
dhulumu. Na tukawawekea miadi ya maangamizo yao. 59

60. Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha
kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda
mrefu. 60

61. Basi wawili hao walipo fika zinapo kutana hizo
bahari mbili walimsahau samaki wao, naye akashika njia yake kaporonyokea
baharini. 61

62. Walipo kwisha pita alimwambia kijana wake: Tupe
chakula chetu cha mchana. Kwa hakika tumepata machofu kweli kwa hii safari yetu.
62

63. Akasema (kijana): Waona! Pale tulipo pumzika penye
jabali basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha
nisimkumbuke ila Shet'ani tu. Naye akashika njia yake baharini kwa ajabu.
63

64. (Musa) akasema: Hayo ndiyo tuliyo kuwa tunayataka.
Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia waliyo jia. 64

65. Basi wakamkuta mja katika waja wangu tuliye mpa
rehema kutoka kwetu, na tukamfunza mafunzo yaliyo toka kwetu. 65

66. Musa akamwambia: Nikufuate ili unifunze katika ule
uwongofu ulio funzwa wewe? 66

67. Akasema: Hakika wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja
nami. 67

68. Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo
undani wake? 68

69. Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda,
utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako. 69

70. Akasema: Basi ukinifuata usiniulize kitu mpaka mimi
nianze kukutajia. 70

71. Basi wawili hao wakatoka, hata walipo panda jahazi
(yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Unaitoboa uwazamishe watu wake? Hakika
umefanya jambo baya. 71

72. Akasema: Sikukwambia hutaweza kuvumilia kuwa pamoja
nami? 72

73. (Musa) akasema: Usinichukulie kwa niliyo sahau,
wala usinipe uzito kwa jambo langu. 73

74. Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana,
akamuuwa. (Musa) akasema: Ala! Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama
hakika umefanya jambo baya kabisa! 74

75. AKASEMA: Je! Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi
kuvumilia kuwa pamoja nami? 75

76. Akasema: Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya
usifuatane nami, kwani umekwisha pata udhuru kwangu. 76

77. Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja.
Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta
ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli
taka ungeli chukua ujira kwa haya. 77

78. (Yule mtu) akasema: Huku ndio kufarikiana baina
yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia.
78

79. Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu
wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme
anaghusubu majahazi yote. 79

80. Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni
Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri. 80

81. Basi tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye
bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma.
81

82. Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili
mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni
mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina
yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda
hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza
kuyasubiria. 82

83. Na wanakuuliza khabari za Dhul- Qarnaini. Waambie:
Nitakusimulieni baadhi ya hadithi yake. 83

84. Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia
za kila kitu. 84

85. Basi akaifuata njia. 85

86. Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika
checmchem yenye matope meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe
Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema. 86

87. Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na
kisha atarudishwa kwa Mola wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana.
87

88. Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata
malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu. 88

89. Kisha akaifuata njia. 89

90. Hata alipo fika matokeo ya jua aliliona
linawachomozea watu tusio wawekea pazia la kuwakinga nalo. 90

91. Ndio hivyo hivyo. Na Sisi tulizijua vilivyo khabari
zake zote. 91

92. Kisha akaifuata njia. 92

93. Hata alipo fika baina ya milima miwili, alikuta
nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wanafahamu lolote. 93

94.
Wakasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Hakika Juju-wa-maajuju
wanafanya uharibifu katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina
yetu na wao ngome? 94

95. Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora
zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina
yenu na wao. 95

96.
Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza
nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya
(chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie. 96

97. Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa.
97

98. Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu
Mlezi. Na itapo fika ahadi ya Mola wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola
wangu Mlezi ni kweli tu. 98

99. Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao. Na
baragumu litapulizwa, na wote watakusanywa pamoja. 99

100. Na siku hiyo tutawadhihirishia wazi Jahannamu
makafiri waione. 100

101. Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa paziani
hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia. 101

102. Je, wanadhani walio kufuru ndio wawafanye waja
wangu ndio walinzi wao badala yangu Mimi? Hakika Sisi tumeiandaa Jahannamu iwe
ndipo mahala pa kuteremkia makafiri. 102

103. Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika
vitendo vyao? 103

104. Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia
imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri. 104

105. Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao
Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya
Kiyama hatutawathamini kitu. 105

106. Hiyo Jahannamu ni malipo yao kwa walivyo kufuru na
wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume wangu. 106

107.
Hakika wale walio amini na wakatenda mema mashukio
yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi. 107

108.
Watadumu humo; hawatataka kuondoka. 108

109. Sema: Lau kuwa bahari ndio wino kwa maneno ya Mola
wangu Mlezi, basi bahari ingeli malizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola
wangu Mlezi, hata tungeli ileta mfano wa hiyo kuongezea. 109

110. Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa
Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake
Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya
Mola wake Mlezi. 110
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright � 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani