Tarjuma
ya Quran Tukufu kwa kiswahili

KWA JINA LA
MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU 0

1. HAKIKA wamefanikiwa Waumini, 1

2. Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao, 2

3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi, 3

4. Na ambao wanatoa Zaka, 4

5. Na ambao wanazilinda tupu zao, 5

6. Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono
yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. 6

7. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio
warukao mipaka. 7

8. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
8

9. Na ambao Sala zao wanazihifadhi 9

10. Hao ndio warithi, 10

11.
Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo.
11

12. Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya
udongo. 12

13.
Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika
kalio madhubuti. 13

14.
Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na
tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa,
na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka
Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji. 14

15.
Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa.
15

16.
Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa.
16

17. Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi
hatukuwa wenye kughafilika na viumbe. 17

18. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na
tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa. 18

19. Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na
mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula; 19

20. Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta
na kuwa kitoweo kwa walao. 20

21. Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa
- tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika
hao manufaa mengi, na pia mnawala. 21

22. Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa. 22

23. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema:
Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye.
Basi je! Hamwogopi? 23

24.
Walisema wale wakuu walio kufuru katika watu wake:
Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na
lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika.
Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani. 24

25. Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi
mngojeeni tu kwa muda. 25

26.
Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa
wamenikanusha. 26

27.
Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na
uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize
ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye
katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu.
Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. 27

28. Basi utakapo tulia wewe na walio pamoja nawe humo
marikebuni, sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliye
tuokoa na watu madhaalimu! 28

29. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho
wenye baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji. 29

30.
Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini
Sisi ni wenye kuwafanyia mtihani. 30

31.
Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kuwaambia:
Muabuduni Mwenyezi Mungu! Hamna mungu asiye kuwa Yeye. Jee, hamwogopi? 31

32. Na wakubwa katika watu wake walio kufuru na
wakakanusha mkutano wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya
dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binaadamu kama nyinyi; anakula mlacho,
na anakunywa mnywacho. 32

33. Na nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika
mtakuwa khasarani. 33

34.
Hivyo anakuahidini ati ya kwamba mtakapo kufa na
mkawa udongo na mifupa kuwa mtatolewa? 34

35.
Hayawi! Hayawi hayo mnayo ahidiwa. 35

36.
Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na
kuishi basi. Wala sisi hatutafufuliwa. 36

37. Huyu si lolote ila ni mtu anaye mzulia Mwenyezi
Mungu uwongo, wala sisi sio wa kumuamini. 37

38.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa sababu
wananikanusha. 38

39.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache
watakuwa wenye kujuta. 39

40. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya
kama takataka zinazo elea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu!
40

41.
Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine. 41

42.
Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine. 42

43.
Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala
kuikawiza. 43

44.
Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja.
Kila umma alipo wafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya
hawa, na tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Wakapotelea mbali watu wasio
amini. 44

45.
Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na
ishara zetu na hoja zilizo wazi. 45

46.
Kumwendea Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna,
nao walikuwa watu majeuri. 46

47.
Wakasema: Je, tuwaamini wanaadamu wawili hawa kama
sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu? 47

48. Basi wakawakanusha, na wakawa miongoni mwa walio
angamizwa. 48

49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
49

50. Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni
Ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipo inuka penye utulivu na
chemchem za maji. 50

51. Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema.
Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda. 51

52. Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi
ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi. 52

53.
Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali.
Kila kundi likifurahia kwa waliyo nayo. 53

54. Basi waache katika ghafla yao kwa muda. 54

55. Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyo wapa mali na
watoto 55

56. Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe
hawatambui. 56

57. Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi
wananyenyekea, 57

58. Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini,
58

59. Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi,
59

60. Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo
zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi, 60

61. Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya
kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia. 61

62. Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo
wake. Na tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa. 62

63.
Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo
vitendo vinginevyo wanavyo vifanya. 63

64. Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio
dekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapo yayatika. 64

65.
Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
65

66.
Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi
nyuma juu ya visigino vyenu, 66

67. Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani)
kwa dharau. 67

68. Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo
wafikia baba zao wa zamani? 68

69. Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?
69

70. Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na
wengi wao wanaichukia Haki. 70

71. Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi
zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho
wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao. 71

72. Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi
ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanao ruzuku. 72

73. Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo
Nyooka. 73

74. Na hakika wale wasio iamini Akhera wanajitenga na
Njia hiyo. 74

75. Na lau tungeli warehemu na tukawaondolea shida
waliyo nayo bila ya shaka wangeli endelea katika upotofu wao vile vile,
wakitangatanga. 75

76. Na hakika tuliwatia adhabu kali; lakini
hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala hawakunyenyekea. 76

77.
Mpaka tulipo wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo
ndipo wakawa wenye kukata tamaa. 77

78. Na Yeye ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na
nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu. 78

79. Na Yeye ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na
kwake Yeye mtakusanywa. 79

80. Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye
mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu? 80

81. Bali wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza.
81

82.
Walisema: Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa
ndio tutafufuliwa? 82

83.
Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa
haya ila ni visa vya uwongo vya watu wa zamani. 83

84.
Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama
nyinyi mnajua? 84

85.
Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je,
hamkumbuki? 85

86.
Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola
Mlezi wa A'rshi Kuu? 86

87.
Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je,
hamwogopi? 87

88.
Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila
kitu, naye ndiye anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua?
88

89.
Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema:
Basi vipi mnadanganyika? 89

90. Bali tumewaletea Haki, na kwa yakini hao ni waongo.
90

91.
Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hanaye mungu
mwengine. Inge kuwa hivyo basi kila mungu angeli chukua alivyo umba, na baadhi
yao wangeli washinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazo msifu.
91

92.
Mjuzi wa siri na dhaahiri, na ametukuka juu ya hayo
wanayo mshirikisha nayo. 92

93.
Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha adhabu waliyo
ahidiwa, 93

94. Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu
madhaalimu hao. 94

95. Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyeshsa tuliyo
waahidi. 95

96.
Kinga maovu kwa kutenda yaliyo mema zaidi. Sisi
tunajua wayasemayo. 96

97. Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na
wasiwasi wa mashet'ani. 97

98. Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi,
wasinikaribie. 98

99.
Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola
wangu Mlezi! Nirudishe. 99

100.
Ili nitende mema sasa
badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao
kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa. 100

101.
Basi litapo pulizwa
baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana.
101

102.
Ama wale ambao mizani zao
zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa. 102

103.
Na wale ambao mizani zao
zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu
watadumu. 103

104.
Moto utababua nyuso zao,
nao watakuwa na nyuso zilizo kunjana. 104

105.
Je! Hazikuwa Aya zangu
mkisomewa, na nyinyi mkizikanusha? 105

106.
Mola wetu Mlezi!
Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio potea. 106

107.
Mola wetu Mlezi! Tutoe
humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli sisi ni wenye kudhulumu. 107

108.
Atasema Mwenyezi Mungu:
Tokomeeni humo, wala msinisemeze. 108

109.
Bila ya shaka lilikuwapo
kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na
uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanao rehemu. 109

110.
Lakini nyinyi mliwakejeli
hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka. 110

111.
Hakika Mimi leo nimewalipa
kwa vile walivyo subiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu. 111

112.
Atasema: Mlikaa muda gani
katika ardhi kwa hisabu ya miaka? 112

113.
Watasema: Tulikaa siku
moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu. 113

114.
Atasema: Nyinyi hamkukaa
huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua. 114

115.
Je! Mlidhani ya kwamba
tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? 115

116.
Ametukuka Mwenyezi Mungu,
Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu. 116

117.
Na anaye muomba - pamoja
na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka
hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi. 117

118.
Nawe sema: Mola wangu
Mlezi! Samehe na urehemu nawe ni Mbora wa wanao rehemu. 118
Imetarjumiwa na Sheikh Ali Muhsin
Al-Barwani
Ikiwa
una ushauri au maoni juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com
Copyright © 22 August 1997, Sheikh
Ali Muhsin Al Barwani