(e) Njia ya Maandishi:
Njia nyingine anayoitumia Allah (s.w) katika kuwasiliana na waja wake ni njia ya maandishi, yaani maandishi yaliyoandikwa tayari.
Nabii Mussa (a.s) aliletewa ujumbe kutoka kwa Allah (s.w) kwa maandishi yaliyoandikwa tayari katika mbao kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo: “Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha (ya kila namna) na maelezo ya kila jambo.
Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako wayashike vema haya…” (7:145) “Na Musa zilipotulia ghadhabu zake, aliziokota zile mbao.
Na katika maandiko yake (hizo mbao) ulikuwamo uwongofu na rehema kwa wale wanaomuogopa Mola wao”. (7:154). Kwa ujumla tumeona kuwa chanzo cha elimu ni “Allah (s.w). Lolote tunalolifahamu tumefunzwa na Allah kwa njia mojawapo katika njia tano tulizoziona.