Amri ya Kumfuata Mtume (s.a.w)
Sema, "Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni, (hapo) Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakughufirieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye maghufira (na) mwenye rehema." (3:31) "Na anachokupeni Mtume basi pokeeni na anachokukatazeni jiepusheni nacho". (57:7)

Amri ya Kumfanya Mtume (s.a.w) Kiigizo "Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana." (33:21) Kutomfuata Mtume (s.a.w) ni Uasi Na anayemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kuiruka mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamwingiza Motoni, humo atakaa milele, na atapata adhabu zifedheheshazo. (4:14)

Siku hiyo wale waliokufuru na kumwasi Mtume watatamani ardhi isawazishwe juu yao (yaani lau kuwa wamefukiwa tu kaburini bila ya kufufuliwa). Wala hawataweza kumficha Allah Hadith yo yote (katika ammbo waliyoyafanya). (4:42) “Je, hawajui ya kwamba anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwa yeye atapata moto wa Jahannam kukaa humo daima? Hiyo ndiyo hizaya kubwa." (9:63)  “… Na watakao muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi bila shaka watapata moto wa Jahanam, wakae humo milele." (72:23)

Aya hizi zote kwa ujumla zinatuonyesha wazi kuwa kufuata sunnah, ya Mtume (s.w) si jambo la hiari kwa Muislamu. Hivyo ule uoni walionao baadhi ya Waislamu kuwa sunnah ni jambo la hiari, ukilifanya unapata thawabu na ukiliacha hupati dhambi ni uoni potofu kama tutaizingatia pia aya ifuatayo: "Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika wamepotea upotofu ulio wazi (kabisa). (33:36)