Nafasi ya Sunnah katika Uislamu
Mtume Muhammad (s.a.w) kama ilivyokuwa kwa Mitume waliomtangulia, alikuwa ni mjumbe wa Allah (s.w) aliyeteuliwa ili aufundishe Uislamu na kuusimamisha katika jamii, yeye mwenyewe akiwa ni kiigizo chema. Hivyo ili watu waweze kuufahamu Uislamu vilivyo na kuweza kuusimamisha katika jamii hawana budi, pamoja na kuisoma Qur-an kwa mazingatio, kumfuata Mtume, kumtii na kumfanya kuwa kiigizo chao kitabia na kimwenendo. Qur-an inasisitiza jambo hili katika aya nyingi na baadhi ya hizo ni hizi zifuatazo:

Amri ya Kumtii Mtume (s.a.w)
Utii kwa Allah (sw) umesisitizwa sambamba na utii kwa Mtume (s.a.w) kama tunavyojfinza katika aya zifuatazo: “Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa." (3:132)  “Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu nyenu, walio katika nyie (Waislamu wenzenu). Na kama mkikhitalifiana juu ya jambo lo lote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Hiyo ndiyo kheri, nayo ina matokeo bora kabisa." (4:59) Na mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na tahadharini (na kukhalifu amri zao). Na mkikengeuka basi jueni ya kwamba juu ya Mtume wetu ni kufikisha tu (ujumbe) waziwazi. (Na akishafikisha hana lawama; lawama juu yenu). (5:92) ................Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni katika wanaoamini (kweli). (8:1)

“Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye na hali mnasikia." (8:20) Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume, na kama mkikengeuka, basi ni juu yake huo (mzigo) aliotwika; (kazi aliyopewa kufikisha ujumbe). Na juu yenu (huo mzigo) mliotwikwa (kutii). Na mkimtii mtaongoka; hapana juu ya Mtume ila kufikisha (ujumbe wake) wazi wazi. (24:54) Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu. ( 47:33) Na mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume. Mkipuuza (hapana lawama juu yake). Juu ya Mtume wetu ni kufikisha tu kuliko wazi wazi. (Naye amekwisha kukufikishieni). (64:12)

Amri ya Kumfuata Mtume (s.a.w)
Sema, "Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni, (hapo) Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakughufirieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye maghufira (na) mwenye rehema." (3:31) "Na anachokupeni Mtume basi pokeeni na anachokukatazeni jiepusheni nacho". (57:7) Amri ya Kumfanya Mtume (s.a.w) Kiigizo "Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana." (33:21) Kutomfuata Mtume (s.a.w) ni Uasi Na anayemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na kuiruka mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamwingiza Motoni, humo atakaa milele, na atapata adhabu zifedheheshazo. (4:14)

Siku hiyo wale waliokufuru na kumwasi Mtume watatamani ardhi isawazishwe juu yao (yaani lau kuwa wamefukiwa tu kaburini bila ya kufufuliwa). Wala hawataweza kumficha Allah Hadith yo yote (katika ammbo waliyoyafanya). (4:42) “Je, hawajui ya kwamba anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwa yeye atapata moto wa Jahannam kukaa humo daima? Hiyo ndiyo hizaya kubwa." (9:63)  “… Na watakao muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi bila shaka watapata moto wa Jahanam, wakae humo milele." (72:23)

Aya hizi zote kwa ujumla zinatuonyesha wazi kuwa kufuata sunnah, ya Mtume (s.w) si jambo la hiari kwa Muislamu. Hivyo ule uoni walionao baadhi ya Waislamu kuwa sunnah ni jambo la hiari, ukilifanya unapata thawabu na ukiliacha hupati dhambi ni uoni potofu kama tutaizingatia pia aya ifuatayo: "Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika wamepotea upotofu ulio wazi (kabisa). (33:36)